26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Tutaiboresha Bonyokwa ilingane na kata zingine – Bonnah

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli amesema kata ya Bonyokwa tayari imeingizwa kwenye mradi wa uboreshaji miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano wakati utekelezaji utakapoanza.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya ofisi ya Serikali ya Mtaa Kisiwani, Bonnah amesema kata hiyo ambayo ni mpya ina changamoto kubwa za miundombinu na kwamba kipaumbele ni kuiwezesha iwe na barabara za lami hadi kwenye mitaa.

“Sasa hivi kipaumbele chetu tunataka tuweke barabara za lami tuiboreshe hii kata iweze kulingana na kata zingine. Bonyokwa tunataka ibadilike tupate barabara hata tano na taa,” amesema Bonnah.

Mbunge huyo pia alikagua eneo kitakapojengwa kituo cha polisi na kuwaomba wananchi kujitolea kushiriki katika ujenzi huo ili iwe rahisi kwa Serikali na wadau wengine kuwaunga mkono.

“Kata yetu inahitaji ipate kituo cha polisi kwa sababu kilichopo kiko mbali hadi Stakishari hivyo, naomba wananchi tujumuike katika ujenzi, unaweza ukawa huna fedha lakini ukaja kusogeza tofali…wadau hawawezi kufanya kitu kabla wenyewe hatujaanza,” amesema.

Aidha ameishukuru familia ya Emmanuel Ole iliyotoa eneo hilo na tofali 1,500 pamoja na uongozi wa Hospitali ya Harmony Memorial iliyopo Bonyokwa ambao nao umeahidi kutoa tofali 1,000 na saruji mifuko 50.

Naye Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumike Malilo, amesema barabara inayoelekea katika Zahanati ya Bonyokwa tayari imeanza kukarabatiwa na Tarura kwa kiwango cha changarawe ambapo pia itajengwa mifereji na Sh milioni 150 zimetengwa.

Kwa upande wa sekta ya elimu Tumike amesema maabara mbili zinajengwa katika Shule ya Sekondari Bonyokwa zitakazogharimu Sh milioni 97 na kwamba Sh milioni 160 zimetengwa kufanya upanuzi wa shule hiyo ambapo wataanza kujenga ghorofa.

“Tunamshukuru mheshimiwa mbunge tumepokea Sh milioni 14 kutoka katika Mfuko wa Jimbo ambazo zitatumika kukarabati paa la zahanati yetu, barabara ya Mtaa wa Msingwa na kuweka umeme Shule ya Sekondari Bonyokwa,” amesema Tumike.

Aidha katika Shule za Msingi za Kifuru na Bonyokwa amesema kila moja imeongezewa madarasa mawili sambamba na ununuzi wa madawati na kwamba bado wanaendelea kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi mtaa wa Kisiwani.

Mmoja wa wananchi wa Mtaa wa Kisiwani Athumani Msoke, amesema kero nyingine zinazowakabili ni kukosekana kwa maji ya uhakika na gharama kubwa za urasimishaji makazi ambapo wamekuwa wakitozwa Sh 350,000 kinyume na bei elekezi ya Serikali ya Sh 150,000.

Kuhusu changamoto ya maji mwakilishi wa Dawasa Mkoa wa Kinyerezi amesema ratiba ya maji imekuwa ikibadilika kutokana na umeme kukatika katika na kuahidi kuwa hadi mwishoni mwa mwezi huu kero hiyo itaisha kwa sababu tayari wameanza kulaza mabomba makubwa ya usambazaji maji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles