Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM), umewataka Watanzania kuyapuuza madai ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ya kumtaka Rais Dk. John Magufuli aruhusu mjadala wa Katiba Mpya ili kuachana na vita ya uchumi, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
Hayo yalisemwa juzi na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alipokuwa akizungumza kuhusu kauli ya Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, wakati wa kampeni za udiwani mkoani Arusha pamoja na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuhusu suala la Katiba Mpya ya nchi.
Shaka alisema kinachotamkwa na Lowassa ni mkakati wa majaribu hatari ili kuitia nchi kwenye machafuko, ghasia na fujo kwa nia ya kuitoa Serikali kwenye mwelekeo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015/2020 .
“Tunawapa tahadhari wananchi wasikubali kufuata mkumbo wa siasa za kibabe za Lowassa na Chadema kudai katiba mpya kibabe. Katiba iliyopo ni ya kidemokrasia imeliongoza Taifa kwa miaka 54 ya Uhuru na Muungano,” alisema Shaka
Alisema uzuri wa Katiba iliyopo unafahamika na lowasa pamoja na Chadema kwani hata Lowassa ikiwa mbunge wa Mondoli kwenye Bunge Maalumu la Katiba, alipiga kura ya ndiyo kupinga Mapendekezo ya Rasimu ya Tume ya Jaji Joseph Warioba na kukataa Muungano wa serikali tatu..
Kaimu huyo Katibu Mkuu alisema matatizo ya wananchi ni kupata huduma za afya, maji safi na salama, elimu yenye ubora,ujenzi wa barabara za lami na ajira wala si katiba kwani katiba iliopo inakidhi haja.
“UVCCM tunajua Afrika inajua na dunia inafahamu kasi ya Rais na utendaji wa Serikali yake si ya kawaida katika kuwatumikia wananchi. Jaribio lolote la uharibifu wa amani lazima likabiliwe kwa nguvu zote,” alisema.