Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umemtaka mwanasiasa mkongwe kingunge nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, kunyamaza kwani yeye ndiye mwasisi wa uasi na usaliti ndani ya chama hicho tawala kabla ya kuamua kujiondoa mwaka 2015.
Akizungumza jana Kaimu Katiba Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema kauli na shutuma zilizotolewa na Mzee Kingunge akiwatuhumu Mwenyekiti mstaafu wa CCM Dk. Jakaya Kikwete , Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akidai wameshiriki uasi na usaliti katika uteuzi wa mgombea urais mwaka 2015.
Shaka alisema wakati umefika kwa Kingunge kukaa kimya, ili aweze kuleta wajukuu pamoja na kutubu kwa Mungu asiyemuamini.
“UVCCM tunajua fika Mzee Kingunge haamini uwepo wa Mungu ndiyo maana anakuwa jasiri na mahiri wa kuongopa , kama ni uasi na usaliti yeye ndiye bingwa wa kuchongea wenzake kwa siasa za majungu, alichochea kufukuzwa kwa Mzee Aboud Jumbe akishirikiana na kina Seif Sharif Hamad, hakuogopa aliisaliti hata Serikali ya Mwalimu Nyerere ikwame,” alidai Shaka.
Akijibu hoja na madai ya kwamba vigogo hao watatu walikiuka na kuvunja taratibu za vikao katika uteuzi, Shaka alisema hakuna kiongozi wa CCM aliyevuruga taratibu ila kilichofanyika ni kuhakikisha mgombea yeyote anayeteuliwa anatokana na misingi na maadili ya chama hicho.
“Chama chetu mapema kabisa kiliweka msimamo bayana, mgombea atakayebainika kutumia rushwa, anayegawa fedha na mwenye tuhuma za ufisadi au aliyekosa maadili ya uongozi , hateuliwi kuwa mgombea urais na kupeperusha bendera ya CCM, Kingunge na wenzake walifikiri mzaha mwisho wakajionea umadhubuti wa CCM,” alisema.