26 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

UVCCM: Magufuli amemamliza kazi kabla 2020

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala amesema Rais Dk. John Magufuli amemaliza kazi 2020, kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM.

Akizungumza katika mahojiano maalumu mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na televisheni ya Star TV, Kilakala alisema anaamini kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambao ndiyo mkataba baina ya chama na wananchi, hadi kufikia mwaka 2020 Rais magufuli atakuw hana deni tena na wananchi.

“Hadi sasa kuna mambo mengi yamefanyika katika sekta zote, ikiwemokatika sekta za elimu, afya, miundombinu na sekta ya maji, kwa hiyo niseme hadi ikifika 2020, Rais Magufuli atakuwa hana deni tena na wananchi,” alisema.

Alisema kwenye sekta ya afya, katika miaka minne ya utawala wa Rais Magufuli amejenga hospitali mpya 69 za wilaya zilizogharibu Sh bilioni 1.5 zinazotokana na mapato ya ndani.

Alisema hiyo ni hatua kubwa kwa kuwa tangu uhuru hadi kufikia mwaka 2015, katika kipindi chote hivho zilijengwa hospitali 77 tu za wilaya, hivyo ujenzi wa hospitali 69 katika kipindi cha miaka minne ni jambo la kipekee.

Alisema tayari ndani ya muda wa uongozi wa Rais Magufuli amejenga vituo vipya vya afya zaidi ya 352, vitu ambavyo mwanzo havikuwepo.

Alisema tayari shule mpya zimejengwa katika ameneo yote ya nchi na shule kongwe zimekarabatiwa na kuwa za kisasa zaidi, huku wananchi wakifaidika na sera ya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari.

Kilakala alisema kupitia Ilani ya Uchaguzi mwaka 2015, CCM iliaminiwa na wananchi wengi kupitia ilani yake ya uchaguzi ambayo ni ni mkataba wa chama na wananchi kwa hiyo inaendelea kusimamia ilani hiyo kuhakikisha inatekelezwa ikiwa imefikia katika hatua nzuri.

Alisema kwa sasa, yale yaliyobebwa na Ilani ya chama iliyobebwa na Rais Magufuli na kunadiwa kwa wananchi ambao waliielewa na kukipa chama hicho ridhaa ya kuongoza kwa sasa imetekelezwa kwa kiasi kikubwa.

Hali ya demokrasia

Kuhusu kuminywa kwa demokrasia nchini, Kilakala alisema demokrasia haijaminywa na Serikali ya Rais Magufuli ambayo ni wazi kwamba inaongoza katika suala la utawala bora.

“Tunapozungumzia vyama vya siasa kufanya shughuli zake, tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani hajazuia mikutano ya hadhara na kila mbunge wa chama anatakiwa kufanya shughuli za kisiasa katika maeneo yake,” alisema.

Alisema ajenda ya CCM kwa sasa ni maendeleo na mafanikio, ni kuwafuta machozi wananchi na kuwashughulikia wananchi kuhakiksha wanapatana maendeleo.

Alisisitiza kwamba sera walizozinadi kupitia ilani ya chama hicho zipo kwenye mkataba wao na wananchi, ambao ndio waliowapa ridha kwa kishindo.

“Sera ya CCM kwa wananchi ni kutaua kero zao na kuhakikisha wanapata kwa uhakika huduma zote muhimu za msingi.

“lakini zaidi kuna haki ya demokrasia katika nchi yetu na CCM inaamini kuwa maendeleo hayana chama, ndiyo maana pamoja na kwamba Rais hajapata kura nyingi katika Mkoa wa Dar es Salaam lakini anatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika mkoa huu,” alisema.

Alisema pia kuwa ni wajibu wa vijana kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwania nafasi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ili kuonyesha uwezo wao katika uongozi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu mwishoni mwa wiki, Kilakala alisema ni wazi kwamba mahitaji ya vijana kwa sasa ni mengi na hakuna wa kuwatetea kama hawajaamua kujitetea wenyewe.

Alisema aliona ni vyema kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais  Magufuli, kwa kuwa imeonyesha imani kubwa kwa vijana na kuwataka vijana waliopewa nafasi za uongozi kuhakikisha kuwa hawamuangushi.

“Na sasa, katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ni wajibu wa vijana kujitokeza na kuchukua fomu na kugombea. Mahitaji ya vijana ni mengi katika taifa hili.

“Sasa hivi tuko wengi, mahitaji yetu ni mengi, tujitafakari na kuchukua hatua. Hakuna mtu yeyote anayeweza kututetea kama sisi wenyewe hatujaamua kujitetea,” alisema.

Maendeleo bila itikadi

Alisema kwa kauli ya Rais, alisema amewasamehe waliochagua upinzani na kwamba CCM na serikali yake kazi yake ni kupeleka maendeleo katika maeneo yote ya nchi bila kujali chama.

Kilakala alieleza kuwa kungekuwa na uwezekano wa kususia maendeleo kwa sababu Jiji la Dar Salaam linaongozwa na upinzani, lakini kwa kuthamini kwamba wananchi wote wana haki sawa kupata maendeleo na kuthaminiwa utu wao, Serikali haiwezi kuwa ya kibaguzi.

Alisema CCM inaamini binadamu wote ni sawa na kila mtu ana haki ya kuthaminiwa na kutambuliwa utu wake, hivyo isifike mahala mtu yeyote akanyanyaswa kwa sababu alikuwa upinzani, kwa kuwa jukumu lao ni kuongoza nchi na wananchi, bila kuangalia chama, dini, kabila au rangi.

Alieleza kuwa katika teuzi zake, CCM inaangalia uwezo, weledi na uchapakazi wa mtu, kwa hiyo anaamini hili wimbi la wapinzani kuhamia CCM ni ishara kuwa wameujua na kuufanhamu ukweli kwa sababu hata viongozi wakuu waliowania urais 2015 wamehamia CCM.

“Kwa hiyo hii inamaanisha kuwa yale waliyoyatarajia wangeyafanya kama wangepewa ridhaa tayari yanafanywa na Rais Magufuli. Kuna wabunge pia ambao waliona kuwa yale waliyoyatarajia na kuyasema majimboni kwao tayari yanatekelezwa na Rais Magufuli.

“Kwa hiyo haina sababu ya kuendelea kupinga, mimi nipongeze maamuzi yao ya kujua ukweli na kuunga mkono juhudi,” alisema.

Alisisitiza kuwa wabunge na wanachama kutoka upinzani waliojiunga na CCM ni kwa sababu wameufahamu ukweli na wametumia vizuri demokrasia.

Wabunge kununuliwa

Alisema anashangazwa na propaganda kuwa wabunge wanaotoka upinzania na kurudi CCM wamenunuliwa na kuhoji mbona aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu alipotoka CCM kwenda upinzani hakuna aliyesema amenunuliwa.

Alisema katika mkakati maalumu wa Tanzania ya kijani ulioasisiwa na UVCCM unamaanisha Tanzania ya CCM, ikiwa na lengo la maalumu kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa

“Mkakati huu umefanikiwa kwa asilimia kubwa na matokeo yake yataonekana wazi Novemba 24, ambapo tutashinda kwa zaidi ya asilimia 90 kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alisema.

Alisema vijana sasa hivi wanathaminiwa na wamepewa nafasi za juu za uongozi kitaifa.

Amani nchini

Alisema vijana wengi waliopo sasa wameukuta Uhuru na wameukuta Muungano, mambo yanayowafanya Watanzania waishi kwa amani, umoja na mshikamano, kwa sababu ya uasisi uliofanywa na Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.

“Leo hii tunajivunia kwa sababu Mungu aliwapa maono hayo. Hatubaguani kwa rangi dini wala kabila, wote tunapendana na tunaishi wamoja.

“Wote tunaishi pamoja, kwa mfano hapa Dar watu tunaishi kwenye nyumba ya vyumba sita kila chumba kina mtu wa dini, imani na kabila tofauti na wanaishi salama, tukipoteza amani hii hatuna mahala pa kukimbilia,” alisema.

Alisema ni wajibu wa vijana kuhakikisha kwamba wanailinda amani hii na kutumia nguvu zote kuhakikisha wanailinda amani na hawatumiwi kwa namna yoyote kuharibu amani hii.

Alisema ni suala la kushukuriu kwa kupata viongozi wenye nia ya dhati kuitoa Tanzania hapa ilipo kuipeleka mahala pengine, hivyo wanahitaji kuungwa mkono kwa dhati.

Alisema wapo wanawaombea mabaya viongozi wao, lakini wanatakiwa kutambua kuwa Mungu huwa hapokei dua mbaya na kwamba wanapowaombea wenzao mabaya watarajie ndiyo wanapata mafanikio.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles