27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YATOA NENO BIASHARA YA UTUMWA LIBYA

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAKATI biashara ya utumwa nchini Libya ikielezwa kuendelea kushamiri, Serikali imesema hadi sasa hakuna raia wa Tanzania aliyeripotiwa kuuzwa.

Wengi wanaodaiwa kuuzwa ni vijana kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, wanaotumia njia za panya kwenda Ulaya.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba, akizungumza na MTANZANIA jana alisema: “Bado hatujapata taarifa za kuwepo Mtanzania yeyote katika kundi hilo wanaodaiwa kuuzwa.

“Lakini pia tumeelekeza balozi zetu zote zilizo karibu na nchi hiyo kufuatilia endapo kuna Mtanzania ambaye yupo katika utumwa huo.”

Pia alisema Serikali ya Tanzania inalaani endapo ni kweli kama kuna watu wanauzwa huko nchini Libya.

 WANASIASA WACHACHAMAA

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) na Hussein Bashe (CCM) wa Nzega Mjini, wametumia kurasa zao za kijamii kulaani vitendo hivyo na kutaka dunia kuvichukulia hatua.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Zitto aliandika: “Kwanini Watanzania waliopo Dar tusichukue hatua dhidi ya udhalilishaji wa Waafrika? Siku ya Ijumaa tukutane ubalozi wa Libya hapa nchini kuongea na balozi na kumpa risala yetu kupinga biashara ya utumwa inayofanyika nchini Libya. Mnaonaje?

“Waziri Mahiga (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustino Mahiga), umechukua hatua gani dhidi ya Libya kuhusiana na unyama dhidi ya Waafrika unaoendelea Libya? Umemwita balozi wa Libya nchini kujieleza?”

Naye Bashe aliandika: “Thanks (asanteni) mpaka sasa walounga mkono Petition hii ya kuitaka AU kuchukua hatua dhidi ya aina hii ya unyama kuuza Waafrika, mpaka sasa watu 57 elfu wameisha sign.”

UBALOZI WA LIBYA

Jana Serikali ya Libya ilikanusha taarifa za mamia ya watu kuuzwa kwenye minada nchini humo kwa kiasi kidogo cha chini ya Dola za Marekani 400.

Taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Libya nchini, ilisema si kweli kwamba watu hao walikuwa wanauzwa, bali ilikuwa ni kuwatorosha ili wafike katika kituo chao kama wahamiaji na wala si kama watumwa.

Taarifa hiyo ambayo ilisainiwa na Kaimu Balozi wa Libya, Saleh Kosa, ilisema mapatano yale yalikuwa ni gharama za kuwasafirisha na wala si gharama za kuuza uhuru wao ili wawe watumwa.

“Serikali ya Libya, mara tu baada ya kupata taarifa hizo ilivituma vyombo husika kufanya uchunguzi jumuishi na wa kina kuhusu madai hayo ambayo ni makosa kwa mujibu wa sheria za Libya na baadaye isambazwe kwa watu wote na pia kuwachukulia hatua za kisheria wote wanaohusika bila ya kujali kama makosa yenyewe yamefanywa kwa lengo la kuvukisha wahamiaji au utumwa,” alisema Kosa.

Alisema Libya inaamini kwamba mambo kama hayo, huwa ni sehemu yanayofungamana na uhamiaji haramu ambao Libya ndiyo nchi iliyodhurika zaidi na kwamba imekataa kuwajibika peke yake kubeba jukumu la kukomesha uhamiaji haramu.

“Libya inapenda kuhakikisha kwamba katika kukomesha suala la uhamiaji haramu na mambo yanayohusiana nayo inalazimu kuwapo kwa juhudi za pamoja za kimataifa na zilizoratibiwa ili kupambana na hali hiyo.

“Kwa kigezo hiki, Libya inaomba kuwepo na mikakati kivitendo na yenye athari kubwa baina ya nchi wanazotoka wahamiaji haramu, nchi wapitiazo na waendazo na pia kushirikisha taasisi husika za kimataifa na za kikanda,” alisema.

Kosa alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inaweka upya msisitizo wake kuiunga mkono Serikali ya nchi hiyo, kwa kuipa uwezo wa kiufundi na kilojistiki ili kuisaidia katika kudhibiti mipaka yake.

“Kuuhimiza Umoja wa Nchi za Ulaya na jumuiya ya kimataifa kushirikiana na nchi watokazo wahamiaji ili kufanya miradi ya maendeleo ya kudumu kwa lengo la kukomesha suala hili na athari zake hatari.

“Pia kutekeleza vifungu vya tamko la pamoja kuhusu uhamiaji na maendeleo, lililokubaliwa katika vikao vya Novemba 22 na 23 mwaka 2006 mjini Tripoli, Libya.

“Kuisaidia Libya kumudu gharama za kujenga na kuendesa vituo vya kuwaweka wahamiaji na kutoa misaada kusaidia maeneo yote yaliyodhurika na uhamiaji nchini Libya na pia kuvisaidia vyombo vya usalama vya Libya kuwa na uwezo unaohitajika,” alisema.

Aidha alisema kwa mara nyingine Serikali ya Libya inalaani biashara ovu ya uuzaji na usafirishaji binadamu ikiwa ni ya kimataifa au ya kikanda.

Alisema endapo kuna lililotokea kuhusu hilo la wahamiaji, basi itakuwa jambo alilolitenda mtu binafsi na wala si suala la kuratibiwa.

“Sisi tunalikana na kulilaani vikali kwa imani kwamba kushughulikia suala la wahamiaji ni lazima kuwe ni kwa kuzingatia heshima yao kama wanadamu.

“Serikali ya Umoja wa Kitaifa inawahakikishia kuwapo kwa mahusiano ya kindugu baina ya Walibya na ndugu zao Waafrika, ambao kwa karne nenda rudi wamekuwa wakiunganishwa na mashikamano ya urafiki na kuwa malengo yanayofanana,” alisema.

USHUHUDA WA ALIYEWAHI KUUZWA

Harun Ahmed, ni mmoja tu kati ya maelfu ya vijana kutoka Ethiopia ambao wamejaribu kufunga safari ndefu kupitia jangwa la Sahara hadi Libya, lengo lao kuu likiwa kufika Ulaya.

Kijana huyo mwenye miaka 27 ambaye sasa anaishi Ujerumani, amenukuliwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), akieleza jinsi alivyonunuliwa na kuuzwa mara tatu na wafanyabiashara ya kuuza watumwa.

Alisema kuna wakati alizuiliwa miezi kadha na waliokuwa wamemteka, akateswa na hata kunyimwa chakula.

“Nilizaliwa Wilaya ya Agarfa katika eneo la Bale, Jimbo la Oromia nchini Ethiopia, niliondoka Ethiopia kwenda Sudan mwaka 2013.

“Baada ya kuishi mwaka mmoja na miezi kadhaa Sudan, nilianza safari kwenda Libya nikiwa na wahamiaji wengine – tulilipa dola 600 kila mmoja kwa waliokuwa wanatusafirisha. Tulikuwa watu 98 kwenye lori.

“Tulisafiri kwa siku sita katika jangwa la Sahara na tukafika eneo moja katika mpaka wa Misri, Libya na Chad ambako wanaowasafirisha wahamiaji hubadilishana wahamiaji.

“Katika eneo hilo la mpakani, kundi la majambazi lilituteka nyara wote na kutupeleka Chad. Walitusafirisha kwa siku mbili jangwani na kutupeleka hadi kwenye kambi yao.

“Walikuwa na silaha kali. Na walizungumza Kiarabu na lugha nyingine. Walileta gari na kusema kwamba wale miongoni mwetu ambao wangelipa dola 4,000 kila mmoja wangeweza kupata fursa ya kuingia kwenye gari hilo.

“Lakini wale ambao hawangeweza, wangesalia humo kambini. Hatukuwa na pesa hizo, lakini tulizungumza wenyewe na kuamua kwamba tujifanye kwamba tulikuwa na pesa hizo tupate fursa ya kuingia kwenye gari hilo.

“Tulisafiri kwa siku nyingine tatu na kufika eneo ambalo huwa wanawauza wahamiaji,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles