29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

USTAA NI MZIGO MZITO KWELI, ILA UNAUBEBAJE?

KUNA msemo unaosema, msanii ni kioo cha jamii. Hili halina ubishi hata kidogo, ndiyo maana watu wengi hupenda kufanana kwa mambo fulani na baadhi ya wasanii. Maana yake kinachofanywa na wasanii huchukuliwa kama njia ya wengine kufuata.

Tatizo ni pale baadhi ya wasanii wanapofikia hatua ya kufanya mambo ya hovyo mbele ya jamii, ndipo wengine kwenye jamii huwaiga na kuharibu utamaduni wetu.

Bahati mbaya zaidi ni kwamba, kuna baadhi ya wasanii wanalazimisha maisha… hana kitu anataka kuonekana ana gari, matokeo yake anakodisha gari. Kwa wasanii wa kike ni mbaya zaidi, maana akiishiwa fedha ndipo vishawishi vinapoanzia.

Ustaa haumaanishi hivyo. Unavyoambiwa ustaa ni mzigo, unapaswa kuishi maisha safi, ukijinasibisha jina lako na mambo unayofanya kwa jamii.

Kumbuka kuwa, wewe kama kioo watu wanakufuatilia kuona maisha yako. Watu watapenda kujua unakula nini, unatembelea gari la aina gani, unaishi kwenye nyumba gani nk.

Lakini hilo siyo sababu ya wewe ‘ku-fake’ maisha yako. Ishi maisha yako halisi. Angalia mipango yako ya mbele. Ustaa una mwisho, hizo shoo unazopiga leo, kuna siku zitafikia mwisho wake.

Kabla ya wewe leo hii kuwa staa kumbuka kuna mastaa wengine wengi walitangulia kabla yako. Ni suala la kupokezana vijiti.

Wapo baadhi ya mastaa ambao wameweza kutunza ustaa wao mpaka leo, lakini ukweli ni kwamba viwango kisanii ukiwalinganisha na kizazi cha leo, hawawezi kufanana. Kila mmoja anakuwa bora kwa enzi zake na zama zake.

Ni kweli wasanii kama Sugu, Profesa Jay, Afande Sele, Juma Nature, Jaydee na wengine wa levo hizo bado ni maarufu lakini hawawezi kulingana na Diamond au Ali Kiba. Siyo kwamba hawana uwezo, ila zama zimepita.

Ni vyema msanii akijiwekeza. Akakumbuka kuna kesho yake, aweke vitegauchumi kila mahali kwa namna anavyoweza ili kujiandalia maisha bora hapo baadaye. Siyo sahihi hata kidogo kuishi mradi siku zinakwenda, kutegemea bahati.

Hayo ni mawazo ya kimasikini. Heshimu kipaji ulichopewa na Mungu, ithamini kesho yako. Fikiria kuhusu familia yako, watakula nini, watasoma wapi nk. Usichanganye ustaa na majukumu ya familia.

Kubwa unalopaswa kuweka akilini mwako ni kwamba, wewe kama kioo, watu wataendelea kufuatilia maisha yako ili wajifunze kupitia kwako. Kama msanii una kazi kubwa kwelikweli, lakini ni jukumu lako kuikabili.

Kila la kheri wasanii wote wa Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles