LABDA ulidhani uchafuzi wa mazingira ni chanzo cha magonjwa ya mlipuko. Unaweza kuwa sahihi lakini hiyo ni moja kati ya madhara mengi anayoweza kupata mtu asiyeona tabu kukaa mazingira machafu.
Katika utafiti wa hivi karibuni wa taasisi mbili, Lung Care Foundation (LCF) na Pulmocare Research and Education (PURE), watoto wanaoishi mazingira yenye hewa chafu wako hatarini kupata tatizo la ongezeko la uzito (unene).
Utafiti huo nchini India uliwafikia watoto 3,157 katika shule 12. Maeneo yaliyotumika katika utafiti huo ni Delhi, ambako kuna kiwango kikubwa cha uchafuzi wa mazingira. Pia, yaliguswa maeneo ya Kusini mwa India, Kottayam na Mysuru, ambako kunasifika kwa kiwango kizuri cha hewa safi.
Katika kile kilichoonekana kwenye majibu ya utafiti, ilibainika kuwa asilimia 39.8 ya watoto kutoka Delhi walikuwa na changamoto ya uzito mkubwa, ukilinganisha na asilimia 16.4 ya wale wanaoishi Kottayam na Mysuru.
Akizungumzia uhusiano wa hewa chafu na ‘ubonge’, Mkurugenzi wa PURE, Dkt. Sundeep Salvi, anasema: “Hewa chafu hubeba kemikali fulani hivi ziitwazo Obesogens, ambazo zinaathiri ufanyakaji kazi ndani ya mwili.”
“Mtu anapovuta hewa chafu, hizo kemikali zinaingia mwilini. Zinapoingia, zinakwenda kutibua mfumo wa homoni, hivyo kusababisha ongezeko la uzito,” anasema Dkt. Salvi akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Kwa upande mwingine wa utafiti huo, ulibaini kuwa unene ni chanzo kikubwa cha ugonjwa wa pumu kwa watoto. Kwamba mtoto mwenye uzito mkubwa ana asilimia 79 ya kupata tatizo hilo la upumuaji.
Delhi, ambako tumeona kuwa ndiyo sehemu inayokabiliwa na hewa chafu zaidi India, asilimia 29.3 ya watoto walibainika pia kusumbuliwa na pumu. Ni tofauti na maeneo yenye hewa safi (Kottayam na Mysuru) kwani utafiti ulikuta ni asilimia 22.6 pekee.