Nahitaji ufafanuzi kutoka kwa Mzee Makamba

MZEE Yusuf Makamba
MZEE Yusuf Makamba
MZEE Yusuf Makamba

Na LEAH MWAINYEKULE,

MZEE Yusuf Makamba ni aina ya mwanasiasa ambaye wengi wetu hupenda sana kumsikiliza. Tangu alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wengi tulikuwa tukifuatilia hotuba zake kwa karibu.

Binafsi, nilikuwa napendelea sana kusikiliza hotuba zake kutokana na umahiri wake wa kunukuu vifungu vya Maandiko Matakatifu kila alipokuwa akizungumza.

Mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao ulikuwa na lengo la kumchagua Rais John Magufuli kuwa mwenyekiti mpya wa chama, tulitarajia mmoja wa wazungumzaji angekuwa Mzee Makamba, kweli akazungumza.

Alipoinuka na kusogelea jukwaa kuu kwa ajili ya kuzungumza, kila mtu alitulia kumsikiliza.  Kama kawaida alianza kwa kunukuu kifungu cha Biblia na kuendelea na hotuba yake iliyokuwa na nukuu nyingine kadhaa, huku akizioanisha na uhalisia wa yaliyokuwa yakiendelea Dodoma kwa wakati huo na yaliyokuwa yakiendelea katika siasa za Tanzania kwa ujumla.

Nukuu moja ambayo imeniacha nikitafakari tangu alipoisema, ni ile aliyosema yafuatayo: “Wapinzani nataka mjue Jakaya aliwabatiza kwa maji, lakini huyu anayekuja atawabatiza kwa moto.

Kwa wasomaji wa Biblia, watagundua kwamba Mzee Makamba aliitamka hiyo sentensi kwa kuchukua maneno yaliyosemwa na Yohana Mbatizaji, wakati akizungumzia ujio wa Yesu Kristo.

Yohana alikuwa akiwabatiza watu katika Mto Yordani na katika Injili ya Mathayo Mtakatifu 3:11, anasema:  Kweli mimi nawabatiza kwa maji…bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi…yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

Mzee Makamba ameitumia nukuu hiyo katika kumwelezea Rais Magufuli, kama mwenyekiti mpya wa CCM.  Nilivyomwelewa, alikuwa akieleza kwamba Rais Jakaya Kikwete alikuwa kiongozi mpole ambaye wakati mwingine alikuwa hafuatilii sana mambo na maneno yaliyotoka kwa wapinzani, lakini sasa Rais Magufuli anavyouvaa uenyekiti wa chama, basi wapinzani wakae tayari kunyooka.

Wapo ambao hawatakubaliana na tafsiri yangu, lakini ukiiangalia historia ya hotuba za Mzee Makamba, utagundua kwamba ni mtu wa kutoa vijembe, ambaye hata wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, alitumika kwa ajili ya kutoa maneno ya ‘kuudhi’ kwa vyama vya upinzani na wagombea wao.

Ni mahiri sana wa kuzungumza na akiongea kila mtu anamsikiliza na kucheka kutokana na namna anavyowasilisha hotuba zake.  Hata kwa hili la juzi, ni rahisi sana kwa mtu yeyote anayemfahamu huyu mzee kujua alichokuwa akikimaanisha.

Kauli hiyo ya Mzee Makamba ndiyo iliyonifikirisha na kunifanya nijiulize kama kweli alimaanisha ninachodhani alimaanisha.  Mwanzo, nilidhani sentensi yake ilikuwa imewalenga wanachama wa CCM, ambao Rais Magufuli kwa sasa ni mwenyekiti wao.

Kwamba wanachama wa CCM huenda walikuwa wamebweteka kutokana na upole wa Rais Kikwete, lakini sasa anashika hatamu Rais Magufuli ambaye sote tunamfahamu namna asivyopenda mchezo mchezo na kuendekeza wavivu na wafujaji.

Mwanzo nilidhani kwamba Mzee Makamba alikuwa amewalenga wanachama wa CCM kutokana na ukweli ambao hata Rais Magufuli mwenyewe aliueleza namna baadhi ya wanachama walivyokuwa na tabia zisizofaa, kama vile kuendekeza masuala ya rushwa.  Nilidhani aliwalenga wao na kuwaonya kwamba kutokana na ukali wa mwenyekiti wao mpya, basi “atawabatiza kwa moto.”

Hata hivyo, niliposikiliza vizuri na kuamua kurudia kumsikiliza kesho yake, nikagundua kwamba kumbe Mzee Makamba alikuwa akiwalenga wapinzani, watu ambao Magufuli ni Rais wao, lakini si mwenyekiti wa vyama vyao.

Watu ambao hawatakiwi kuongozwa na kanuni za Mwenyekiti Magufuli, bali zile zinazotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.  Watu ambao wala hawatakiwi kujieleza kwa Mwenyekiti Magufuli, bali kwa Msajili Jaji Francis Mutungi.

Nahitaji ufafanuzi kutoka kwa Mzee Makamba.  Kauli yake ililenga nini hasa?  Au kubatiza huku kwa moto ndiyo kunahusisha haya masuala ya marufuku ya shughuli za kisiasa hadi wakati wa uchaguzi?

Au kubatiza huku kwa moto kunahusisha kunyimwa kabisa kwa vibali vya maandamano ya amani vya kudai masuala mbalimbali ambayo wapinzani wanadhani yana tija kwa taifa?  Au kubatiza huku kwa moto kunamaanisha wapinzani hata wakitaka kutoa hoja zao katika chombo wanachoweza kusemea – Bunge – basi wazimwe na kunyamazishwa kabisa?

Mzee Makamba, naomba ufafanuzi wako.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here