27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

UTAFITI: KITAMBI KINAONGEZA HATARI YA KUPATA SARATANI

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA


TUNAISHI katika jamii ambayo uzito wa kupita kiasi umekuwa sehemu ya mila na desturi yetu– licha ya kwamba ushahidi umeonesha kuwa uzito kupita kiasi au unene una athari mbaya kiafya.

Staili ya maisha, vyakula na shughuli za kila siku za mwanadamu ni baadhi ya vitu vinavyosababisha idadi kubwa ya wake kwa waume kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi na wakati mwingine kuwa na vitambi.

Tatizo la unene na vitambi litazidi kuongezeka ikiwa serikali, hususan wananchi wenyewe hawatachukua hatua za dharura na mipango madhubuti kulikabili.

Vitambi hupunguza maisha ya watu wenye hali hiyo, hivyo kusababisha upotevu wa rasilimali watu.

Kuna wengi wanatambua athari za tatizo la unene na vitambi, lakini hawafanyi chochote kulirekebisha, hii inatokana na ukweli kwamba idadi kubwa ya watu hawajui maana halisi ya kuwa na afya njema.

Lakini pia wengi wanafahamu kuwa uzito kupita kiasi au unene unaongeza hatari ya kupata aina 11 ya saratani ikiwamo ya matiti, tezi dume na utumbo mpana.

Lakini ni sababu gani husababisha hali hii hasa? Kitu muhimu ni kufahamu kwamba seli za mafuta hubadili mazingira ndani ya mwili wa mwanadamu.

Hutoa mlolongo wa kamikali ambazo zinaweza kuzifanya seli zilizo karibu nazo kujishughulisha tofauti na utaratibu wao wa kawaida na kusababisha uwezekano wa seli hizo kugeuka vivimbe vya saratani.

Mchakato huu hutokea kwa namna nyingi katika sehemu tofauti za mwili na kusababisha aina tofauti ya saratani kujitengeneza.

Kwa mujibu wa utafiti mpya, mafuta ya tumboni ndiyo mchawi mkubwa zaidi anayetuweka katika hatari ya kupata maradhi ya saratani.

Mafuta ya tumboni, ambayo ni chanzo cha kitambi kuibuka yanaweza kuzalisha protini inayohimiza seli za kawaida kuwa seli za saratani.

Watafiti wa Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani wanasema katika upande wa tathmini ya saratani, kutathmini kiwango cha mafuta tumboni ni sahihi zaidi ikilinganishwa na kutathmini hali ya unene wa mwili.

Timu hiyo ya utafiti imetoa ripoti ikisema, waliwalisha panya chakula chenye mafuta mengi na kufanya utafiti juu ya matokeo ya kitendo chao hicho kwa panya.

Wakagundua kuwa mafuta tumboni yamezalisha idadi kubwa ya protini maalumu, ambayo inazifanya seli za kawaida kuwa dhaifu na kubadilika kuwa seli za saratani.

Yakilinganishwa na mafuta ya chini ya ngozi, mafuta ndani ya maini yanaweza kuzalisha protini nyingi zaidi ya aina hiyo.

Baada ya hapo, watafiti waliweka mafuta yaliyokusanywa katika mwili wa binadamu kwenye mwili wa panya.

Matokeo yakaonesha kuwa mafuta yanazalisha protini nyingi zaidi ya aina hiyo, seli nyingi zaidi zinakuwa seli za saratani.

Mafuta haya yaliyozidi kuzunguka eneo la tumbo na kutengeneza kitambi tukijuacho huwatokea watoto, vijana kwa watu wazima wakiwamo wazee bila kujali jinsia zao.

Kwa  mujibu  wa  tafiti  mbalimbali  za  kitaalamu, mwili wa binadamu una seli kati  ya bilioni 50 hadi 200 za mafuta zilizogawanyika katika  sehemu mbalimbali  za  mwili wa binadamu.

Kwa wanawake, seli hizo zinapatikana zaidi katika maeneo ya matiti, nyonga, kiunoni na kwenye makalio.

Kwa upande wa wanaume, zinapatikana  zaidi kifuani, tumboni na kwenye makalio pia.

Mafuta haya ya tumbo yanayotengeneza kitambi, hukusanywa kwa njia kuu mbili; kutoka kwenye tishu zilizo chini ya ngozi na kutoka kwenye ogani za ndani kama vile moyo na kongosho.

Kwa maneno mengine sababu kuu ya kutokea kitambi ni ukosefu wa ulingano wa kalori, yaani mtu kula vyakula vinavyotia nguvu kwa wingi kuliko namna anavyoweza kuviondoa kama taka kutoka mwilini.

Lakini pia, huweza kusababishwa na chembe za urithi za unene kutoka kwa wazazi, sababu za kimazingara na nyinginezo ikiwamo kukosa usingizi na ulaji mbovu.

Kwa sababu hiyo, utafiti umependekeza kuwa, watu wanatakiwa kutilia maanani mafuta yaliyomo ndani ya tumbo katika kudhibiti kitambi kupitia udhibiti wa chakula na ufanyaji wa mazoezi.

Watafiti wanasema udhibiti wa kitambi kwa njia hizo ni mzuri zaidi kiafya pale zinapoendeshwa kwa mpangilia mzuri badala ya matumizi ya dawa.

Wanaonya kuwa dawa nyingi zinazodaiwa kuwa na uwezo wa kupunguza vitambi na uzito mkubwa au unene ni sumu.

Kwa mujibu wa tafiti nyingi za kisayansi, dawa hizi kwa kiasi kikubwa zina kemikali kama vile phentermine, sibutramine, phenolphthalein, caffeine, hydroxycitric acid (HCA) na senna ambazo zina madhara makubwa kwa afya ya binadamu.

Tafiti hizo zimekuja huku mapema mwaka huu wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikuja na kampeni ya kupiga vita saratani kwa kuhamasisha umuhimu wa kutambua mapena na kuzuia kusambaa kwake.

WHO lilisema saratani ndio chanzo cha kifo cha mtu mmoja kati ya sita duniani, na hadi asilimia 50 ya aina zote za saratani zinazoweza kuzuilika.

Lakini idadi ya visa vipya vya ugonjwa huo inatarajiwa kuongezeka kwa takriban asilimia 70 katika miongo miwili ijayo.

Wakati WHO pia likionya kuhusu unene na hususani kitambi, lilikiri kuwa utumiaji tumbaku ndio hatari kuu ya chanzo cha kuugua saratani.

Lilisema tumbaku ni chanzo cha takriban asilimia 22 ya vifo vya jumla vinavyotokana na saratani.

Lilisema saratani ya matiti inaongezeka, hususan katika mataifa yanayoendelea, ambako visa vingi hutambuliwa katika awamu ya mwisho wakati ugonjwa tayari umesambaa katika mwili wa mwathirika.

Licha ya kuidhinishwa kwa baadhi ya malipo ya matibabu katika bima ya kitaifa ya afya nchini, bado tatizo lipo kutokana na kutowapo kwa taasisi za kutosha za umma zinazotoa huduma hizo – na kwa chache zilizopo, hazina vifaa stahili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles