28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Utumikishwaji watoto upigwe vita kwa vitendo

watotoNa Amina Omari

TATIZO la utumikishwaji wa watoto chini ya umri wa miaka 18 ni moja ya changamoto kubwa katika maeneo mengi hususani katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.

Kwani wapo watoto wamekuwa wakitumikishwa kwa kupewa kazi ngumu ambazo zipo juu ya uwezo wao kiumri hali inayosababisha athari za kimwili pamoja na kisaikolojia.

Tanzania ni moja ya nchi inayokabiliwa na changamoto ya uwepo wa watoto ambao wanatumikishwa hususani katika kazi hatarishi kama vile maeneo ya madanguro, baa, shambani pamoja na majumbani.

Hata hivyo, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Wekeza tatizo limeonekana zaidi katika mikoa ya Tanga na Kigoma kwa watoto wengi kutumikishwa kazi katika mazingira ambayo si salama kwa umri wao na hatarishi.

Kwa upande wa Mkoa wa Tanga utumikishwaji wa watoto upo kwa kiwango kikubwa katika maeneo ya mashamba makubwa ya chai, mkonge pamoja na utumikishwaji wa kazi za ndani.

Kwa upande wa Mkoa wa Tanga si jambo la kustaajabisha kukutana na mtoto mitaani akiuza kahawa, karanga pamoja na maji wakati ambao wenzake wapo shule wakipatiwa elimu.

Vile vile ukipata bahati ya kutembelea maeneo ya mashamba ya chai katika eneo la Amani utakutana na  makundi ya watoto hususani wa kike wakiwa wanajishughulisha na kazi za kilimo  kama sehemu ya kuongeza kipato cha familia.

Kwa mtazamo wangu kumtumikisha mtoto kwa shughuli za uzalishaji mali kunachangia kupunguza utu wa mtoto na kuweza kumwathiri katika makuzi na ukuaji wake kwa ujumla.

Kwani hali hii inasababishwa na jamii kuwa na uelewa mdogo  kuhusu athari za utumikishwaji huo hali inayochangiwa na umasikini katika ngazi ya kaya.

Jamii inatumia tatizo la umasikini wa kipato kuwatumia watoto kama chambo cha kuwaingiza katika shughuli za utumikishwaji wa watoto ili kuweza kuongeza kipato katika ngazi ya familia.

Lakini katika hili la utumikishwaji  muhanga mkuu ni mtoto wa kike ambaye kwa kiasi kikubwa utumikishwaji huo unaathiriwa na mfumo wa tamaduni zetu ulivyo.

Mfumo huo unatoa fursa kwa mtoto wa kike kuanza kupewa majukumu ya kazi pamoja na malezi wangali bado wadogo ilhali wa kiume wakiwa wanapewa fursa ya kupewa kipaumbele cha elimu.

Hata hivyo, licha ya Serikali kuingia mikataba mbalimbali ya kimataifa pamoja na kutungwa  kwa sheria za kuwalinda watoto dhidi ya utumikishwaji, lakini bado mpaka sasa wameendelea kuteseka.

Kama tunaamini kuwa watoto ni rasilimali ya kesho hivyo wazazi na walezi ipo haja ya kuhakikisha tunawalinda watoto wetu katika kuhakikisha hawatumikishwi katika ajira hatarishi.

Na kama kuna ulazima wa kuwafanyisha kazi basi ziwe ni zile ambazo zinafanyika chini ya usimamizi maalumu na ambazo hazitaweza kuwaathiri kiakili wala ukuaji wake.

Wazazi hususani wa vijijini na wale walioko katika maeneo ya shambani  wapewe elimu stahiki juu ya madhara ya utumikishwaji wa watoto ili waweze kuwalinda na kuacha kuwatumia katika shughuli za uzalishaji mali.

Serikali iweke mazingira rafiki ya kutolea elimu kwa kuhakikisha shule zinakuwa na miundombinu bora ya kutolea elimu, walimu pamoja na vifaa viwepo vya kutosha.

Moja ya eneo ambalo linasababisha watoto wengi kuingia kwenye utumikishwaji ni shule nyingi kuwa na mazingira duni ya kutolea elimu hususani upande wa majengo pamoja na uhaba wa walimu.

Pia Serikali kuhakikisha sheria za kupinga utumikishwaji kwa watoto zinafuatwa na kusimamiwa kwa ukaribu ili kuhakikisha watoto wanakuwa katika makuzi yaliyobora na salama.

[email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles