24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

UTATA WATOTO 1,300 KUTOWEKA KIBITI

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


UTATA umeibuka baada ya kuwapo kwa taarifa za kupotea watoto 1,300 katika Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.

Taarifa za kupoteza kwa watoto hao katika kipindi cha kati ya mwaka 2016 na Julai mwaka huu, zilipatikana juzi wakati Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro alipofanya ziara ya kikazi wilayani Kibaha, Pwani.

Katika ziara hiyo, IGP Sirro alizungumza na wazazi, walimu, viongozi wa mashirika ya umma, wazee maarufu, wastaafu mbalimbali na kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani kuhusu taarifa hizo.

Kupitia mkutano huo, IGP Sirro, alieleza taarifa ya wanafunzi zaidi ya 1,300 mkoani humo ambao hadi sasa hawajulikani walipo na hawajaonekana shule wala katika familia zao.

IGP Sirro alisema huenda watoto hao ni watoro, hivyo  aliwataka wazazi washirikiane na Jeshi la Polisi kujua walipo.

Pia aliwataka wazazi kusaidiana na walimu wa shule za msingi na sekondari, ambazo wanafunzi walikuwa ni watoro ama hawajaripoti shule kwa miezi kadhaa, kutoa taarifa kwani wapo baadhi ya watoto wanaotumika kufundishwa uhalifu hata wa kutumia silaha na watu wasio wema.

Kutokana na utata wa taarifa hizo, MTANZANIA ilizungumza na IGP Sirro, ambaye alisema taarifa za kutoonekana kwa watoto hao zinatokana na Idara ya Elimu na wazazi.

“Ni taarifa ya muda mrefu, kipindi cha mwaka jana na mwaka huu, ni zaidi ya mwaka mmoja niliipata Wizara ya Elimu kule, ndiyo maana nimeelekeza wazazi ambao hawawaoni watoto wao kutoa taarifa.

“Maana kama mtoto humuoni shuleni wala nyumbani, ni lazima uripoti,” alisema IGP Sirro.

Kupotea kwa watoto hao kumezua sintofahamu kutokana na wazazi kudaiwa kuripoti tukio hilo polisi.

Hadi sasa haijaelezwa wanafunzi hao waliopotea ni wa shule za msingi au sekondari.

Hata hivyo, kwa sasa hali ya usalama katika Wilaya ya Kibiti na Rufiji imeimarika tofauti na miezi kadhaa iliyopita, lilipoibuka kundi la wahalifu ambao walikuwa wakiua watu wakiwamo askari polisi.

Katika matukio hayo ya mauaji, watu hao wasiofahamika walimuua Mwenyekiti wa zamani wa CCM Tawi la Njia nne liliopo katika Kijiji cha Muyuyu, Kata ya Mtunda wilayani Kibiti, Iddy Kirungi na mtoto wake, Nurdin Kirungi naye alifariki siku mbili baadaye baada ya kupigwa risasi ya tumbo.

Wauaji hao baada ya kutekeleza unyama huo, walitokomea kusikojulikana hali iliyotishia usalama wa raia na mali zao, huku wengine wakilazimika kuzikimbia nyumba zao kwa hofu ya kupoteza maisha.

Jeshi la Polisi Pwani kupitia kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, ambaye kwa sasa ni Kamanda wa Kanda Maalumu ya Kibiti, alithibitisha baadhi ya watu kuyakimbia makazi yao.

Akizungumza na MTANZANIA mapema mwaka huu, Diwani wa Kata ya Mtunda, Omary Twanga (CCM), alisema kutokana na mauaji hayo wilayani humo, hali imekuwa tete kwani wananchi wengi wanahofia usalama wao na watu waliofika katika msiba wa Kirungi hawazidi 20.

“Jambo hili ni la muda mrefu na wananchi wengi sasa wameingiwa na hofu, wanataka kuharibu sifa nzuri tuliyonayo ya kuitwa kisiwa cha amani,” alisema. 

WATENDAJI WAKIMBIA

Mauaji yaliyotikisa wilayani humo yalisababisha baadhi ya watendaji kukimbia vituo vyao vya kazi kutokana na kuingiwa hofu.

Vyanzo vya habari vimeliambia gazeti hili kwamba Mtendaji wa Chumbi C katika Kata ya Chumbi alikimbia kituo chake cha kazi.

Baadhi ya wakazi wa Kibiti waliozungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa majina gazetini, waliiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina wa matukio hayo. 

MATUKIO YALIYOTIKISA KIBITI

Mei 5, mwaka huu, kada wa CCM Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Amir Chanjale, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Aprili 29, mwaka huu, mkazi wa Kijiji cha Mgomba Kaskazini, Kata ya Mgomba, Ikwiriri, Hamad Malinda, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Aprili 14 mwaka huu, askari wanane waliuawa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi katika Kijiji cha Makengeni wilayani Kibiti.

Machi Mosi, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana, aliuawa.

Februari 21, mwaka huu, watu watatu akiwamo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, waliuawa kwa risasi.

Wengine waliouawa katika tukio hilo ni Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji mapato ya ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na Rashid Mgamba ambaye ni mlinzi, mgambo ambao walipigwa risasi kichwani na begani na walikufa papo hapo eneo la tukio.

Februari 3, mwaka huu, watu wasiojulikana walivamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga na kuichoma moto, huku yeye mwenyewe akifanikiwa kutoroka.

Januari 19, mwaka huu, mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Nyambunda, Oswald Mrope ambaye ni mfanyabiashara, aliuawa baada ya kupigwa risasi mbele ya familia yake.

Novemba 6, 2016, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyang’unda, Kijiji cha Nyambunda, Mohammed Thabiti, alipigwa risasi akielekea nyumbani kwake.

Oktoba 24, 2016 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyambunda, Ally Milandu, aliuawa kwa kupigwa risasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles