Na AVELINE KITOMARY
MATUMIZI ya tumbaku yanatajwa na wataalamu wa afya kuwa hatari zaidi kutokana na athari mbaya ambazo mtumiaji anaweza kuzipata.
Tumbaku ina sumu aina ya ‘Nicotine’ ambayo ina zaidi ya kemikali 4,000, hizi huweza kuathiri sehemu mbalimbali ya mwili hivyo kila baada ya sekunde nne mtu mmoja hufariki kutokana na matumizi ya tumbaku.
Kutokana na tumbaku kuweza kusababisha madhara ya kiafya, hali hiyo husababisha maisha ya watumiaji kuwa mafupi zaidi kuliko wasiotumia.
Madhara ya tumbaku ni pamoja na ugonjwa wa moyo, saratani, magonjwa ya mapafu, vidonda vya tumbo, ngozi kujikunja, magonjwa ya meno, magonjwa ya mifupa na mengineyo.
Kemikali za tumbaku huweza kusababisha aina mbalimbali za saratani kama vile saratani ya koromeo, mapafu, ngozi, mdomo na ulimi.
Matumizi ya tumbaku pia husababisha magonjwa ya moyo, kutokana na kufanya moyo kwenda mbio na hivyo kuongeza msukumo wa damu mwilini (high blood pressure), hali hiyo husababisha mshtuko wa moyo na hata kifo.
Madhara mengine ni kemikali hizo kupunguza uwezo wa misuli kujishikilia vizuri kwenye mifupa pia ngozi kujirekebisha hivyo basi, ngozi huzeeka haraka na kupoteza uwezo wa kulainika, mtumiaji huonekana mzee kuliko umri wake.
TAKWIMU ZA MATUMIZI YA TUMBAKU
Siku ya kutokuvuta tumbaku huadhimishwa kila ifikapo Mei 31 kila mwaka, lengo ni kukuza uelewa wa watu kuhusu madhara ya matumizi ya zao hilo.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), linaeleza kuwa kila mwaka kampuni ya bidhaa za tumbaku huwekeza zaidi ya dola bilioni tisa za Marekani kutangaza bidhaa zake zaidi ikiwalenga vijana kwa nia ya kujaza nafasi ya watu milioni nane ambao bidhaa hiyo inawaua kila mwaka.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya tangu mwaka 2000 hadi 2025 inaonesha kupungua kwa idadi ya watu wanaotumia tumbaku duniani kutoka watu bilioni 1.39 mwaka 2000 hadi bilioni 1.37, watu takribani milioni mbili wameacha matumizi ya tumbaku.
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa Bara la Afrika lina kiwango cha chini zaidi ya matumizi ya tumbaku ikilinganishwa na mabara mengine.
Mwaka 2000, taarifa ya WHO ilionesha watumiaji wa tumbaku Afrika walikuwa ni asilimia 18.5 ikilinganishwa na kiwango cha juu kilichorekodiwa kwa Bara la Asia ya Kusini cha asilimia 47, hii inaonesha kuwa bado kuna kiwango kidogo cha matumizi.
Hii imetokana na jitihada zinazofanywa na serikali za nchi mbalimbali katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara za matumizi ya tumbaku.
MATUMIZI YA TUMBAKU NA ATHARI ZA KIUCHUMI
Juni 2, mwaka huu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ilizindua utafiti mdogo wenye malengo matano ikiwamo ya kutoa taarifa za kiwango cha matumizi ya tumbaku hapa nchini.
Katika utafiti huo, taarifa zilizolengwa kutolewa ni za watu wazima ikijumuisha tathimini ya matumizi ya tumbaku, kutathmini watu waliojaribu kuacha matumizi ya tumbaku.
Utafiti huo pia umelenga kujua kiwago cha athari ya tumbaku kwa watu wasiotumia kwani kuna watu hawatumii sigara lakini wanaathirika, pia kujua gharama za matumizi ya tumbaku kwa mwezi kwa kila mtumiaji.
Lengo lingine ni ufikiwaji wa taarifa ya madhara ya tumbaku kwa wananchi huku wakiangalia zaidi elimu ya matumizi ya tumbaku na ni wananchi wangapi wanapata taarifa kupitia njia mbalimbali na kupima uelewa na mtazamo wa jamii kuhusu madhara yake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti huo ulioanza mwaka 2018, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema Tanzania kama nchi nyingine za Kiafrika wavutaji wa tumbaku wako hatarini kuyumba kiuchumi na kupata magonjwa yasiyoambukizwa kama tahadhari hazitachukuliwa mapema.
Ummy anasema utafiti huo umeonesha kuwa kwa wastani matumizi ya tumbaku kwa mtu mmoja kwa mwezi inagharimu kiasi cha Sh 28,840.
“Hizo fedha ambayo zimetumika kununulia tumbaku ingetosha kupunguza kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kwa mtu mmoja kwa mwezi kwa asilimia 58 na umaskini wa kupindukia wa uhitaji wa chakula kwa mtu mmoja mmoja kwa mwezi kwa asilimia 85.
“Kwa kutumia taarifa za Matokeo ya Viashiria Muhimu vya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya binafsi kwa Tanzania Bara wa mwaka 2017/18, fedha za kujikimu kwa ajili ya mahitaji ya msingi kwa mwezi kwa mtu mmoja ni Sh 49,320 na mahitaji ya chakula kwa mwezi kwa mtu mmoja ni Sh 33,748,” anasema Ummy.
Kwa mujibu wa utafiti huo, matokeo yameonesha kuwa mtu mmoja kati ya 10 anatumia tumbaku na katika kila Watanzania 100 watu nane wanatumia tumbaku sawa na asilimia 8.7.
Ufiti huo pia umeonesha kuwa watu wenye umri wa miaka 15 au zaidi nchini Tanzania wanatumia tumbaku ya aina yeyote na hivyo kufanya nchi kuwa na watu milioni 2.6 wanaotumia zao la tumbaku kati ya watu zaidi ya milioni 55, katika idadi hiyo wanaume ni asilimia 14.6 huku wanawake ni asilimia 3.2.
UELEWA WA JAMII
Katika mabango mbalimbali, pakiti za sigara, mitandao ya kijamii, pia vyombo vya habari matangazo yamewekwa ili kuwatahadharisha watumiaji kuwa bidhaa za tumbaku ni hatari kwa afya.
Ingawa uelewa wa madhara ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja haujawekwa wazi kama ilivyo afya lakini utafiti umebaini kuwa yapo.
Ummy anasema watu wanne kati ya 10 ambao ni sawa na asilimia 40.3 nchini wamewahi kuona onyo la matumizi ya tumbaku kupitia redio au runinga.
Anasema matokeo ya utafiti yameonesha kuwa watu tisa kati ya 10 sawa na asilimia 92.3 wenye umri wa miaka 15 au zaidi wanaamini uvutaji wa sigara husababisha magonjwa, wakati watu wanane kati ya 10 sawa na asilimia 84.4 wanaamini kuvuta hewa ya mtu anayevuta sigara kunaweza kuwasababishia magonjwa hata kama wao hawavuti sigara.
“Katika kipindi cha miezi 12 iliyopita taarifa inaonesha kuwa watu wanne kati ya 10 sawa na asilimia 32.9 wameathiriwa na moshi wa tumbaku sehemu za kazi, ikiongozwa na sehemu za mabaa na kumbi za starehe kwa asilimia 77 sawa na watu milioni tatu, maeneo ya huduma za biashara za vyakula asilimia 31.1 sawa na watu milioni 3.5 na majumbani asilimia 13.8 sawa na watu milioni 4.1,” anabainisha Ummy kupitia utafiti huo.
Anasema utafiti huo una umuhimu wa kipekee katika wizara yake kwani matokeo yake yatasaidia katika kutathmini hatua zilizofikiwa katika kupambana na magonjwa makuu manne yasiyoambukiza ambayo ni saratani, magonjwa ya moyo, magonjwa ya mfumo wa hewa na kisukari.
MIKAKATI YA UDHIBITI
Katika kuhakikisha elimu dhidi ya athari ya tumbaku inaifikia jamii ipasavyo, Ummy anatoa maelekezo kwa watendaji wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na wadau wengine, kutengeneza au kupitia upya sheria ya kudhibiti matumizi ya tumbaku ili iendane na Mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara yake.
“Wizara ya Elimu inaendelea kuimarisha juhudi za kuwakinga wanafunzi dhidi ya tumbaku na bidhaa zake, Wizara ya Mambo ya Ndani kuhakikisha wale wanaokiuka miongozo kama vile kuendelea kuvuta sigara kwenye maeneo ya wazi wanachukuliwa hatua stahiki.
“Watengenezaji na wauzaji wa sigara wafuate miongozo iliyowekwa na Serikali ikiwamo kutokuweka mabango au kutangaza na kuhamasisha matumizi ya sigara, kupitia bidhaa kama miamvuli, T-shirts, kofia na kutowauzia watoto wenye umri chini ya miaka 18.
“Jamii kuacha kutumia tumbaku na bidhaa zake na taasisi za utafiti kufanya tafiti za kuangalia vifo vitokanavyo na matumizi ya tumbaku ili kuwe na takwimu za nchi na siyo kutegemea za kutoka nje,” anaeleza Ummy.