29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

USIBISHE SAMATTA ANAISHI KWENYE NDOTO YA NGASSA, BOBAN

NA MARTIN MAZUGWA


DUNIANI tunaishi mara moja tu unapopata nafasi ya kufanya mazuri na kutimiza ndoto zako ni bora ukafanya  hivyo, muda haujawahi kuwa rafiki wa mwanadamu hata mara moja na usipoweza kuishi ndoto zako basi kuna watu watatumia ndoto zako kuishi maisha yao.

Mchezo wa soka unaongoza kwa kupendwa kutokana na kuwa na wapenzi wengi ambao wanausapoti mchezo huu tofauti na michezo mingine kama ngumi, riadha, gofu na tenisi ambayo haipewi kipaumbele.

Unapotaja mfalme wa soka Tanzania kwa sasa lazima unamtaja staa wa klabu ya Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali   kutokana na spidi yake ya kuzifumania nyavu mara 15 katika michezo 45 aliyoshuka dimbani hadi sasa.

Sishangai kwa Samatta kufunga, maana ni kazi yake, nimemshuhudia akiwatesa makipa wengi, najua anafurahia kufunga hajaanza kufanya hivyo leo au jana, alianza zamani akiwa kwao Mbagala ambapo hakuna aliyemjua.

Samatta anaipenda na kuiheshimu kazi yake, hajawahi kuidharau miguu yake inayompa ulaji hata mara moja, heshima hiyo ndiyo imepelekea kufika pale alipo hivi sasa.

Alipotajwa katika kikosi cha wiki cha wachezaji waliofanya vizuri katika Ligi ya Ulaya (Europe League) wala sikushangaa, maana nyota huyu amezaliwa kushinda, hajawahi kuwaangusha Watanzania alianza kutengeneza ufalme wake Afrika na sasa yupo barani Ulaya.

Siku zote mwenye kiu huhitaji maji na si maji kuhitaji mwenye kiu, anachokifanya Samatta hivi sasa ni kuishi kwenye ndoto za kaka zake, Mrisho Ngassa na Haruna Moshi ‘Boban’, ambao walipokuwa wanacheza ndoto zao zilikuwa kwenda Ulaya walipopata nafasi wakashindwa na wakaamua kurudi nyumbani.

Boban na Ngassa walikuwa Watanzania wa kwanza kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa, lakini walishindwa kufanya hivyo matokeo yake walirudi nyumbani na kuendelea kucheza viwanja vyenye vumbi, ambavyo vinalalamikiwa kila kukicha na wachezaji kutokana na ubovu.

Kwa watu waliowahi kuwashuhudia  nyota hawa walipokuwa katika ubora wao ni tusi kusikia kuwa walishindwa kucheza Ulaya na kubaki hapa nchini, wakimalizia soka lao huku wakishindwa kupewa heshima yao wanayostahili.

Wakali hawa walishindwa kucheza na nyakati, wameshtuka wakati tayari jua limezama, Ngassa alipaswa kuwa Mtanzania wa kwanza kukipiga ndani ya EPL na kuweka rekodi na kuwa chachu kwa vijana ambao walikuwa wakimwona kama ‘role model’ wao.

Ngassa ambaye ni moja kati ya nyota wenye vipaji vya hali ya juu kutokana na ubora wake kipindi hicho, kocha mwenye heshima raia wa Italia, Gianfranco Zola, alishindwa kuficha hisia zake mbele yake na kuamua kumwita kufanya majaribio katika klabu ya West ham, jambo ambalo si la kawaida hata kidogo.

Samatta endeleza ndoto za kaka zako hawa ambao waliwahi kuamka na kuiacha ndoto hii tamu ambayo wewe umeamua kulala ili uimalizie.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles