31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Utafiti ulivyotoa matumaini kuongezeka uhai Stamigold

Na Mwandishi Wetu

 MGODI wa Stamigold Biharamulo (SBM) umeendelea kuajiri Watanzania pekee kwa uendeshaji wa shughuli mbalimbali.

Idadi kamili ya waajiriwa inafikia 468 wakiwamo wafanyakazi 222 walioajiriwa kwa mkataba, 200 walioajiriwa na watoa huduma, vibarua 28 na wanafunzi wa mafunzo 18.

Mgodi umeendelea kuchangia huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo yanayouzunguka kwa kusaidia katika nyanja za elimu, ukarabati wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo na miundombinu ya barabara pamoja na ulinzi na usalama.

 Kwa kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Juni 2019, mgodi umechangia Sh139,763,830.00 katika uendelezaji wa shughuli za jamii.

Mgodi umeendelea kuzalisha na kuuza madini ya dhahabu na madini ya fedha.

Mipango ya mgodi ni kuzalisha wastani wa wakia 1,200 kwa mwezi (sawa na wakia 14,400 kwa mwaka) ili kukidhi gharama za uendeshaji na kupata faida katika mwezi husika.

Kwa mwaka wa fedha 2018/19 mgodi ulivuka malengo kwa kuzalisha wakia 15,008.15ambapo 13,194.58zilikuwa za madini ya dhahabu na 1,813.57 za madini ya fedha zote zenye thamani ya Sh bilioni 38.4.

Katika kufanikisha uzalishaji huo, mgodi ulitumia Sh 33,558,829,900 kugharamia uendeshaji wa mtambo wa kuchenjua dhahabu, gharama za kuchimba na kusafirisha mbale (ore) na miamba bure (waste), ukarabati wa mitambo na vifaa, mishahara ya wafanyakazi na gharama nyingine za usimamizi wa mgodi.

Aidha, uongozi wa Stamigold umeendelea kupunguza gharama za uzalishaji na uendeshaji wa mgodi.

Gharama hizo zimepungua kutoka wastani wa Dola za Marekani 1,800 kwa wakia moja katika kipindi cha Januari hadi Machi 2018 na kufikia wastani wa dola 940.14 kwa wakia moja katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Juni mwaka huu.

Gharama hizi ni stahimilivu kwa kuzingatia wastani wa bei ya dhahabu katika soko la dunia ambapo katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Juni mwaka huu wakia moja ya dhahabu imeuzwa kwa wastani wa  Dola za Marekani 1,145.56.

Katika kuhakikisha kuwa kampuni inapunguza gharama zaidi katika eneo la utafiti, kampuni ilikodi mtambo wa zamani aina ya Diamond kutoka Stamico kwa uchorongaji, ambao iliufanyia marekebisho ili kusaidia katika utafiti.

Shughuli za utafiti wa madini katika leseni maalumu ya uchimbaji Na. SML157/2003 ziliendelea ambapo mgodi umeweza kubaini uwepo wa mbale za uzani wa tani 884,041 zenye grade ya 1.20g/t zenye jumla ya wakia 34,146 za dhahabu.

Kiasi hiki cha dhahabu kitaweza kuchimbwa kwa muda wa miaka miwili hivyo kuongeza muda wa uhai wa Mgodi kwa miaka miwili zaidi hadi 2021.

Mgawanyo wa Wakia za Dhahabu Katika Maeneo Yaliyofanyiwa Utafiti Ndani ya Leseni Na. SML157/2003

Na Eneo Kiasi cha Wakia
1. Pit04 2,919
2. Project08 7,328
3. Pit06 10,831
4. West-West Pit Extension 13,068
Jumla 34,146

Aidha, mgodi unaendelea kufanya utafiti zaidi na umeingia mkataba na Stamico kufanya uchorongaji wa mita 7,000 tangu Agosti mwaka huu kwa kutumia mtambo aina ya Reverse Circulation (RC).

Kutokana na uchorongaji huo, mgodi unatarajiwa kuongeza uhai wake zaidi kwa miaka mitatu hadi kufikia 2024.

Mgodi unamiliki visusu vinavyokadiriwa kufikia tani 8,600,000 vyenye wastani wa gredi ya gramu 1.15 kwa tani ambapo ni sawa na takribani wakia 200,000 za dhahabu.

Visusu hivyo vinakadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 260 na vinaweza kuchenjuliwa kwa miaka saba kulingana na tafiti mbili tofauti zilizofanyika kwa wakati tofauti ili kujiridhisha na makisio hayo.

Kwa sasa mgodi umeendelea kutafuta fedha ili kuutekeleza mradi huo.

Wakati huo huo, mgodi unaangalia uwezekano wa kumpata mbia kupitia maombi mbalimbali yaliyowasilishwa na kampuni zenye uhitaji wa kushirikiana na Stamigold katika uendelezaji wa mradi huu.

Mgodi umekamilisha ukarabati wa mtambo wa uchenjuaji wa madini ya dhahabu.

Ukarabati huo ulihusisha ubadilishwaji wa rollers, liners, lifters na conveyor belt yenye urefu wa mita 300.

Juhudi zote hizo ni katika kuboresha mtambo huo ili uweze kunyonya kiasi kikubwa cha dhahabu.

Gharama Kubwa za Nishati

Mgodi unaingia gharama kubwa za uendeshaji kutokana na matumizi ya nishati ya mafuta (diesel).

Unatumia wastani wa lita 15,000 za mafuta kwa siku ili kukamilisha shughuli za utendaji za kila siku.

Matumizi hayo ya mafuta yanaugharimu mgodi takriban Sh bilioni 1 kwa mwezi.

Uongozi wa mgodi umeendelea kufuatilia uunganishaji wa umeme wa gridi ya taifa ili kupunguza matumizi ya mafuta katika uendeshaji wa shughuli za mgodi.

Majibu ya Shirika la Umeme (Tanesco) kwa sasa ni kuwa kwa kuwa mgodi unahitaji umeme mkubwa (3.5MW) itabidi usubiri kukamilika kwa njia ya umeme wa maji toka Rusumo kwenda Geita.

Uunganishaji wa umeme unatarajiwa kupunguza gharama za ununuzi wa nishati kwa takribani Sh milioni 700 kwa mwezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles