26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

CCM ‘wamemmiss’ Lowassa

lowassa

INAWEZEKANA nikawa tofauti na wengine waliofuatilia Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika mjini Dodoma Jumamosi iliyopita.

Utofauti wa hoja yangu ni mtazamo katika kuchambua kile nilichokiona na kukisikia kikizungumzwa na wajumbe waliopata nafasi ya kuhutubia mkutano huo.

Mkutano huo ulikuwa mahususi kwa ajili ya kumteua Mwenyekiti mpya atakayekiongoza chama hicho kikongwe hadi uchaguzi wa ndani wa CCM utakaofanyika mwakani kwa kufuata kalenda. Mkutano huo uligusa hisia za wafuatiliaji wa siasa kila pembe ya nchi hii.

Tofauti na mikutano mikuu ya nyuma ya chama hicho ambayo ilipambwa kwa hoja mbalimbali, zikiwamo hoja za kupambana na ufisadi, Mkutano Mkuu wa mwaka huu ulitawaliwa na jina la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye alikihama chama hicho mwaka jana na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Pamoja na jina la Lowassa mara nyingi  kuonekana chungu midomoni au kelele masikioni mwa baadhi ya  Wana-CCM, lakini ndani ya mkutano huo, jina hilo liliibuka upya na kuonekana tamu kwenye ndimi za baadhi ya viongozi waliopewa nafasi ya kuwahutubia wajumbe wa mkutano huo.

Utamu wa jina hilo uliwasilishwa kwa kauli mbalimbali na vijembe, hata hivyo, kwa jicho la tatu ilikuwa rahisi kutambua kwamba kauli hizo ziliashiria kukosekana kwa Edward Lowassa, swahiba wao wa siku nyingi, aliyekuwa akitajwa mara nyingi kwamba alikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho, wakati akiwa kada wake.

Kikwete, aliyekiongoza chama hicho tawala tangu mwaka 2006, alikabidhi kijiti cha uenyekiti kwa Rais John Magufuli na kumfanya awe Mwenyekiti wa tano kukiongoza chama hicho.

 Katika miongo kadhaa iliyopita, tumeshuhudia namna CCM kilichojinasibu kama chama cha wakulima na wafanyakazi, kikigeuka na kuwa pango la mafisadi na walarushwa.

Kutokana na hilo, wafuatiliaji na wapenzi wa chama hicho walitegemea kuwa katika mkutano huo wa Julai 23 mwaka huu, ungetoa fursa ya kipekee kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu, kingejielekeza kwenye ajenda ya kujiimarisha kutokana na ukweli kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulionesha kwamba kilikuwa kimepoteza imani kwa wananchi, kingeeleza mikakati yake ya baadaye ya kujipanga upya, lakini muda mwingi waliutumia kurusha vijembe kwa wapinzani.

Tayari wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wameeleza bayana kwamba, kitendo hicho cha Mkutano Mkuu huo kutawaliwa na jina la Lowassa, kinaonesha hofu waliyonayo dhidi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), na kwamba wanakiri kwamba walitikiswa  katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Hali iliyoonyesha woga na hofu kwa nguvu ya Lowassa, walijikuta wakitumia vijembe huku wengine wakikwepa kumtaja kwa jina.

Katika mkutano huo pia, Mwenyekiti Kikwete, ambaye alikuwa akihitimisha ngwe yake, aliutumia kumtupia vijembe pia Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, kwamba ametoka ngazi ya kitaifa (alipokuwa CCM) na kwenda kugombea uenyekiti wa Chadema ngazi ya wilaya, jambo ambalo halikuwa la kweli.

Katika mazungumzo yake hayo, alionesha kusikitishwa na hatua ya kiongozi huyo wa kitaifa kujishushia heshima kwa kwenda kugombea nafasi hiyo ambayo alisema anagombea na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea.

Kikwete alitoa kijembe hicho kwa kile kinachoonekana kutokuwa na uhakika na maneno yake. Ukweli ni kwamba Sumaye anagombea nafasi ya uenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani na si Wilaya, hagombei na Kubenea kama alivyosema na badala yake Mbunge huyo anagombea nafasi ya umakamu mwenyekiti.

Mbali na hilo, alionekana kumlenga Askofu  Gwajima pale aliposema kuwa alileta mfarakano kwa kudai kuwa hataki kukabidhi uenyekiti wa CCM.

Pamoja na yote hayo, Kikwete alikiri kwamba kukatwa kwa jina la Lowassa kulitishia CCM kuanguka katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

“Kama kuna kitu nakifahamu vizuri maishani ni CCM. Katika historia ya CCM hakuna wakati kulikuwa na tishio la kugawanyika kama mwaka jana”.

Kauli hiyo ya Kikwete inadhihirisha pasipo shaka, kuwa kitendo cha Lowassa kukihama chama kilichomlea, kiliwatikisa CCM.

Maneno hayo na mengine, ndiyo yaliyotawala katika hotuba ya Kikwete badala ya kueleza mikakati ambayo Mwenyekiti mpya, John Mgufuli angepaswa kuifanya.

Naye Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuph Makamba, alipotakiwa kutoa neno kwa niaba ya wazee, badala ya kutoa maoni ya kukijenga chama, alishusha vijembe vizito kwa Lowassa.

Duru zaidi zilitafsiri kitendo hicho kwamba Mzee Makamba alitumika kama spika ya kuzungumzia mengine mengi dhidi ya Lowassa, ambayo yalijaa kwa muda mrefu moyoni mwa Kikwete.

Katika tafsiri hiyo hiyo, upo mtazamo wa ujumla kwamba, ulifika wakati muktadha wa kisiasa wa mkutano huo haukueleweka,  kwa sababu ajenda za muhimu za kusimamia siasa za ndani ya chama hicho zilihama ghafla na kuparamia wanasiasa ambao wamekwisha kukitegea kisogo chama hicho.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdalah Safari, katika tathimini yake juu ya kile kilichotokea ndani ya Mkutano Mkuu wa CCM, anasema mkutano huo ulikosa ajenda za msingi na badala yake ukapambwa kwa jina la Lowassa.

Katika mahojiano yake na gazeti hili, Profesa Safari anasema jambo hilo linaonyesha pasipo shaka kuwa bado wanamwogopa mwanasiasa huyo mwenye ushawishi mkubwa katika jamii nchini.

Anasema jambo hilo linaonesha wazi kuwa joto la Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana bado linaendelea kuwatoa jasho.

“Tangu tumalize uchaguzi wa mwaka jana, ndani ya CCM hakuna ajenda nyingine zaidi ya kumjadili Lowassa, jambo linaloonesha wazi Lowassa bado ni tishio kwao.

“Chadema tunafarijika kusikia upepo wa Lowassa unaendelea kukitesa chama hicho, ndiyo maana tunaamini kiongozi tuliyempokea ni mtu makini.

“Bado anaendelea kuogopwa, hawana ajenda nyingine katika vikao vyao zaidi ya kumtaja,” alisema Profesa Safari.

Kutokana na hilo, inaonesha wazi kwamba chama hicho kikongwe kimechanganyikiwa, kinaumizwa na kile kilichotokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana baada ya kupoteza majimbo muhimu, hususan Dar es Salaam.

Chama hicho tawala kilipoteza majimbo kama Kinondoni, Kibamba, Ubungo, Temeke na Kawe, huku Halmashauri ya Jiji ikichukuliwa na upinzani, ni moja ya mshtuko walioupata CCM.

MAMBO YALIYOVUTIA WENGI

 Jambo jipya ambalo limewavutia wengi ni pale Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Rais John Magufuli, alipowataka wajumbe wa Mkutano Mkuu huo kutafakari juu ya kuwapo vyeo visivyo na tija na nafasi ya chipukizi wa chama.

Katika hilo, alisema si sahihi kwa watoto wenye umri wa miaka minane hadi 15 kujihusisha na siasa, huku akihoji wanasoma muda gani?

 

NA ELIZABETH HOMBO – 0712792216

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles