24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Utata kifo cha Mungai, Adaiwa kutapika hadi mauti yanamkuta

MWANASIASA mkongwe na waziri wa zamani wa Serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne, Joseph Mungai.
MWANASIASA mkongwe na waziri wa zamani wa Serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne, Joseph Mungai.

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SAALAM

MWANASIASA mkongwe na waziri wa zamani wa Serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne, Joseph Mungai, amefariki dunia.

Mungai aliyezaliwa Oktoba 24,1943 alifariki dunia   Dar es Saalam  jana baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Taarifa za kifo cha kiongozi huyo mstaafu, zilianza kusambaa kupitia mitandao mbalimbali ya  jamii jana saa 12 join.

Akizungumza na MTANZANIA jana, mtoto wa marehemu, William Mungai, alisema baba yake alifariki dunia wakati akipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.

Alisema kabla ya kifo hicho baba yake alianza kulalamika kuumwa na tumbo na kutapika ambako alipelekwa katika hospitali moja ambayo hakutaka kuitaja.

Alisema baada ya kufikishwa hospitalini hapo, hali yake ilizidi kubadilika na kuwa mbaya zaidi na hivyo wakaamua kumkimbiza Muhimbili kwa matibabu zaidi.

“Ni kweli baba amefariki dunia saa 10 jioni leo (jana) wakati tukimpeleka Muhimbili baada ya kulalamika kuumwa na tumbo. Hivi tunavyoongea, ndiyo tunatoka Muhimbili ila taarifa zaidi tutawapatia baada ya kikao cha ndugu,” alisema William kwa kifupi.

Ingawa William hakutaka kuzungumzia kifo hicho kwa undani, taarifa zilizopatikana na ambazo hazijathibitishwa, zinasema kiongozi huyo alikunywa kinywaji katika hoteli moja maarufu ya  Dar es Salaam.

Watu walio karibu na familia ya Mungai walilieleza MTANZANIA, kuwa, jana mchana Mungai alikuwa katika hoteli hiyo iliyopo Msasani akipata kinywaji kwa kuwa alikuwa na mazoea ya kufika mahali hapo.

“Mzee jana alikuwa katika hoteli ya (anaitaja) akiendelea na kinywaji akipendacho cha whisky. Inasemekana baada ya kutoka hotelini hapo na kurudi nyumbani kwake, alianza kutapika huku akilalamika kusikia maumivu makali ya tumbo.

“Vijana wake walimpeleka hospitali ya karibu, lakini hali ilizidi kuwa mbaya ndipo familia iliamua kumkimbiza Muhimbili ambako aliaga dunia,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Mkuu wa Kitengo cha  Mawasiliano  ya Umma na Huduma kwa Wateja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, aliiambia MTANZANIA kwa simu, kuwa walipokea mwili wa marehemu katika idara ya magonjwa ya dharura jana saa 11.20 jioni.

Mungai  aliwahi kuwa Mbunge wa Mufindi kupitia CCM kwa miaka 35.

Pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini enzi za utawala wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na pia katika awamu za pili, tatu na nne.

Baadhi ya nyadhifa alizowahi kushika kwa nyakati tofauti ni uwaziri wa iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Pamoja na hayo, hivi karibuni wakati Rais Dk. John Magufuli akiwa katika ziara ya kiserikali nchini Kenya, alikaririwa akisema Mungani pamoja na kwamba ni mtanzania aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, asili yake ni Kenya.

Moja ya tukio kubwa la kukumbukwa katika utawala wake, Mungai alifuta Umoja wa Michezo wa Shule za Msingi (UMISHUMITA) na Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari (UMISETA), kitendo kilicholalamikiwa na wadau wengi wakati huo.

Wabunge

Baadhi ya wabunge wa majimbo ya Mkoa wa Iringa wakizungumzia kuhusu taarifa za kifo cha  Mungai, walielezwa kusikitishwa na taarifa hizo huku kila mmoja akisema alikuwa kiongozi mkweli aliyesimamia alilokuwa analiamini.

Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Oscar Chumi(CCM), alisema wana Mufindi wamepata pigo kubwa la kuondokewa na mtu aliyekuwa nguzo yao.

“Tutamkumbuka kwa mambo mengi ambayo leo hii siwezi kuyaelezea yote. Huyu ndiye aliyekuwa mwanzishi wa taasisi ya Mufindi Education Trust (MET) ambayo ilisaidia mno vijana wengi kupata elimu ya msingi.

“Kutokana na hali hiyo, mpango huu ulizalisha wasomi wengi ambao hivi sasa wako serikalini wakiwa na nyadhifa kubwa,”alisema Chumi.

Alisema alitumia uwezo wake wote kuwahamasisha wananchi katika shughuli nyingi za maendeleo, jambo ambalo sasa matunda yake tunayaona.

Alisema marehemu Mungai atakumbukwa kwa kuazisha Benki ya Wananchi wa Mufindi ambayo ilikuwa ya kwanza nchini.

“Kama kuna urithi katuachia basi ni benki hii, maana ndiyo ya kwanza nchini na Vicoba kwa wajasiriamali wadogo wadogo,”alisema Chumi.

Alisema jambo jingine ni uanzishaji wa Kiwanda cha Chai Bora na kile cha pareto ambavyo vimekuwa na manufaa makubwa kwa Mkoa wa Iringa.

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema Mungai alikuwa kiongozi wa wazi asiyegopa kusimamia ukweli.

Alisema amepokea kwa mshtuko taarifa ya msiba huo  na  kubainisha kuwa alimfahamu Mungai akiwa nje ya ulingo wa siasa.

“Alikuwa kiongozi mzuri tangu uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Ametoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi yetu, tunapaswa kuenzi yale mazuri waliyoyafanya na sisi tunaanzia pale  alipoishia.

“Alikuwa kiongozi muwazi na alituunga mkono wapinzani ingawa hakushinda… kwa ujumla alikuwa mtu mkweli asiyefungamana na siasa za upande wowote,” alisema Msigwa.

Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto (CCM), alisema ni dhahiri Taifa limempoteza kiongozi shupavu na kiunganishi katika siasa za sasa za ushindani.

“Niseme kwa kweli nimesikitishwa sana na hizo taarifa kwa sababu alikuwa mtu anayejua siasa.

“Alianza kuwa kiongozi akiwa na umri mdogo kuliko wanasiasa wote wa Mkoa wa Iringa wakati huo, lakini pia alikuwa kiunganishi pale kunapotokea misuguano yoyote,” alisema.

Alisema atakumbukwa kwa kuanzisha Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES).

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles