MWANDISHI WETU
UTAMADUNI wa wanawake kubana misuli ya uke umekuwa ukifanywa na jamii nyingi barani Afrika kwa miaka mingi. Katika pwani ya Afrika Mashariki hasa jamii ya Waswahili wamekuwa wakipokezana utamaduni huu kutoka kizazi kimoja hadi kingine lakini katika miaka ya hivi karibuni hasa katika miji mikuu kama vile Mombasa, Kenya, Dar es Salaam na Tanga kwa upande wa Tanzania, wanawake wamekuwa wakitumia mbinu nyingine ambazo ni za kisasa japo huenda zikahatarisha maisha yao.
Ukipita mtaa wa Likoni jijini Mombasa, pwani ya Kenya, utamaduni huu wa wanawake kubana njia zao za uzazi si geni.
Kwa upande wa Tanga, wasichana wamekuwa wakifundishwa kabisa na wakubwa wao namna ya kubana njia zao za uzazi.
Munira Ali, ni mkazi wa Mombasa, anasema anaelewa faida zake na wanachotumia zaidi kwa shughuli hiyo wenyewe wanaita shabu.
”Hii shabu husaidia maana yake kuna wengine humwaga maji mengi. Sasa hii shabu ukitia huko, humfanya mtu kuwa mkavu halafu huvuta na kubana,” anasema Munira.
Hiki ndio hasa kinachowahangaisha wanawake hawa wa Mombasa, baadhi yao wana wasiwasi kuwa uke wao ni mpana kiasi kwamba hawawatoshelezi waume wao.
Ndio maana wanatumia shabu ili kujaribu kubana na kurudisha ile hali ya zamani.
Lakini hapa mbinu wanazo tumia zinahusisha bidhaa za kemikali wanazonunua dukani.
”Hii ndio shabu na kazi yake ni kuchukua hiki kipande unaponda kisha unafunga kwenye pamba. Na unachanganya na mafuta mazito yenye harufu nzuri mfano manukato ya udi. Sasa hiyo inasaidia ukitia huku chini shabu inavuta,” anasema Munira.
Wanawake hawa pia wameelezea hofu yao kuwa wanaume huenda wakawaacha au kuwatafutia mke wa pili iwapo hawatawaridhisha kimapenzi. Yote haya wamejifunza kutoka kwa makungwi ambao huwapa ushauri nasaha wasichana wanapo olewa, kuhusu njia za kumridhisha mume.
Mbali na shabu ambayo inatengenezwa kwa chumvi, kuna bidhaa nyingi zinazopatikana madukani kama vile choki, inayotengenezwa kutokana na chokaa maalum yenye kemikali inayoaminiwa kuvuta misuli ya uke na kubana.
MADHARA YAKE
Bidhaa hizi wanazonunua hawajui zimetokana na nini na wala hazina maelezo ya namna ya kutumia. Pia hakuna ushauri wa daktari wala hawana hofu kuhusu madhara yanayoweza kujitokeza hapo baadae.
Daktari Kinuthia Muriu, ni mtaalamu wa afya ya uzazi, anasema matumizi ya bidhaa hizi yapo miongoni mwa wanawake.
”Kwa makabila fulani huwa wana njia nyingi wanazotumia kubana njia ya uzazi, nyingine ni mbaya, huweka hadi chumvi inayounguza mwili hali ambayo baadae husababisha madhara. Kuna wale wanaopata msukumo kutoka kwa jamii, fikra zao wanaona kama wana maumbo yaliyo na shida hivyo, wanahitaji ushauri nasaha ili waweze kujikubali,” anasema daktari huyo.
Dk. Muriu anasema kuna njia mbalimbali zinazotumika kisayansi zinakubaliwa ili kuandaa mwili wa mzazi kwa mfano, wakati wa kuuandaa mwili na kurekebisha mwili kama kubana njia za uzazi na wengi hufuatilia matibabu hayo, kuna mazoezi kama yale kitaalamu yanaitwa Kegel, mazoezi yanayosaidia kurejesha maumbile ya mwanamke.
KUFUSHA SEHEMU ZA SIRI
Ukiacha hao wanaotumia shabu, wengine hutumia udi kujifusha. Utamaduni huu umeshamiri zaidi mkoani Tanga, ambapo wao bila udi maisha hayaendi.
Mara nyingi binti anapotaka kuolewa, basi atafundishwa namna ya kujifukiza ili kuweka harufu nzuri ukeni na kuufanya ubane kwa lengo la kumridhisha mwanamume.
Hata hivyo, madaktari wa magonjwa ya wanawake wanaonya kuhusu suala hili, kwani mvuke wa moto huingia sehemu za siri na hivyo unaweza kusababisha madhara.
Onyo hilo lilitolewa baada ya mwanamke mmoja kujiunguza sehemu zake za siri baada ya kutumia mvuke wa maji kufusha sehemu za siri.
Mwanamke huyo alikuwa na tatizo la kubadilika muundo wa maumbile ya sehemu zake za siri, kitaalamu wanaita ‘prolapsed vagina’ na kuamini kuwa tiba hiyo itamfanya akwepe kufanyiwa upasuaji.
Kufusha kwa mvuke sehemu za siri, kitendo ambacho uhusisha kukaa kwenye chombo chenye maji ya moto chenye mchanganyiko wa maji na dawa na kufusha kwa kutumia udi ambapo wengi huka bila nguo na kuchukua chotezo chenye moto na kuweka udi na ule moshi wake kuulekezea kwenye sehemu za siri yamekuwa ni mambo ya kawaida na maarufu hivi sasa.
Tiba hiyo na tiba nyingine katika maeneo nyeti, imekuwa ikifanyika kwenye saluni na nyumba za Spa katika maeneo mbalimbali ya mijini.
Gazeti la La Times liliripoti tiba ya kufusha kuwa maarufu zaidi mwaka 2010.
Mwaka jana, mwanamitindo wa Kimarekani, Chrissy Teigen, pia aliweka picha yake akifanyiwa tiba ya namna hiyo.
Nyumba za Spa zimekuwa zikitangaza kutoa huduma hiyo iitwayo ‘v-steaming’ ikidaiwa kuwa imekuwa maarufu miaka mingi barani Afrika na Asia. Wanasema tiba hiyo, ambayo wakati mwingine huitwa Yoni steaming hufanyika ili kuondoa uchafu sehemu za siri.
Wataalamu hata hivyo, wanasema kuwa ni hatari na hakuna uthibitisho wowote kisayansi kuwa ni tiba yenye kufanya kazi kiafya, ikiwamo kupunguza maumivu wakati wa hedhi au kusaidia kupata watoto.
Dk. Vanessa Mackay, ambaye ni msemaji wa shule ya wataalamu wa magonjwa ya wanawake, anasema ni ‘imani’ kuwa sehemu za siri zinahitaji usafi wa hali ya juu kiasi hicho au tiba ya namna hiyo.
Anasema inashauriwa kutumia sabuni zisizo na manukato kwenye eneo la nje la maungo hayo pekee.
”Sehemu za siri za mwanamke zina vijidudu vizuri, ambavyo husaidia kulinda maungo hayo,” anaeleza katika taarifa yake.
Anasema kuzifusha sehemu za siri kunaweza kuathiri vijidudu hivyo na kusababisha kuwashwa, athari nyingine kupata maumivu mithili ya kuwaka moto, pia ngozi laini pembezoni mwa sehemu za siri inaweza kuungua au kubabuka.
Madaktari kadhaa wameeleza hadithi kuhusu mwanamke aliyepata madhara kutokana na kufusha sehemu zake.
Dokta Magali Robert, aliyeandika taarifa ya mwanamama huyo wa miaka 60 huko Canada, anasema alijaribu kufukiza sehemu zake za siri baada ya kupata ushauri wa daktari wa tiba za kienyeji wa Kichina.
Mwanamke huyo alikaa kwenye maji yaliyokuwa yamechemka kwa dakika 20 kwa siku mbili mfululizo kabla ya kujisalimisha kwa dharura baada ya kupata majeraha.
Alilazimika kuahirisha upasuaji ili kuuguza majeraha aliyoyapata.
Dk. Robert anasema taarifa hizi za kupotosha huwafikia watu kwa wingi kwenye mitandao na taarifa kutoka kwa watu.
”Watu wanaotoa huduma kwa wanawake wanapaswa kufahamu tiba mbadala ili waweze kuepuka madhara,” anaeleza.
MATIBABU BAADHI YA KLINIKI
Wataalamu wanasema ‘matibabu’ yanayotolewa na baadhi ya kliniki binafsi katika mataifa mbalimbali yakiwemo ya Uingereza na Marekani, yanaweza kumsababishia mwanamke kuungua vibaya, kupata makovu na maumivu ya mara kwa mara.
Wakati wa matibabu haya, kifaa huingizwa ndani ya uke kwa ajili ya kuchemsha kukata nyama ya uke.
Ingawa matibabu haya si ya upasuaji na yanaweza kufanyika kwa muda mfupi tu, wataalamu wanashauri kuwa ni muhimu kuwa salama.
Matibabu hayo kwa njia ya vifaa vya kuchoma seli yameidhinishwa kwa matumizi ya matibabu ya kuua seli za saratani ya mfuko wa uzazi ama nyama ya uke pamoja na masundosundo ya sehemu za siri (genital warts), lakini hayajafanyiwa vipimo vya ukarabati wa mwili.
HATARI KUBWA
Mamlaka ya viwango vya bidhaa nchini Marekani (FDA), inasema kuwa itachukua hatua iwapo wenye kuuza tiba hatari isiyo na dhihirisho la faida wataendelea kufanya hivyo.
Inasema wengi miongoni mwa waotengenezaji bidhaa hizo wamekuwa wakidai tiba hiyo inaweza kuponya maradhi na dalili zinazosababishwa na kipindi cha ukomo wa kupata mtoto (menopause), uwezo wa kudhibiti mkojo na uwezo wa kufanya tendo la ngono.
“Bidhaa hizi zina hatari kubwa na hazina ushahidi wowote wa kuithibitisha ushahidi wa matumizi yake. Tuna wasi wasi mkubwa wanawake wanadhurika,” linasema onyo la FDA.
Paul Banwell, ni daktari wa upasuaji wa kurekebisha maumbile ya mwili na mjumbe wa Jumuiya ya Madaktari wa Upasuaji wa Kurekebisha Mwili wanaokubalika anasisitiza kuhusu onyo hilo: “Kumekuwa na ongezeko kubwa la haja ya afya ya wanawake na maslahi ya kingono, pamoja na kwamba hili linapaswa kuungwa mkono, ni muhimu elimu yoyote na tiba vinavyotolewa vitolewe kwa umakini bila kuwapo upotoshaji au uchochezi wa masoko.”
Dk. Vanessa Mackay, kutoka Chuo cha Uingereza cha madaktari bingwa wa masuala ya uzazi cha Royal College of Obstetricians and Gynaecologists (RCOG), anasema: “Hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba vifaa vya ukarabati wa uke usiotumia vifaa unafaa katika kuboresha misuli ya uke ama kubadili muundo wa uke. Kama wanawake wanahofu juu ya muonekano ama mguso wa uke wao wanapaswa kuongea na wataalamu wa afya wenye taaluma.”
Wataalamu wanasisitiza kuwa ni muhimu kukumbuka kwamba kila mwanamke ana uke tofauti. Uke wa mwanamke mmoja na tofauti na wa mwanamke mwingine kama wanavyotofautiana wanawake wenyewe katika mwonekano wao wa sura na rangi.
Dk. Vanessa anasema: “Ili kuimarisha misuli inayozingira uke, wanawake wanashauriwa kujaribu mazoezi ya sehemu ya chini ya tumbo (pelvic) ya sakafuni yanayoweza kusaidia kuboresha na kuimarisha misuli na uwezo wa kupata shauku ya ngono.”
Ukavu wa uke ni jambo la kawaida lakini ni tatizo linaloweza kutibiwa ambalo wanawake wengi wanalipitia wakati mmoja maishani mwao.
Unaweza usababishwa na mambo kadhaa ikiwamo kufukia kipindi cha ukomo wa hedhi – menopause, kunyonyesha, uzazi, kutopata shauku kabla ya ngono na baadhi ya dawa za kuzuia mimba.
Wanawake wanashauriwa kujaribu kujisaidia wenyewe kabla ya kuwatembelea wataalamu wa afya, ikiwamo kutumia vilainishi vya uke.
Taasisi ya RCOG inasema kama tatizo litaendelea, daktari anaweza kumpatia dawa ya vichocheo vya mwili (hormone) kwa ajili ya uke inayofahamika kama oestrogen.