30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

AINA YA SUMU MWILINI, NAMNA YA KUZITOA

SUMU ni kitu chochote ambacho kinaweza kuingia mwilini na kusababisha mifumo ya mwili ishindwe kufanya kazi ipasavyo.

Kutegemeana na namna ambavyo sumu inategenezwa, pia namna ambavyo inampata mtu, tunaweza kuzitenga sumu katika makundi yafuatayo.

Kundi la kwanza ni sumu zinazozalishwa ndani ya mwili wa kiumbe husika zinazotokana na utendaji kazi wa mwili kwa asili yake – kitaalamu inaitwa Toxins, kundi la pili ni sumu ambazo huingia kwa njia ya kung’atwa na mdudu au mnyama (Venom) – mfano ni snake-venom, kundi lingine ni sumu ambazo kwa asilimia kubwa hutokana na kemikali zinazotengenezwa na binadamu kwa matumizi mbalimbali mfano dawa kwa ajili ya kutibu magonjwa, kuua wadudu na viumbe wasababishao magonjwa na matumizi mengine.

Kwa aina hii ya sumu, mtu anaweza kuathirika kupitia njia zisizopungua tano kama kwa njia ya kumeza, kuvuka hewa, kupakaa au kugusa kwa ngozi, kuchoma sindano na njia ya mionzi.

Kwa upande wa sumu ambazo ni kemikali zinazotengenezwa na binadamu, pindi zinapoingia katika mfumo wa utendaji kazi wa mwili huleta athari ambazo hutofautiana kwa kutegemea aina ya sumu.

Asilimia kubwa ya athari zinazojitokeza baada ya kuathirika na sumu hizi, zinafanana na athari ambazo mtu huzipata pindi anapopatwa na tatizo lililosababishwa na viumbe (bakteria au virus) wanaosababisha magonjwa.

Miongoni mwa athari hizo ni viungo kukakamaa au kupata degedege, kutapika, ngozi kuharibika, maumivu ya kichwa/viungo, kuharisha, kifua kubana, kupoteza uwezo wa kuona, kupoteza fahamu na hatimaye kifo, endapo matibabu yatakosekana.

Kama ambavyo athari za sumu hutofautiana kulingana na aina ya sumu, pia huduma ya kwanza na matibabu yanaweza kutofautiana kulingana na aina ya sumu.

Jambo la kwanza katika kumsaidia mtu aliye athirika na sumu ni kutambua aina ya sumu iliyomletea tatizo, hii itasaidia katika kuanzisha njia sahihi ya kutoa msaada, pia kusaidia kuchagua aina bora ya dawa kinzani (Antidote) ambayo itatumika kupunguza makali ya sumu iliyotumika. Kitu kingine ni kubaini njia ambayo sumu imeingia mwilini (imeingingia kwa njia ya kinywa, hewa, kupakaa katika ngozi au sindano?) hii itasaidia katika kuandaa mazingira mazuri ya kumpumzisha mwathirika wa sumu, pia itasaidia katika kuandaa vifaa na vitu ambavyo vitapunguza sumu mwilini. Mfano, kama ni katika ngozi, maji safi ya kusafisha eneo la ngozi ambalo limegusana na sumu, au kama ni sumu ambayo mtu amekunywa, kuandaa namna bora ya kumtapisha ili kuzuia isizidi kuingia katika mfumo wa mwili. Pia kwa baadhi ya mazingira kumtapisha mtu kunasaidia kutambua aina ya sumu ambayo mtu ameitumia.

Kwa baadhi ya mazingira kumtapisha mtu husaidia kubaini aina ya sumu, kwa kuwa zipo ambazo mtu anapoitumia kwa asili yake ni kama tindikali, inapopita katika koo hadi tumboni tayari itakuwa imeunguza njia, hivyo kumtapisha kutamsababishia azidi kuungua na hivyo utakuwa unazidi kumuumiza.

Jambo lingine ambalo linafanyika katika kumsaidia mtu aliyeathirika na sumu ni kupambana na dalili zinaonekana kwa wakati huo (symptoms), kama ni maumivu, degedege na kifua kubana, matibabu yatatolewa kulingana na dalili.

Kulingana na aina ya sumu, kuna uwezekana mtu kwa kufahamu au kutofahamu akawa amepatwa na sumu mwilini mwake lakini asiweze kuziona dalili zozote kwa wakati huo, dalili zinaweza kuanza kuonekana hata baada ya zaidi ya mwezi.

Sumu inasababisha mtu apoteze uwezo wake wa mwili kufanya kazi ipasavyo na hata kupoteza maisha, pindi unapohisi kuwa mwili wako una sumu, usisubiri kuona dalili bali onana na wataalamu wa afya kwa msaada zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,896FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles