27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

LHRC yalaani matukio ya ukatili kwa watoto kuongezeka nchini

Na Clara Matimo, Mwanza

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) kimeonyesha kusikitishwa na kulaani kuendelea kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto nchini huku kikishauri na kuiomba serikali kuweka mfumo sahihi wa utoaji taarifa za matukio hayo.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mwanasheria  ambaye pia ni  Mratibu wa LHRC Mkoani Dodoma, William Mtwazi, alipozungumza na MTANZANIA Digital, ambapo kauli hiyo imekuja kufuatia takwimu zilizotolewa Septemba 21 mwaka huu jijini Mwanza na Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Sebastian Kitiku, zikitaja kwamba zaidi ya watoto 9000 wamefanyiwa vitendo vya ukatili kuanzia Januari mwaka 2020 hadi Desemba kati yao 5000 wamebakwa, 3500 wamepewa mimba na 1000 wamelawitiwa.

Kitiku alitoa takwimu hizo  wakati akizungumza kwenye  kikao ambacho hufanyika  kila mwaka cha kutathmini malezi chanya ya familia katika kushughulikia masuala ya ukatili dhidi ya watoto kilichokutanisha mashirika zaidi ya 25 yanayojishughulisha kupambana na ukatili wa kijinsia kutoka  nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Uganda na Tanzania lengo likiwa ni kupata suluhu mbadala ya kutokomeza  vitendo hivyo.

Mtwazi amesema idadi hiyo ni kubwa na inatisha,  LHRC inaungana na watetezi wa haki za binadamu kulaani vitendo hivyo na kuiomba  serikali kuhakikisha mbinu zote za kisheria na kiuchunguzi zinafanyika ili kuwawajibisha wote watakaobainika walishawishi, walichochea ama kupelekea kufanyika kwa vitendo hivyo wachukuliwe sheria  iwe fundisho kwa wengine ambao wana nia ya kutenda  ukatili dhidi ya watoto.

“Watoto 9,500 kufanyiwa vitendo vya ukatili ni idadi kubwa ambayo inahuzunisha na kukatisha tamaa, watoto wa kike wanaopewa mimba wanakatisha masomo yao lakini sisi watetezi wa haki za binadamu hatupaswi kuvunjika moyo wajibu wetu ni kuielimisha jamii ili kuhakikisha vitendo hivi vinakwisha ukizingatia serikali inapambana kumaliza changamoto hii sasa badili ya kumaliza tatizo ndiyo linaongezeka.

Ukisoma ripoti zetu za haki za binadamu kwa miaka mitatu mfululizo  kuanzia mwaka 2018, 2019 na 2020 vitendo vya ukatili kwa watoto viliongezeka ikiwemo kupigwa, mimba za utotoni, kulawitiwa, kunyanyaswa na kukeketwa  wanaofanya vitendo hivyo wengi wao ni ndugu wa karibu wa watoto hao ndiyo maana huwa tunawaambia  wazazi au walezi wasiwe wakali sana kwa watoto wao wawe marafiki  wakiwa marafiki  watoto wataweza kuwaambia mambo ambayo wanafanyiwa au vishawishi wanavyopewa na hao wanaotaka kuwafanyia ukatili hata kama ni ndugu,” amesema Mtwazi na kuongeza:

“Ili tutokomeze vitendo hivyo dhidi ya watoto  tunahitaji ushirikiano wa pamoja  baina ya wazazi, walezi, jamii na serikali pia kuwepo na mfumo sahihi wa utoaji wa taarifa ambao utawalinda wale wanaotoa taarifa wasiweze kudhuriwa na waliotenda vitendo hivyo.

Mtwazi amesema ingawa ipo sheria ya mtoto ya mwaka 2009  ambayo pamoja na mambo mengine inaweka wajibu  na majukumu ya wazazi na watoto lakini mamlaka zingine za serikali ambazo zimepewa majukumu ya kuwalinda watoto kama ustawi wa jamii, jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia  wawe karibu na jamii kwa kuielimisha kuhusu madhara yatokanayo na vitendo vya ukatili kwa kundi hilo ambalo ni taifa la kesho.

“Jukumu letu kama watetezi wa haki za binadamu  ni kuhakikisha tunaendelea kuihamasisha jamii, kuielimisha na kuiomba serikali kufuatilia kwa karibu sana makuzi na malezi ya mtoto pia kuwahamasisha wazazi wawe walinzi namba moja wa watoto wao  kwa kufuatilia mienendo yao  kila sehemu wanapoenda,”amesema Mtwazi.

Rais  Mstaafu wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania (TSA), Dk. Catherine Mung’ong’o, ametaja madhara ya kiafya wanayoyapata watoto wanaofanyiwa ukatili wa kubakwa ama kulawitiwa kuwa ni kupata magonjwa ya kuambukizwa kama ukimwi, kulegea kwa misuli ya kuzuia haja kubwa na ndogo hivyo kutokwa na haja bila kujitambua pia watoto wa kike wanapokuwa wakubwa wakipata ujauzito huwalazimu kujifungua kwa njia ya upasuaji.

“Madhara  wanayoyapata watoto kutokana na kubakwa ama kulawitiwa ni makubwa sana, watoto wa  kike au wa kiume wote hupata tatizo la kulegea misuli inayozuia haja kubwa na ndogo isitoke ikilegea husababisha haja hizo zitoke bila yeye mwenyewe kujitambua mtoto wa kike akibakwa akachanika kwa kuwa amechanika bila mpangilio  hata kama akitibiwa kovu litabaki hivyo  akikuwa akipata ujauzito  wakati wa kujifungua lazima afanyiwe upasuaji hawezi kujifungua kwa njia ya kawaida. 

  “Misuli ikilegea inatibika kwa njia ya upasuaji lakini inategemea jinsi alivyopasuka kama amepasuka vibaya hata akifanyiwa upasuaji tatizo haliishi, haja kubwa na ndogo itaendelea kutoka bila yeye kujua hali hiyo inawaathiri kisaikolojia watoto wengi  kwa sababu wanatengwa na wanafunzi wenzao darasani hivyo wanashindwa kufanya vizuri kwenye mitihani baadhi wanaweza hata kukatisha masomo,”ameeleza Dk. Mung’ong’o.

Nao baadhi ya watoto akiwemo Laulian Magnusy(14), Victor Josia(14) ambao ni wanafunzi  wa shule ya sekondari mlimani iliyopo jijini Mwanza  na Angelina Enock (15), wameiomba serikali kuongeza adhabu kwa watakaobainika kufanya vitendo hivyo kwa watoto badala ya kufungwa miaka 30 wafungwe kifungo cha maisha pia ndugu watoe ushirikiano kuanzia polisi hadi mahakamani hata kama aliyetenda kosa ni ndugu wa karibu ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia hiyo ovu.

Novemba mwaka  2020 LHRC iliwaunganisha waandishi  wa habari kutoka mikoa ya kanda ya ziwa  katika mfumo wa utoaji  taarifa za ukiukwaji wa haki za binadamu kwa njia ya mtandao ujulikanao kwa jina la haki kiganjani ili waweze kuwasaidia  wananchi wanyonge wakiwemo watoto kupata msaada wa kisheria bure na haraka kupitia simu zao za mkononi lengo likiwa ni kutokomeza ukiukwaji wa haki za binadamu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles