30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

SERIKALI HAIJUI HASARA UKOSEFU UMEME WA UHAKIKA

Na JUSTIN DAMIAN


WAKATI Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) likikadiria ukosefu wa umeme wa uhakika, unaikosesha sekta ya viwanda shilingi 31 bilioni kwa mwaka, Serikali imesema haifahamu ni kiasi gani kinapotea kutokana na ukosefu wa umeme wa uhakika.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na CTI juu ya Changamoto za Upatikanaji wa Umeme wa Uhakika Viwandani unasema ukosefu wa umeme umekuwa ni changamoto kubwa katika maendekeo ya viwanda.

Alipoulizwa na gazeti hili kama Serikali inafahamu ni kiasi gani inapoteza kutokana na ukosefu wa umeme wa uhakika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof Justin Ntalikwa alisema Serikali haifamu kiasi kinachopotea

“Hakuna tafiti rasmi kuhusu athari za kutokuwa na umeme wa uhakika ambazo zimesababisha nchi kupoteza kiasi cha fedha kichobainishwa,” alisema

Hata hivyo alisema, Serikali inatambua kwamba kukosekana kwa umeme wa uhakika kunakwamisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii hususan katika sekta za viwanda, biashara na shughuli za kijamii.  Prof Ntalikwa hakusema kwa uhakika lini umeme utakuwa wa uhakika.

“Kukosekana kwa umeme wa uhakika kunaweza kusababisha matatizo ya kupungua kwa mapato ya Serikali kupitia mauzo ya umeme, ukosefu wa ajira,  kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa bidhaa mbali mbali kunakosababisha kupanda kwa gharama za maisha n.k. Ili kuepuka matatizo hayo, Serikali inalazimika kutumia kiasi kikubwa cha rasilimali fedha kutekeleza miradi ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme,” alifafanua

Viwanda ndiyo watumiaji wakubwa wa meme lakini kwa kipindi kirefu sekta hii nyeti imekuwa ikishindwa kutoshelezwa na nishati ya umeme.

Kwa mujibu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mahitaji ya umeme kwa ajili ya viwanda ni zaidi ya asilimia hamsini ya umeme wote unaozalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya taifa.

Taarifa za TANESCO zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha Januari, 2014 mpaka June, 2015 kiasi cha GWh3,920  zilitumika viwandani kati ya  GWh 7,721 zilizozalishwa.

Pamoja na uwezo wa kuzalisha umeme kuongezeka kutoka Megawati 1,226.24 mwezi Aprili, 2015 hadi Megawati 1,461.69 mwezi Aprili, 2016, utafiti uliofanywa na gazeti hili umegundua umeme unaopatika bado si wa uhakika kutokana na kukatika mara kwa mara jambo ambalo limekuwa na athari kwa viwanda.

Ukuwaji wa sekta ya viwanda umeonekana kushuka kutokana na ukosefu wa umeme wa uhakika ulioiathiri sana sekta hiyo kati kati ya mwaka jana (2015), kwa mujibu wa takwimu

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (TBS) katika ripoti yake ya robo tatu ya mwaka inasema shughuli za uzalishaji viwandani ilikua kwa asilimia 3.6 katika robo tatu ya mwaka 2015 ukilinganisha na asilimia 6.3 kwa robo tatu ya mwaka 2014.

Katika kipindi cha Julai mpaka Septemba 2015 uzalishaji viwandani ulishuka kidogo ukilinganisha na mwaka 2014 kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa chakula, vinywaji na uzalishaji katika viwanda vya tumbaku.

Uzalishaji kwenye viwanda vya nguo,madawa na bidhaa za plastiki ulishuka katika kipindi cha robo tatu ya mwaka 2015 ukilinganisha na mwaka 2014,” inasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, uzalishaji wa umeme ulishuka kwa asilimia 1.2 katika robo tatu ya mwaka 2015 ukilinganisha na asilimia 14.2 kwa robo tatu ya mwaka 2014.

Mkurugenzi wa Sera na Ushawishi wa CTI  Hussein Kamote anasema, kushuka kwa ukuaji wa sekta ya viwanda kunatokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika kuanzia katikati ya mwaka jana.

“Ukisoma ripoti ya robo tatu ya mwaka ya NBS utaona uzalishaji wa umeme ulishuka. Kuna uhusiano wa kati ya kushuka huko na uzalishaji wa viwandani,” anasema na kueleza.

Kwa mujibu wa ripoti ya CTI, serikali inapoteza kodi inayofikia shilingi bilioni 9.5 kwa mwaka. Kwa mujibu wa ripoti hiyo jumla ya ajira 7,341 zinapotea kwa mwaka.

Ripoti ya CTI imeshauri TANESCO kugawanywa sehemu mbili. Sehemu ya kwanza  iwe kampuni ya umma itakayohusika na uzalishaji wa umeme pamoja na makampuni mengine binafsi na sehemu ya pili usambazaji ambayo itafanya kazi ya kuhudumia wateja, kuwaunganisha masoko na bili.

Ripoti hiyo imeishauri Serikali kuondoa kodi kwenye vifaa vinavyoingia nchini kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na usambazaji ili kupunguza gharama za umeme kwa kuwa vifaa hivyo vinagharama kubwa na kufanya umeme kuuzwa kwa  gharama kubwa.

Hata hivyo pamoja na jitahada za Serikali kuzalisha umeme kupitia vyanzo mbali mbali, Tanzania bado inanunua umeme kutoka nchi jirani ili kukidhi mahitaji ya wananchi wake walioko pembezoni mwa nchi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umegundua kuwa, Tanzania inanunua umeme kutoka nchi za jirani za Uganda, Kenya na Zambia. Umeme huo husambazwa katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Gridi ya Taifa.

Kutoka Uganda, Tanzania inanunua umeme wa MW 10 na kusambazwa katika maeneo ya Mkoa wa Kagera. Umeme wa MW 5 umeunganishwa kutoka Mbala nchini Zambia na kusambazwa katika Mkoa wa Rukwa.

Tanzania pia umeunganishwa na Kenya kupitia njia ya umeme msongo wa kilovoti 33, ambapo umeme wa MW 1 kutoka Kenya unatumika katika maeneo ya Loliondo mkoani Arusha.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati na Madini, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, uwezo wa mitambo ya kufua umeme (installed capacity) nchini ulikuwa ni MW 1,439.97 ambapo MW 1357.69 ni uwezo wa mitambo iliyounganishwa katika gridi ya Taifa na kiasi cha MW 82.28 ziko nje ya gridi ya Taifa.

Aidha, uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji (hydro)  ni MW 566.79 sawa na asilimia 41.75 ya mitambo yote wakati mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi ni MW 607.00 sawa na asilimia 44.71.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles