30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

KUPATA RISITI HAKI YA MTEJA, AKINYIMWA KOSA LA JINAI

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM


KAMA ilivyo ada kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa tathmini ya makusanyo ya kodi ya kila mwezi, hii ni katika dhana nzima ya kuhakikisha Mamlaka inaendelea kusimamia na kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuongeza mapato ili kuiwezesha nchi kujitegemea yenyewe na ikiwa ni pamoja kuwahudumia wananchi wake.

Kutokana na mikakati mbalimbali ambayo mamlaka imejiwekea, tangu kuanza kwa mwaka wa fedha wa 2016/17, TRA imeshakusanya zaidi ya Sh trilioni nane na kwamba imejipanga kuhakikisha inakusanya mapato ya kutosha hadi kuvuka lengo walilowekewa na Serikali la kukusanya Sh trilioni 15.1.

Baadhi ya mikakati waliyojiwekea ni kuhakikisha mamlaka inaendelea kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi, inafichua wakwepa kodi na kupambana na rushwa, inapanua wigo wa kodi kwa kusajili wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa, maofisa wa TRA kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu, kusimamia kwa karibu matumizi ya mashine za kielektroniki za EFDs na utoaji wa risiti, kufuatilia na kudai malimbikizo ya kodi kutoka kwa wadaiwa sugu, ikiwa ni pamoja na kuendelea na ukaguzi wa kodi kwa wafanyabiashara.

Azma ya kuendelea kuongeza mapato inaweza kutekelezeka kwa kuhakikisha sheria na kanuni mbalimbali za kodi zinafuatwa na kutekelezwa kwa usahihi.

Sheria hizo ni pamoja na ile sheria ya matumizi ya mashine za kutolea risiti za kodi za kielektroniki (EFDs).

Utaratibu wa matumizi ya EFDs ulifanyika katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza iliwahusu wafanyabiashara ambao walisajiliwa kutoza VAT na awamu ya pili iliwahusu wafanyabiashara ambao  hawakusajiliwa na VAT ambao mauzo yao kwa mwaka ni zaidi ya Sh milioni 14.

Katika kuhakikisha inaongeza wigo wa walipa kodi, baada ya Serikali kuiagiza TRA kutoa bure mashine za EFDS kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ambao uwezo wa kununua mashine unaweza kuathiri mitaji yao ya  biashara, mamlaka hiyo imeshatekeleza agizo hilo kwa baadhi ya wafanyabiashara.

 Kwa wafanyabiashara wakubwa hawatahusika na mgao wa mashine hizo bure bali wao wataendelea na utaratibu wa zamani wa kujirejeshea gharama za mashine.

Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata, anasema Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 inamtaka mfanyabiashara kununua, kutumia mashine, kutoa risiti na kulipa kodi.Kwa upande wa mnunuzi kanuni ya kodi ya Ongezeko la Thamani ya 2010, inamtaka mnunuzi wa bidhaa apewe au adai risiti inayotokana na bidhaa iliyonunuliwa.

Anasema pamoja na kuwepo sheria hiyo, changamoto ambayo TRA iliibaini ni kwamba baadhi ya wafanyabiashara hawana mashine na wengine walionazo hawazitumii mashine hizo kutoa risiti pindi wanapofanya mauzo na hivyo kuikosesha Serikali mapato.

Pia mamlaka hiyo ilijidhihirisha kuwa baadhi ya wanunuzi wa bidhaa hawana utamaduni wa kudai risiti kama ushahidi wa kuonyesha mali iliyonunuliwa na ikiwa ni pamoja na ushahidi wa kuonyesha kuwa kodi stahili imelipwa serikalini.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015, kutokutoa risiti za EFD ni kosa ambalo adhabu yake ni faini au kifungo kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Kutokana na hali hiyo, mamlaka inaendelea kuwasisitiza wananchi na wafanyabiashara wote  wanaostahili kulipa kodi kulipa kwa wakati, ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wanaostahili kutumia mashine za kielektroniki kuzitumia kutoa risiti ili Serikali ipate mapato.

Kwa upande wa wananchi nao wametakiwa kuwa wazalendo kwa kudai risiti kwa bidhaa au huduma wanazozipata ili kuhakikisha kodi stahiki inaenda serikalini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles