31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yenye njaa kuishukia Singida leo

JACKLINE LAIZER, ARUSHA

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Simba leo itashuka dimbani kuumana na Singida United, katika mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 15, baada ya kushuka dimbani mara tano na kushinda michezo yote.

Kwa upande wake, Singida United inaburuza mkia, ikiwa na pointi tatu, baada ya kushuka dimbani mara saba na kuchapwa mara nne na kutoka sare tatu.

Wekundu hao wa Msimbazi ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC , katika wao uliopita uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, waliwasili jana jijini hapa kwa msafara wa watu 22 unaojumuisha viongozi, benchi la ufundi na wachezaji.

Katika mchezo huo, Simba itawakosa wachezaji wake mahiri kiungo Jonas Mkude, mshambuliaji John Bocco na mabeki Shomary Kapombe, Mohamed Hussein.

Pia itakosa huduma ya kinda Ally Salum, wote hao wanasumbuliwa na majeraha.

Akizungumza na MTANZANIA baada ya kuwasili jijini hapa,  Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu aliwapongeza na kuwashukuru wapenzi, mashabiki na wadau wa Simba wa mkoani hapa kwa mapokezi makubwa waliyoyafanya huku akiwahaidi ushindi katika mchezo wao wa leo na mechi nyingine zilizo mbele yao.

Alisema wachezaji wao wako  timamu kimwili na kiakili na kuongeza kuwa nguvu zao zote wamezihamishia Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho( Kombe la Azam)
lengo likiwa kuhakikisha wanatwaa ubingwa na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.

“Tumeshashinda michezo mitano mpaka sasa na nia yetu ni kushinda mechi zote mpaka tutwae ubingwa, baada ya kushindwa kuendelea na michuano ya kimataifa nguvu zetu tumezielekeza Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho hivyo wapenzi wa Simba hatutawaangusha,” alisema Lweyemamu.

 Alipoulizwa kuhusu hali mbaya za viwanja hasa maeneo ya kuchezea kama inaweza kuathiri mwenendo wa timu yao alisema: “ Ni kweli viwanja vingi haviridhishi lakini haiwezi kuwa sababu ya sisi kutopata matokeo mazuri, asilimia kubwa ya wachezaji viwanja hivyo ndivyo walivyovizoea.”

Uwanja wa Sheikh Amri Abeid unatumiwa na timu ya Singida United kwa ajili ya michezo ya nyumbani, baada ya Uwanja wake Namfua kufungiwa  hadi utakapofanyiwa marekebisho.

Ligi  hiyo pia itaendelea viwanja vingine, Azam FC inayokamata nafasi ya sita, baada ya kucheza michezo minne na kujikusanyika pointi tisa itakuwa nyumbani Uwanja wa Azam Complex kuumana na Ruvu Shooting  iliyoko nafasi ya tisa, baada ya kushuka dimbani mara saba na kujikusanyia pointi tisa.

Alliance iliyopo nafasi ya nane, baada ya kucheza michezo sita na kujikusanyia pointi tisa, itaumana na Tanzania Prisons iliyojikita nafasi ya tano, baada ya kushuka dimbani mara sita na kukusanya pointi 10, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Nyamagana.

Kagera Suga baada ya kushuka dimbani mara saba na kukamata nafasi ya pili ikiwa na pointi 13 itaikaribisha Ndanda Uwanja wa Kaitaba, Manispaa ya Bukoba.

Ndanda  ipo nafasi ya 18, baada ya kushuka dimbani mara saba na kujikusanyia pointi nne.

Mchezo mwingine niMwadui FC itakayokuwa mwenyeji wa JKT Tanzania Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles