Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe.
Umesema suala la kupata misaada kutoka nje lisiwe kipaumbele badala yake vijana wote wajitume kwa ajili yatTaifa lao.
Pia umoja huo umewashukuru vijana wa Mabibo Hosteli kwa kuanzisha harambee ya kuchangia vifaa tiba katika hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Mkoa wa Dar es Salaam na kuungwa mkono na umoja huo.
Msimamo huo umetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alipokabidhi msaada wa vifaa vya kumsaidia mama mjamzito wakati wa kujifungua.
Vifaa vingine vilikuwa ni kwa ajili watoto waliozaliwa chini ya miezi saba, katika Hospital ya Mwananyamala.
Alisema vijana wa CCM ndiyo wenye jukumu na wajibu wa awali wa kubuni, kuanzisha au kuibua masuala katika kuunga mkono na kuchangia maendeleo vijana wengine waige, kufuata na kutekeleza.
Alisema kitendo cha kukabidhi vifaa ni sehemu ya kukamilisha dhana ya maendeleo endelevu kwa nia ya kujenga nchi na kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli na sera za CCM katika ilani ya mwaka 2015-2020.
“Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe kwa ghrama, bei yoyote.
“Natoa wito kwa makundi yote ya vijana, kinamama na makundi mengine kujitokeza na kuunga mkono juhudi za Serikali katika nyanja zote za elimu, afya, kilimo na maeneo mengine kuleta nguvu na msukumo wa kurahisisha maendeleo endelevu,”alisema Shaka.
Alisema wanaposema tukutane kazi, tafsiri yake ina maana pana na mojawapo ni ubunifu, uibuaji mipango , kuchemsha bongo na kushughulika maendeleo ya nchi usiku na mchana kwa vile CCM ndiyo yenye ilani na wao kama vijana ni sehemu ya utekelezaji na usimamizi.