27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yatoa elimu umuhimu wa TIN kwa wafugaji, wavuvi na wakulima

Na Clara Matimo, Mwanza

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendela kutoa elimu ya mabadiliko ya  sheria  ya usimamizi  wa kodi ya mwaka 2015 kifungu cha 22  sura 438 yaliyotokea kwenye sheria ya fedha ya mwaka 2021 inayowataka wakulima, wafugaji na wavuvi kuwa na  Namba ya Utambulisho ya Mlipa Kodi  (TIN) ili watu waielewe waweze kuchangia pato la taifa.

Sheria hiyo pia inawataka  wawekezaji, waajiriwa na wafanyabiashara kuwa na TIN ndani ya siku 15 baada ya kuanza shughuli  zao za kiuchumi na atakayepitiliza muda huo adhabu yake ni Sh milioni 1.5.

Hayo yamebainishwa jana na Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka TRA, kanda ya ziwa,  Alex Mwambenja wakati akizungumza na waandishi wa habari  waliotembelea banda lao kwenye maonesho ya 16 ya biashara ya Afrika Mashariki yaliyoandaliwa na Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo  Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza.

Mwambenja amesema   mabadiliko  hayo yalifanywa  Juni 30 mwaka huu kwenye bunge la bajeti yameanza  kutumika  Julai Mosi mwaka huu ambapo yanawataka  wakulima, wafugaji na wavuvi  kuwa na TIN ambayo inatolewa bure na TRA ili waweze kukatwa kodi ya zuio ya asilimia mbili watakapokuwa wanauza bidhaa zao kwenye makampuni lengo ni kuchangia  ukuaji wa pato la taifa. 

“Katika mabadiliko hayo kuna kodi ya majengo ambayo siyo mpya ilikuwepo tangia mwanzo lakini mabadiliko yaliyotokea ni jinsi ya kukusanya kodi sasa wenye nyumba za kawaida zilizo na umeme  watalipa kodi hiyo kupitia ununuaji luku ambayo ni Sh 1,000 kwa kila mwezi, walio na nyumba za ghorofa kila sakafu watalipa Sh 60,000 kwa mwaka sawa na Sh 5,000 kwa mwezi,  nyumba za matope na nyasi hazitozwi kodi ya majengo.

“Waliokuwa wanasamehewa kwa mujibu wa sheria wataendelea kusamehewa  ambao ni wazee  kuanzia umri wa miaka 60 na watu wenye ulemavu ambao hawana kipato lakini walibahatika kujenga au kujengewa nyumba ya kuishi na awe anaishi humo lakini isiwe ya biashara,”amefafanua Mwambenja.

Amewataka wananchi kutopata taharuki kuhusu namna ya ukusanyaji wa kodi hiyo ya majengo bali wafike ofisi za TRA ili waweze kupatiwa elimu zaidi badala ya kusikiliza maneno ya wananchi wa mtaani ambao baadhi yao wanawapotosha na kuwatia hofu.

Amefafanua kwamba wazee wenye umri wa miaka 60  wanapaswa kupeleka vielelezo viwili tu TRA ambavyo ni barua kutoka Serikali ya mtaa ambayo inamthibitisha kwamba anaishi eneo ambalo nyumba hiyo ipo na kitambulisho kinachoonyesha umri wake, ikiwa walio kwenye msamaha waliishalipa kodi zao  za majengo kwa njia ya umeme zitarudishwa,”ameeleza.

Mwambenja amesema ili waweze kurudishiwa fedha hizo inawapasa wafike TRA wajaze fomu za ushirikiano baina yao na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)  mita hiyo iondolewe  kwenye mita zinazokatwa kodi ya majengo  na atarudishiwa fedha zake zote kwa kuwekewa unit za umeme.

  “Msamaha unatolewa kila mwaka hivyo itawalazimu wenye msamaha kuomba kila mwaka, kama ikitokea amefariki na nyumba hiyo akapewa urithi mtu ambaye hajafikisha miaka 60 hatarithi msamaha   ataendelea kulipa kodi ya majengo kama kawaida maana msamaha haumhusu, ”amesema na kuongeza

“Pia wananchi wa mikoa ya kanda ya ziwa wakiyatumia vizuri maonesho haya  kwa kutembelea banda letu  hapa Rock City Mall naamini maswali yao yote tutayajibu maana tutawaelimisha vizuri sana tuna fomu zetu tutawaelekeza namna bora ya kujaza kama una nyumba yenye mita zaidi ya moja na ulilipia kodi ya majengo kwenye mita zote kwa mwezi uliopita utajaza fomu ambayo mita moja ndio itatumika kwa ajili ya malipo ya kodi ya majengo,”alisema.

Kwa mujibu wa Mwambenja nia ya Serikali ni kila jengo moja lilipwe kwenye mita moja hata kama kuna mita zaidi ya moja mwenye nyumba inatakiwa aiorodheshe mita moja ambayo itatumika kulipia  kodi ya majengo.

Afisa mwandamizi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi kanda ya ziwa, Lutufyo Mtafya, alimwambia Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi ambaye alitembelea banda hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel  kwenye ufunguzi wa maonesho hayo “Mkoa  huu ni  wa pili kitaifa ukitanguliwa na Dar es Salaam katika kusajili watu wengi kwenye mfumo wa kuwasilisha return kwa njia ya kielektronic,”alisema.

Kwa upande wake Makilagi, aliwataka TRA kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili watambue mabadiliko ya  sheria hiyo  ya usimamizi  wa kodi ya mwaka 2015 iliyofanyiwa marekebisho June 30 mwaka huu  ili waweze kuitekeleza bila kupewa adhabu ya takwa la kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles