TPA yaboresha Bandari ya Mtwara

BandariNa Mwandishi Wetu, Mtwara

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeanza kuboresha miundombinu katika Bandari ya Mtwara na bandari ndogo za Lindi na Kilwa ili kunufaika na fursa kubwa zilizopo katika mikoa ya kusini.

Fursa zilizopo katika mikoa hiyo na ambazo zinatarajia kuinufaisha bandari hizo ni pamoja na shughuli za watafutaji wa mafuta/gesi, uzalishaji wa gesi asilia na kuhudumia bidhaa zitokanazo na gesi.

Mkuu wa Bandari Mtwara, Stella Katondo, alisema fursa nyingine zilizopo katika mikoa hiyo ni pamoja na kuhudumia bidhaa za viwanda vinavyojengwa mkoani Lindi na Mtwara na mazao mbalimbali yapatikanayo katika mikoa hiyo.

“Uboreshwaji wa bandari hizi unatarajia kuleta manufaa mbalimbali ikiwemo kukuza ajira kwa Watanzania na haswa kwa wakazi wa Mtwara na Lindi pamoja na kukuza mapato ya Serikali,” alisema.

Alisema tayari Mamlaka imeshaanza ujenzi wa gati ya kisasa katika Bandari ya Lindi itakayokuwa na urefu wa mita 4 hadi 8 na mchakato wa ujenzi wa gati nyingine ya kisasa katika Bandari ya Mtwara unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha.

“Ujenzi wa gati hiyo itakayokuwa na uwezo wa kuhudumia meli za aina zote zenye urefu wa mita 300, unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha 2016/2017,” alisema.

Stella alisema ujenzi wa gati hizo utasaidia kuongeza ufanisi wa bandari hizo na kuziwezesha kuhudumia shehena kubwa zaidi ya mizigo.

“Ujenzi wa gati hizi utasaidia kuongeza uwezo wa bandari zetu katika kuhudumia shehena ya mizigo na hatimaye kuongeza pato la Mamlaka na taifa kwa ujumla,” alisema Stella.

Katika hatua nyingine, Bandari ya Mtwara imethibishwa kuwa ni moja kati ya bandari zenye usalama zaidi duniani.

Kwa mujibu wa Stella, ukaguzi wa kuthibitisha ubora huo ulifanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) pamoja na Mamlaka ya Kimataifa ya Usalama wa majini.

Akizungumzia utendaji wa bandari hiyo, alisema katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2013/2014 hadi 2015/2016, shehena iliyohudumiwa katika bandari hiyo ni jumla ya tani 356,356 na 273,882.

Alifafanua kwamba katika jumla ya tani 356,356 zilizohudumiwa mwaka 2013/2014, tani 221,022 zilipakuliwa na tani 135,334 zilipakiwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here