24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

UVUVI HARAMU WATISHIA MANISPAA KINONDONI

NA HARRIETH MANDARI


TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazofaidika na biashara ya uvuvi licha ya changamoto mbalimbali zinazoikumba ikiwemo ya uvuvi haramu  wa kutumia nyavu ndogo, maabomu na fataki au baruti, ambapo kwa  kiasi kikubwa uvuvi huo unachangia kuwepo kwa uhaba wa samaki.

Imeelezwa kuwa kila siku milipuko 50 imekuwa ikisikika katika ukanda wa fukwe za Manispaa ya Kinondoni, hali inayohatarisha kutoweka samaki wote katika ukanda huo kwa kukosa mazalio ya samaki.

Serikali imeanza kupanga mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inakomesha uvuvi huo haramu katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kushirikisha vyombo vya dola kufanya doria katika sehemu  mbalimbali za bahari na kuwachukulia hatua wale wote wanaovua samaki kwa uvuvi huo haramu.

Uvuvi haramu una athari kubwa kwa mazalia ya samaki na kwa watu kwa ujumla, kwani asilimia 40 ya eneo la bahari limeharibiwa na wavuvi haramu na kama hakutakuwepo na uthubutu wa kukomesha uvuvi huo, inaonesha  ifikapo mwaka 2020 -2025 hakutakuwa na mazalia yoyote.

Aina hii ya uvuvi imetajwa kuwa ni miongoni mwa mambo ambayo yanachangia kwa asilimia kubwa madhara ya kuharibu mazalia ya samaki na kusababisha samaki wakubwa  kutoweka na kwenda ukanda mwingine wa bahari.

Katika kuhakikisha vita hiyo ya uvuvi haramu inafanikiwa nchini, Wilaya ya Kinondoni imeanza kuweka mikakati ya kuwadhibiti na kuwafikisha katika vyombo vya dola wavuvi wote wanaotumia uvuvi huo haramu katika maeneo ya Kunduchi, Msasani, Ununio, Kawe Beach, Mbezi Beach na Mbweni .

Katika kutekeleza azma ya Serikali ya kutokomeza matumizi ya zana haramu za uvuvi ambazo zimepigwa marufuku na Serikali, Mkuu  wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, anasema uvuvi haramu ni lazima upigwe vita kutokana na wavuvi hao kutumia nyavu zenye matundu madogo na kuvua  samaki kwa kutumia mabomu kuyalipua  matumbawe baharini kwa lengo la kujipatia samaki.

Anasema uvuvi huo umekuwa ukiathiri kwa kiasi kikubwa si tu huharibu mazingira, bali  huua samaki hasa wadogowadogo na kusababisha mazalia kuharibika na kutozalisha tena samaki kutokana na milipuko kuharibu  makazi  yao. Nyavu za matundu madogo  hukomba vichanga  na hivyo  mbinu inayotumika kuvulia samaki si sahihi na kufanya samaki kupotea na kupunguza uzalishaji kwenye sekta ya uvuvi.

Hapi anasema katika wilaya yake ameanza kuchukua hatua mbalimbali ya kukabiliana na wavuvi hao ikiwemo ya kukabidhi majina 21 ya wavuvi haramu wawili wakiwa viongozi kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda.

Anasema pia ameteketeza zana haramu za uvuvi  zenye thamani ya Sh millioni 60 kwa lengo la kuzindua rasmi vita hivyo dhidi ya kupambana na uvuvi haramu katika wilaya yake na kutoa agizo kwa mvuvi yeyote atakayekutwa anafanya shughuli hiyo achukuliwe hatua.

"Sheria ya uvuvi inatamka wazi aina ya uvuvi na vipimo vya nyavu zinazotakiwa katika kuvulia samaki, hivyo ni wajibu wa kila mtu kuzingatia sheria zilizopo kwani watu wanapotumia mabomu au nyavu zisizokuwa na kiwango zinahatarisha  mazalia ya samaki kuendelea kuzaliana," anasema  Hapi.

Aidha, anasema utumiaji wa zana hizo haramu una madhara mengi kwa watumiaji wenyewe ikiwemo wavuaji samaki  kupata ulemavu wa viungo vya mwili na wakati mwingine kupoteza maisha kutokana na milipuko ya mabomu wanayolipua.

Naye Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Kinondoni, Grace Kakama, akitoa ripoti juu ya zana za uvuvi haramu Pwani ya Manispaa ya Kinondoni hivi karibuni, anasema katika kupambana na vitendo vya uvuvi haramu katika ukanda wa pwani ya manispaa hiyo, jitihada kadhaa zimekuwa zikifanyika ikiwemo kufanya doria za mara kwa mara katika nchi kavu, mialo ya samaki na baharini na  kufanikiwa kukamata nyavu haramu zenye macho madogo aina ya kokoro  zipatazo 57 na zenye wastani wa urefu usiopungua mita 10 kwa kila nyavu.

Anasema  nyavu aina ya monofilament (ghost fishing gear) zipatazo 20 zilikamatwa ambapo nyavu  hizo kwa pamoja zina jumla ya  thamani ya Sh milioni 60, pia zana haramu aina ya mikuki ipatayo 30 ilikamatwa yenye  thamani ya Sh 250,000 ambapo aina  zote za zana haramu zimekamatwa katika nyakati tofauti kuanzia Septemba mwaka jana.

 

"Zana hizo haramu zimekamatwa katika mialo sita ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani ya Manispaa ya Kinondoni, ikiwemo Kunduchi, Msasani, Ununio, Kawe Beach, Mbezi Beach na Mbweni  ambapo takribani asilimia 80 ya nyavu haramu zilikamatwa katika mwalo wa Kunduchi na  Kawe," anasema Grace.

Anasema mapema mwezi huu, walifanikiwa kuwakamata wavuvi haramu saba  wakiwemo wavuvi wawili  wanaovua kwa kutumia  baruti ambapo walifikishwa kituo cha polisi Kawe kwa hatua zaidi  za kisheria.

"Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanyika kudhibiti wavuvi haramu, wapo wavuvi  wenye nia mbaya wamekuwa wakifanya vitendo vya kuathiri mazalia, makuzi na malisho ya samaki na viumbe wengine wa baharini, hivyo kutishia upatikanaji wa samaki, ukosefu wa ajira kwa jamii ya wavuvi .

“Upungufu wa chakula hutokea kwani  samaki ni kitoweo kizuri  na hivyo mazingira yakiharibiwa samaki hawatapatikana," alisema Grace.

Akaongeza kuwa ulipuaji wa baruti katika uvuvi ni tishio kubwa kwa ukanda wa pwani kwani miamba au matumbawe yanayolipuliwa ni kinga dhidi ya kasi kubwa ya mawimbi ya bahari ili yasiweze kuidhuru pwani, hivyo jitihada zaidi zinahitajika kudhibiti ulipuaji huo wa mabomu .

"Tunaomba suala hili la kupambana na uvuvi haramu liendelee kupewa kipaumbele hasa utumiaji wa baruti katika kuvua, tunaomba viongozi kuwa mstari wa mbele kuweka juhudi katika kupambana na vita dhidi ya uvuvi haramu wa baruti kwani hii ni aina  ya uharamia ambayo nguvu ya vyombo vya dola inahitajika sana kuwabaini wanaotengeneza, wanaosambaza na wanaotumia mabomu katika shughuli za uvuvi," anasema  Grace.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles