26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

Uturuki haiwezi kukwepa kivuli cha siasa za utata

Rais Erdogan akilia katika msiba
Rais Erdogan akilia katika msiba

JARIBIO la mapinduzi ya kijeshi lililotokea hivi karibuni nchini Uturuki ni mwendelezo wa hamkani zinazosababishwa na siasa za utata zinazoendeshwa na Rais Recep Tayyip Erdogan.

Mtata huyo aliyeibuka saa 12 baada ya kuzimwa mapinduzi ndiye kiongozi anayeongoza kwa mkono wa chuma, tangu enzi za utawala wa Mustafa Kemal Ataturk mwanzilishi wa mfumo wa kisasa wa taifa hilo.

Erdogan aliibuka kwa mbwembwe nyingi akidai kunusurika kuuawa ingawa watu 240 waliuawa, licha ya kujinadi kuwa Amiri Jeshi Mkuu katika hotuba yake, lakini baadaye katika maziko ya mmoja wa maswahiba zake aliyeuawa alilia hadharani bila kujizuia.

Ameimarisha Uturuki kiuchumi katika kipindi kirefu cha utawala wake lakini kivuli ‘chekundu’ cha damu iliyomwagwa kwa siasa tata hakikwepeki, kama binadamu asivyoweza kukwepa kivuli chake na ikitokea siku ukaangalia kivuli chako usikione basi fahamu kuwa kifo chako kipo karibu na ikitokea Uturuki ikafanikiwa kufuta kivuli chake, basi anguko kuu la taifa hilo limewadia kutokana na kutaka kupambana kwa kila jambo hata yasiyohitaji vita, kwani inatafuta nyingi nasaba zinazoisababishia mingi misiba kwani kiongozi wake Erdogan mwenye umri wa miaka 62 ana sura nyingi za kisiasa zinazotatanisha ithibati ya sera zake zisizoeleweka.

Licha ya kuachia uwaziri mkuu alioutumikia kwa miaka 11 na kuwa Rais mwaka 2014, bado anatamani kujiongezea nguvu za kiutawala zilizosalia kwenye uwaziri mkuu, akikana kuendesha siasa za uhafidhina wa kidini lakini chama chake cha AKP kinajiakisi kidini.

Wananchi wakionesha hasira dhidi ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi
Wananchi wakionesha hasira dhidi ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi

Hata yeye mwenyewe amesoma katika shule ya Kiislamu kabla ya kupata shahada ya utawala katika chuo kikuu cha Marmara jijini Istanbul, alikuwa mwanachama wa chama cha Kiislamu cha Necmettin Erbakan kabla ya kuwa Meya wa Istanbul baadaye mapinduzi ya kijeshi yakaharamisha chama hicho naye akaswekwa jela kwa miezi minne.

Alianzisha AKP akishirikiana na Rais aliyemtangulia, Abdullah Gul, aliyewahi pia kuwa Waziri Mkuu aliyejaribu kuipeleka Uturuki katika mkabala wa kimataifa akakinzwa na mizizi yake ya Uislamu wa Kisunni.

Kimsingi kivuli cha utata wa siasa za nchi hiyo zinazohusisha msigano baina ya jeshi, wahafidhina na wasiopenda uhafidhina hakikuanza kwa Erdogan kwa mvutano unaosababisha utawala wa kimabavu ya kisirisiri.

Mahakama inatumika kunyamazisha upinzani huku ikimkinga Erdogan hata Serikali inapokiuka kanuni za kiutawala, kwa staili hiyo licha ya kufanikiwa kiuchumi Uturuki inajichimbia shimo yenyewe.

Badala ya kutatua changamoto vinatafutwa visingizio vya kunyamazishana kama ambavyo sasa swahiba wa zamani wa kisiasa wa Erdogan aliyegeuka hasimu wake, Fethullah Gulen, aliyekimbilia uhamishoni nchini Marekani anapotakiwa kurejeshwa kushtakiwa kwa kupanga mapinduzi ingawa hakuanza kuandamwa sasa kwani mahakama nchini humo zinaitaka Marekani imkabidhi akujibu tuhuma za ugaidi, lakini ombi hilo halijaridhiwa.

Kinachosababisha mkanganyiko zaidi ni viongozi wa Uturuki kutotambua mwelekeo wa sera zao zinazojiakisi kwa misingi ya Kiislamu, lakini wakivunja misingi ya imani hiyo, kwa kutengua sheria za awali huku ufisadi na ufujaji wa mali za umma ukitamalaki.

Msimamo wa Uturuki kimataifa unayumba kwani licha ya kutarajia masilahi lakini inakiuka misingi ya kibinadamu kwa kuangamiza jamii pinzani wakiwemo Wakurd walioko Kusini Mashariki ingawa ndio wanaoizuia IS isijipenyeze zaidi ndani ya Uturuki.

Kuna maswali mengi hata kuhusu jaribio la mapinduzi la hivi karibuni kwani ni kawaida nchi hiyo kuunda majaribio feki ikitafuta kisingizio cha kuwavurumisha wapinzani kama ilivyowakamata askari 6,000 wa ngazi mbalimbali baada ya jaribio hilo lakini ukweli halisi unakanganya.

Eti ndege iliyomchukua Rais aliyekuwa akirudi Ankara kutoka mapumzikoni mjini Marmaris ilisukwasukwa na ndege za kivita, kama wangetaka kumuua basi wangeweza kumtungua kirahisi na kumaliza mchezo na pia askari waliofika muda mfupi baada ya kuondoka Marmaris na kufyatua ovyo risasi ni utata mwingine!

Sasa Erdogan anataka kurudisha tena hukumu ya kifo iliyofutwa mwaka 2004 nchini humo likiwa mojawapo ya masharti ya kujiunga na EU, kwa mchezo huo wa kuigiza unaoendelea Uturuki haitashangaza kama hamkani ikawa si shwari kadiri siku zinavyoenda.

RAS INNO +255 778 218 730

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles