24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Minjingu Fertilizer katika mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli

JPM alivyotoa mwanga wakulima kutumia mbolea za Minjingu

Na Mwandishi Wetu

NOVEMBA 5, Rais Dk. John Magufuli atatimiza miaka minne tangu alipokula kiapo cha kuwa Rais wa Tanzania na kuwatumikia Watanzania.

Tangu wakati wa kampeni na hata baada ya kushika madaraka, moja ya hoja kuu ya Rais Magufuli ni kuwasaidia Watanzania wanyonge.

Wanyonge hawa ambao amekuwa akiahidi kuwatumikia, wengi ni wakulima ambao ni zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wote.

Katika kuhakikisha wanyonge hawa wanafaidika na kazi za mikono yao, Serikali ya Rais Magufuli imekuwa ikisisitiza zaidi matumizi ya mbolea, hasa ya Minjingu ambayo inazalishwa nchini.

Septemba mwaka huu, wakati wa kikao cha Bunge, Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi, alisema kuna kiwango kidogo cha mboji na kwamba PH ya udongo wa jimbo lake iko chini, hivyo akaomba kupata ruzuku ya mbolea.

Katika majibu yake, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, hakusita kueleza namna ambavyo suluhilo la wakulima nchini ni mbolea ya Minjingu.

Alisema hawawezi kama Serikali kutoa ruzuku ya mbolea kwa watu wa Ukerewe peke yao, bali wanapitia sera ya kilimo ya mwaka 2013 ili kutatua changamoto zilizopo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa ofisa wa Minjingu Mines alipotembelea kiwandahicho cha kutengeneza mbolea Februari,2017.

“Kwa hatua za awali, tunaendelea kusisitiza wananchi wa Wilaya ya Ukerewe watumie mbolea za Minjingu, ambazo zitaweza kuongeza uzalishaji kwenye eneo lao,” alisema Bashe.

Bila shaka ujasiri wa kauli hiyo ya Bashe, ulitokana na msisitizo wa matumizi ya mbolea za Minjingu uliotolewa na Rais Magufuli Juni 7, mwaka huu, alipokutana na wafanyabiashara wa wilaya zote nchini kusikiliza changamoto zinazowakabili ili kuzitatua.

Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, hoja mbalimbali zilibuka, huku baadhi zikianikwa na Rais Magufuli, ikiwamo changamoto zinazoihusu Serikali katika kushughulikia masuala ya wafanyabiashara.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu (Minjingu Mines and Fertilizer Ltd – MMFL), Pardeep Singh Hans ‘Tosky’, alikuwepo na kutoa kero zinazowakabili.

Rais magufuli alimweleza mfanyabiashara huyo kuwa kuna wakati Wizara ya Kilimo (wakati wa Waziri Charles Tizeba), Serikali ilikuwa inaagiza mbolea kutoka nje na alipowauliza kwanini wasitumie mbolea ya Minjingu, alielezwa kwamba wenye kiwanda wamekataa kuuza hadi wapewe fedha za Serikali.

“Kuna wakati Wizara ya Kilimo enzi za Waziri Tizeba walikuwa wanaagiza mbolea kutoka nje, nikauliza kwanini msinunue hiyo mbolea ya Minjingu, jibu nililopewa ni kwamba wewe umekataa kuuza hiyo mbolea, ni lazima upewe kwanza ‘capital’ ya fedha za Serikali ndipo uweze kufanya ‘production’ na kuuza hiyo mbolea, ni kweli ama yalikuwa maneno ya kutengenezwa?” Rais Magufuli alimuuliza mfanyabiashara huyo.

 “Hapana mheshimiwa Rais, hayo yalikuwa ni maneno ya kutengeneza,” alijibu Tosky.

“Basi nimeelewa, nafikiri mnaweza mkaelewa, nimeuliza kwanini mkanunue mbolea nje wakati kuna mbolea pale Minjingu.

“Mkinunua mbolea ya Minjingu kwanza mtakuwa mnaongeza ‘employment opportunity’ (nafasi za ajira) kwa Watanzania, watalipa ushuru kwa sababu wana kiwanda, lakini ‘probably will be even chipper’ (labda pia itakuwa rahisi).

“Nikaambiwa yule tumemfuata amesema lazima apewe kwanza mtaji wa dola milioni kadhaa ndipo anaweza akatengeneza mbolea ya humu, nikasema mbona anatengeneza mbolea anauza, wakasema ‘amekataa yule hafai’ tununue tu kwingine nje,” alisema Rais Magufuli.

Ama kwa hakika kauli hiyo ilikuwa ni kielelezo cha namna Rais Magufuli anavyotamani kusaidia bidhaa za ndani na kuwasaidia Watanzania kupata ajira za uhakika.

CHIMBUKO LA MINJINGU

Machimbo ya mwamba wa Minjingu yapo katika Kijiji cha Minjingu kilichopo kilometa 106, Barabara ya Arusha – Manyara, Kusini Magharibi mwa Jiji la Arusha. Yaligunduliwa mwaka 1956.

Ghala la mbolea la kiwanda cha Minjingu

Bidhaa iliyopatikana katika machimbo haya, awali ilitumika kama malighafi ya kuzalisha mbolea za aina ya SSP na TSP katika Kiwanda cha Mbolea, jijini Tanga cha Tanzania Fertilizer Company – TFC.

Kiwanda cha TFC kilifungwa mwaka 1990 na mwaka 2001 Serikali ikaibinafsisha kwa MMFL kampuni yake ya Minjingu Phosphate Company (MIPCO) iliyoianzisha kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Kiwanda cha MMFL kilianza kutengeneza mbolea zenye mfumo wa punje mwaka 2008, na kufikia mwaka 2011 kikawa kinatengeneza mbolea zenye viwango tofauti vya virutubisho vinavyokidhi mahitaji ya udongo na mimea husika.

 Kwa sasa, Kiwanda cha MMFL kina uwezo wa kuchimba na kuchakata tani 500,000 za madini ya ‘fosfeti’ kwa mwaka.

Aidha, kina uwezo wa kutengeneza mbolea za aina mbalimbali kiasi cha tani 150,000 kwa mwaka.

Vile vile, kuna kiasi cha tani milioni 50 za machimbo ya fosfeti ambayo yanaweza kuzalisha mbolea kwa kipindi cha miaka 50 – 100 ijayo.

 Kiwanda pia kinaendelea kupanua wigo wa uzalishaji wa mbolea itakayokidhi mahitaji ya wakulima hapa nchini na majirani zetu katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati kwa kuingiza mitambo mipya na ya kisasa.

Machimbo ya Minjingu yana madini ya fosfeti ya asili ambayo huyeyuka mara moja inapowekwa katika udongo wenye kiwango kikubwa na cha wastani cha asidi.

Sifa hii inafanya fosfeti ya Minjingu iwe tofauti na nyingine zilizosaidiwa viwandani.

Mazao yalivyostawi kutokana na matumizi ya Mbolea ya Minjingu

Fosfeti ya Minjingu huchimbwa, huchakatwa na kutengeneza mbolea ya kupandia na kukuzia za aina mbalimbali zikiwemo za Nafaka Plus, Top dressing, Golden Leaf Tobacco, Minjingu Chai na Minjingu Organic Hyper Phosphate (MOHP).

Mbolea zote zilizotajwa ziko katika mfumo wa punje na hivyo kumrahisishia mtumiaji wakati wa kuziweka shambani.

Hivyo inashauriwa wakulima wazitumie kwa madhumuni ya kuongeza uzalishaji wenye tija wa mazao ya kilimo na kulinda udongo wa nchi yetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,476FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles