22.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Wagawana mali za kamati ya maafa

NA BENJAMIN MASESE, MWANZA

SAKATA la mwili wa maraehemu, James Masibuka kutozwa faini ya Sh 50,000 na wananchi wa Nzengo ya Kanindo kabla ya kuzikwa, limechukua sura mpya baada ya wananchi kugawana fedha na mali zote za kamati ya maafa.

Uamuzi wa kugawana mali na fedha za kamati hiyo ulifikiwa juzi katika mkutano ulioitishwa na Mwenyekiti wa Nzengo ya Kanindo, Michael Genji kujadili mambo mbalimbali ya mtaa huo.

Katika hali isiyotarajiwa baada ya kusoma agenda 11 za mkutano huo, ghafla kijana wa marehemu Masibuka, Ndawala Masibuka aliinuka na kuomba viongozi wa kamati ya maafa kuongeza agenda ya kujadili tozo ya baba yake ambayo haikuwemo.

Baada ya agenda kukubaliwa alipewa  nafasi ya kueleza ambapo alisema kitendo cha baba yake kutozwa faini ya Sh 50,000  hakubaliani nacho, kwani hakuwa na kosa kwa sababu mahindi alipewa kihalali na Serikali kutokana na kukabiliwa na njaa mwaka 2002.

“Yale mahindi yalitolewa na Serikali kwa watu waliokuwa hawajiwezi,kama uongozi wa serikali ya mtaa kwa wakati huo ulimwandika jina lake na kumpa msaada iweje tena ukamdai wagawane,alihoji.

“Siwezi kukubali kama ni mahakamani tutakwenda kwa sababu kitendo kilichofanywa ni ubadhirifu katika ugawaji wa mahindi, kama baba yangu angekuwa amefanya  kosa la kwenye mtaa hapo ningekubali lakini si mahindi ya Serikali,”alisema Ndawala ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kanindo (Chadema).

Maelezo hayo yalisababisha wananchi kuja juu  huku wakitoa mifano mbalimbali ya watu waliowahi kutozwa faini na kuibuka suala la kugawa Nzengo hiyo kwa kigezo kwamba imekuwa kubwa  ambapo kura zilipigwa.

Katika upigaji wa kura, zaidi ya asilimia 65 ya wananchi wote waliunga hoja ya kugawa mtaa huo huku asilimia 35 wakitaka  kubaki kama ilivyokuwa awali.

Baada ya waliotaka Nzengo kugawanyika kushinda, agenda 11 zilizokuwa zimepangwa kujadiliwa zilifutwa na kuamriwa mali zote na fedha za kamati zikusanywe  na kuletwa mbele ya mkutano kugawana kati ya Nzengo mpya ya Majengo Mapya na Kanindo Original.

Mali za kamati ya maafa zilizokuwepo ni pamoja na Sh 292,500, mapipa mawili, sufuria kubwa 6,  sahani 200, vikombe 120, bakuli za chuma 100, surulu moja, majembe mawili, ndoo za maji 10, miiko 5 ya kupikia ugali, koleo mbili, turubai mbili na taa mbili.

Wananchi wa Nzengo ya Majengo mapya na Kanindo Original waliondoka kwenye mkutano huku wakiwa wamejitwisha mali walizogawana.

Marehemu James Masibuka alifariki Julai 22 na kuzikwa Julai 24, mwaka huu mtaa wa Kanindo ambapo kabla ya mazishi wananchi walitaka familia yake kutoa Sh 50,000 aliyotozwa mwaka 2002 baada ya kutumia peke yake mahindi ya ziada ya msaada uliotolewa   na Serikali.

Kabla ya marehemu kufariki Julai 22, mwaka huu, kijana wake  Ndawala alitoa taarifa katika kikao cha Nzengo  kilichoketi Julai 7,mwaka huu kuomba baba yake apokelewe katika mtaa huo na kumlipia kiingilio cha Nzengo na mke wake kama wageni wapya ambapo  alikubaliwa na kutoa Sh 30,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles