24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

UTAPELI MKUBWA SEKTA YA UTALII

 *Ngorongoro, TANAPA zapoteza mabilioni ya fedha


Na Masyaga Matinyi, Arusha

MAMLAKA ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) zimekuwa zikipoteza mabilioni ya shilingi kwa mwaka  kutokana na udanganyifu unaofanywa na kampuni za utalii kwa kushirikiana na askari wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Arusha.

Udanganyifu huo unafanywa kwa kubadilisha uzito wa gari tupu (tare weight) kwenye nakala ya kadi ya gari (certified copy) tofauti na uzito  kwenye kadi halisi (original card), hivyo kukwepa kulipa tozo zilizowekwa kwa mujibu wa sheria kulingana na uzito wa gari.

Mabadiliko hayo ya uzito hufanyika baada ya gari zinazobeba watalii, nyingi zikiwa “Toyota Landcruiser” (station wagon), kupelekwa katika karakana na kuongezwa urefu (uwezo wa kubeba abiria na mizigo),   baada ya kuingizwa nchini,   kuzifanya ziwe bora zaidi katika kutoa huduma.

Kwa mujibu wa utaratibu, magari yote yanayoingia NCAA na TANAPA yanapaswa kulipa tozo kulingana na uzito wa gari.

Gari tupu lenye uzito usiozidi kilogramu 2,000 hulipa Sh 20,000 na yale yenye uzito kuanzia kilogramu 2,001 hadi 3,000 hutakiwa kulipa Sh 35,000 kabla ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Baada ya kujumlisha VAT ambayo ni asilimia 18, gari lenye uzito usiozidi kilogramu 2,000 linatakiwa kulipa Sh 23,600, na kuanzia kilogramu 2001 hadi 3,000 hulipa Sh 41,300.

Kutokana na udanganyifu huo, Serikali kwa maana ya   NCAA na TANAPA hupoteza Sh 17,700 kwa kila gari linaloingia katika hifadhi hizo kila siku.

Kwa mujibu wa taratibu, gari linapoingia katika hifadhi na kukaa na wageni mathalan kwa siku tano, linapaswa kulipa tozo kwa kila siku linapokuwa ndani ya hifadhi.

Miongoni mwa kampuni kubwa za utalii zinazodaiwa zinajihusisha na udanganyifu huo (jina linahifadhiwa kwa sasa) inamilikiwa na mmoja wa viongozi  wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO).

Alipoulizwa kuhusu tuhuma za udanganyifu unaofanywa na kampuni yake kwa njia ya simu, mmiliki huyo alisema hakuna udanganyifu wowote kwa sababu magari yake hukaguliwa na kupimwa upya uzito na wakaguzi wa polisi.

“Si kweli, hayo yote ni maneno tu, everything is clear…magari yangu yamefuata taratibu zote,  na   baada ya kujiridhisha ndipo polisi wakawaandikia TRA kwa ajili ya kufanya marekebisho ya uzito wa magari,” alisema.

Jitihada za kuonana ana kwa ana na mmiliki huyo hazikuzaa matunda kwa vile alikuwa nje ya Jiji la Arusha, lakini alitoa maelekezo kwa Mtanzania kufika ofisini kwake   kupata vielelezo na maelezo ya kina kutoka kwa ofisa wake wa kitengo cha rasilimali watu.

Mtanzania lilifika na  a kuonana na ofisa huyo  lakini baada ya kuonyeshwa baadhi ya vielelezo, hakuwa na majibu yenye kujitoshelezana  alikiri kuwa mambo mengine hayafahamu.

Utapeli unavyofanyika:

Wamiliki wa kampuni za utalii baada ya kununua magari hayo ambayo mengi huingizwa nchini kutoka Japan, huyapeleka kwenye karakana zilizopo mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na kuyafanyia marekebisho.

Marekebisho hayo hubadili muundo wa gari na kuyafanya kuwa na uwezo wa kubeba abiria tisa, huku kila abiria akiwa kwenye kiti chake kwa nafasi. Vilevile yanakuwa na uwezo wa kubeba mizigo ya abiria husika.

Baada ya magari hayo kubadilishwa, wamiliki kwa kuwatumia mawakala au wafanyakazi wao, huwafuata  polisi wa kikosi cha usalama barabarani wanaokagua magari (vehicle inspectors) ambao huwajazia fomu inayoitwa “Vehicle Inspection Report D” kinyume cha sheria na taratibu.

Katika fomu hizo ambazo Mtanzania imeona nakala zake, wakaguzi hao wa magari huandika mapendekezo kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha, wakiomba uzito wa magari ubadilishwe, ilhali hawana mamlaka hayo katika sheria.

Baada ya kupokea fomu hizo, TRA mkaoni Arusha hukibadilisha uzito wa magari hayo kwa mujibu wa maelekezo ya  polisi hao.

Uchunguzi zaidi umebaini kuwa  baadhi ya askari wanaoshiriki kwenye udanganyifu huo wakati mwingine hujaza fomu hizo bila hata kuyaona magari husika.

Baadhi ya kadi za magari ambayo yanadiwa kubadilishwa uzito na kuikosesha Serikali mapato ni   namba T222 CMP, T214 CMP, T210 CMQ, T203 CMQ, T188 CMQ, T191 CMQ, T197 CMQ, T190 CMQ na T210 AQH.

Mengine ni T227 CMP, T201 CMQ, T222 CMP, T218 CMP, T210 CMQ, T796 CMW na T214 CMQ. Baadhi ya magari yameshushwa uzito hadi   kilo 1550 kutoka kilo 2090.

Wakala wa Vipimo na Mizani wazungumza:

Akizungumzia suala hilo, Meneja wa Mkoa wa Wakala wa Vipimo na Mizani, Dunford Manzi, alisema kuwa na magari yenye taarifa za uongo kuhusiana na uzito wake, ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo.

Alisema  hakuna gari lolote linalofanya biashara ya utalii ambalo limewahi kupelekwa hapo kuhakikiwa uzito wake.

Katika majibu yake ya maandishi kwa Mtanzania, ambayo nakala zimepelekwa kwa Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Manzi alisema;

“Kuwa na gari yenye taarifa za uongo kuhusu uzito wake (false declaration of weight, contrary to section 42 of Weights and Measures Act, Cap 340) ni kosa chini ya Sheria za Vipimo.

 

“Kwa kuwa Wakala wa Vipimo ndiyo taasisi pekee ya Serikali yenye mamlaka ya  sheria ya kuthibitisha   uzito, ujazo, urefu, unene, kasi n.k wa kitu chochote.

“Nawashauri  wamiliki wote wa magari yaliyoongezwa/kupunguzwa na kuathiri uzito wafike Ofisi ya Wakala wa Vipimo (kwa Arusha tupo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Na. 70), kuthibitisha/kutambua uzito mpya.

“Mamlaka ya Mapato (TRA) wawaelekeze wamiliki wa magari yaliyoongezwa au kupunguzwa wafike Wakala wa Vipimo kuthibitisha/kutambua uzito mpya ili wabadilishiwe kwenye kadi za gari.

“Askari wa Usalama Barabarani wawabane walioongeza au kubadili magari bila kurekebisha kadi, mamlaka nyingine zote (TANAPA, NCAA n.k) zisitambue uzito ulioandikwa kwenye kadi ya gari kama haujarekebishwa baada ya gari kufanyiwa mabadiliko”.

 

Makadirio yasiyo rasmi ya upotevu wa fedha:

Katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara kuna kampuni za utalii zisizopungua 350 na inakadiriwa kuna magari yanayofanya biashara ya utalii zaidi ya 3,000.

 

Kwa  udanganyifu unaoendelea kufanyika  maana yake ni kuwa gari ambalo linapaswa kulipa Sh 41,300, linalipa Sh 23,600, hivyo kutolipa Sh 17,700.

Hivyo, mathalan magari 500 kwa mwaka yanaikosesha Serikali mapato ya Sh bilioni 6.372  kwa maana ya 500x 360 siku za mwaka x 17,700 x mashirika 2 yaani NCAA na TANAPA.

 

NCAA, TANAPA washitushwa

Akizungumzia suala hilo, Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Dk. Fred Manongi, alisema hana taarifa za udanganyifu huo kwa sababu  anaamini kadi za magari ni nyaraka ambazo zinatayarishwa na asasi nyingine za umma, hivyo mamlaka hufuata kilichopo kwenye kadi.

“Hiyo taarifa tumeipokea na tutaifanyia kazi, ikiwamo kuwasiliana na mamlaka nyingine zinazohusika   kubaini ukweli na kuchukua hatua stahiki,” alisema.

Meneja Mawasiliano wa TANAPA, Paschal Shelutete alisema: “Hilo hatulifahamu ingawaje kama ilivyo kwa upande wa Ngorongoro, nasi pia tunatoza tozo kutokana na uzito wa gari   linapoingia hifadhini.

 

“Lakini kama ni kweli kuna mchezo huu mchafu unaofanywa na kampuni za utalii, basi tutachunguza na kuchukua hatua  mapato ya Serikali yasiendelee kupotea. Pia tunaamini vyombo vya dola vitafanya kazi yake  kujua ukweli”.

 

Kamanda wa Polisi Arusha

Alipoulizwa kwa njia ya simu akiwa wilayani Ngorongoro, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema yeye hausiki na masuala ya kodi  na akaelekeza TRA ndiyo waulizwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles