25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Trump anatafuta ushindi kwa kubadilisha mbinu kila hatua

Republican U.S. presidential candidate Donald Trump delivers foreign policy speech at the Mayflower Hotel in Washington

NA RAS INNO NGANYAGWA,

WAPINZANI wa Donald Trump waliompuuza kwa jinsi alivyoendesha kampeni za kuteuliwa kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Republican, sasa wanalazimika kujipanga zaidi.

Hilo linatokana na ukweli kwamba alichodhihirisha tangu alipokubali rasmi kuteuliwa, ni mabadiliko ya mbinu na si yule mshari, mwenye mbinu chafuzi, atakayetatanisha uhusiano wa taifa hilo na dunia.

Sera za uendeshaji serikali nchini Marekani hutegemea mtazamo wa Rais ndiyo maana uteuzi wa wagombea huibua maoni mbalimbali duniani, ambapo tayari inafahamika kuwa mchuano ni baina ya ‘fahali’ Trump na jike la mbegu, Hillary Clinton.

GOP inajivunia kukubalika wakiamini watazoa kura kuingia Ikulu na kuanza kazi ya kurejesha usalama, ustawi na mshikamano kwa kujenga nchi karimu inayozingatia sheria na mtangamano katika maeneo haya;

USALAMA WA NDANI

Udhibiti wa uhalifu umepwaya kwa mauaji yaliyoongezeka kwa asilimia 17 katika miji mikubwa 50 ya Marekani ndani ya robo karne, idadi ya askari waliouawa kazini imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 50, huku uhalifu ukiongezeka kutokana na wahamiaji haramu 180,000 walioingia Marekani zaidi ya mwaka jana hivyo kudhibiti uhamiaji haramu mipakani ni kipaumbele cha Republican ikiingia madarakani.

Kimsingi Serikali inapaswa kulinda raia wake hivyo ugaidi katika miji na uhasama baina ya polisi na wananchi, vinatishia ustaarabu wa Marekani na kuanzia Januari 20 mwakani, usalama utaimarishwa serikali mpya itakapoanza kazi madarakani ikiwa itakuwa ni ya Chama cha Republican.

UKUAJI WA UCHUMI

Republican inasema uchumi umeanguka, asilimia 40 ya watoto wote wa Marekani wenye asili ya Kiafrika wanaishi katika umasikini mkubwa, asilimia 58 ya vijana weusi wamepoteza ajira, Walatino milioni mbili wanaishi katika lindi la umasikini kuliko ilivyokuwa kabla Obama hajaingia madarakani.

Vile vile, watu wazima milioni 14 wamepoteza ajira na kipato cha familia za kimarekani kimeshuka kwa dola 4000, huku nakisi ya biashara ikifikia dola bilioni 800 kwa mwaka jana pekee.

Wanajinadi kurekebisha mdororo huo ikiwemo kudhoofika kwa miundo mbinu na bajeti isiyotosheleza wakati deni la taifa la dola Trillioni 19 likiongezeka.

UGAIDI WA KIMATAIFA

Raia wa Marekani ughaibuni wamelengwa kigaidi huku mataifa yanayotuhumiwa kudhamini ugaidi, ikiwamo Iran, ikizawadiwa mrejesho wa dola bilioni 150 kwa mkataba wa nyuklia ambao haukuinufaisha Marekani kwa chochote, usalama wa kimataifa umetatanishwa kwa kukosa udhibiti katika maeneo korofi kivita ikiwamo Syria, Libya, udhaifu unaofanya Wamarekani wajute kuipa madaraka Democratic na sasa ni wakati wa kuiondosha kwenye uchaguzi wa Novemba kwa mujibu wa Trump na chama chake.

Kabla Hillary hajawa Waziri wa Mambo ya Nje, ISIS haikujulikana, Libya ilikuwa thabiti, Iraq iliimarika kiusalama, Iran ilikabwa kwa vikwazo, Syria ilikuwa tulivu na baada ya miaka minne ya Hillary katika nafasi hiyo kuu ya uongozi katika serikali, ISIS imeimarika.

Libya imeraruliwa, Misri ikanyakuliwa na wahafidhina wa Kiislamu na kulazimisha mapinduzi ya kijeshi, vurugu zisizoisha zinarindima Iraq, Iran imesafishiwa njia kurutubisha nyuklia, huku Syria ikiwa imetumbukia katika vita vya wenyewe na kuzalisha wakimbizi na wahamiaji wanaotishia mustakabali wa mataifa ya Magharibi.

Mashariki ya Kati imegubikwa vita vinavyogharimu fedha na maisha ya askari wengi. Republican itaimarisha mahakama na majeshi ya ulinzi ndani na nje ili kudhibiti magaidi, itaachana na sera za ubadilishaji serikali katika mataifa mengine na kushikamana na kuwajibika kikamilifu ndani ya NATO ili kujikinga dhidi ya mashambulizi ya kigaidi.

MKAKATI MBADALA

Kipaumbele cha Republican ni Umarekani kwanza, si utandawazi ili taifa liheshimike duniani kwa mabadiliko ya kiuchumi yatakayosababisha ajira nyingi mpya ingawa yatapingwa na mabwanyenye waliojinufaisha na mfumo uliowapendelea wanaosimama nyuma ya Clinton kwa kutaka kuendeleza ubinafsi, wakimpatia masurufu ya kampeni ili wamdhibiti atimize matakwa yao, ndiyo maana ujumbe wa Hillary ni kuwa mambo hayatabadilika.

Mkakati mpya wa GOP ni kutovumilia uzembe wa viongozi wanaoshindwa kutimiza wajibu waliokabidhiwa watakaochukuliwa hatua stahiki, hawatafunika kombe mwanaharamu apite kama Hillary Clinton alivyofunikiwa kombe na FBI kwa kuficha makosa yake katika anuani-pepe binafsi.

 KUIMARISHA USTAWI

Sera mpya ya biashara inayozingatia ukuaji uchumi na kukabiliana na nchi laghai zinazoangusha maslahi ya kibiashara ya Marekani, kwa kuwa uzoefu wa kibiashara wa mgombea Trump utatumika kuitajirisha Marekani kwa kutumia wabobevu wa kibiashara wa Kimarekani walioko nje na kubadilisha mwelekeo wa kibiashara kwa kuvunja mikataba ya kimataifa isiyoinufaisha Marekani.

Kuwa na mfumo rahisi wa kodi kwa wafanyabiashara kwa kuondoa msururu wa kodi zisizo muhimu, hivyo kusababisha kuzaliwa kwa kampuni mpya zitakazopanua wigo wa ajira bila kizuizi kilichosababisha mdororo wa fursa za kazi na kugharimu taifa dola trilioni mbili kwa mwaka jana pekee.

Kwa kubadilisha mwelekeo utakaosababisha kazi zitakazozalisha dola trilioni 20 kwa sera mpya zitakazoimarisha kiwango cha maisha kwa mapato yatakayoboresha miundombinu ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege na usafiri wa reli.

Kuongeza ajira kutainua elimu kwa watoto kwani wazazi watamudu kuwasomesha watoto wao katika shule bora wazitakazo.

 HAMASA

Marekani lazima ijiamini kwa kuwa historia inaihukumu kwa kukengeuka misingi na inapaswa kuidhihirishia dunia kwamba bado ni imara na thabiti kwa kusimama pamoja kuwa na nguvu tena, kujivunia, kuwa salama na kuwa taifa kuu tena kwa mujibu wa mtazamo wa ‘GOP’ kupitia kinara wake atakayeisaka ‘Ikulu Nyeupe’ mwezi Novemba, ndivyo Republican wanavyojinadi wakiwatangulia mahasimu wao, Democratics ambao bila shaka watajibu mapigo watakapomsimika rasmi mgombea wao, Bi Clinton.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles