CHRISTIAN BWAYA
WANAWAKE wengi wanatamani kujua siri ya kupendwa na wapenzi wao. Katika jitihada za kufahamu namna ya ‘kuwakamata’ wanaume, wapo wanaotumia hata njia za giza ilimuradi wajihakikishie mapenzi kwa wanaume wao.
Ingawa zipo tofauti ndogo ndogo miongoni mwa wanaume, kwa ujumla, uchambuzi wa tafiti mbalimbali za uhusiano unabainisha kuwa kinachowafanya wanaume ‘wakamatike’ ni yale mahitaji yao. Hapa ninakuletea baadhi yake.
Mfanye ajione shujaa wako
Mwanamume anatamani kujihisi ni shujaa asiyeshindwa. Fahari ya mwanamume siku zote ni uwezo anaoamini kwamba anao, unaomfanya mara nyingine awe tayari kufanya mambo yanayoweza kuhatarisha maisha yake kwa lengo la kuthibitisha kuwa wanaweza.
Kama unatamani mwanamume umpendaye aanze (aendelee) kuvutiwa na wewe, chukua hatua ya kumfanya ajione ni shujaa wako. Mahali pa kuanzia ni kubaini na kuvitambua vitu vinavyomfanya ajisikie fahari. Huenda ni tabia fulani maalumu ama ujuzi, maarifa na sifa nyingine za kipekee unazojua anazo.
Tambua tabia hizo, ujuzi au sifa zozote alizonazo, utamfanya ajiamini. Mwanamume anayejiamini huwa na moyo wa kuchangamka zaidi na hivyo huwa na msukumo wa kufanya vizuri zaidi ili awe shujaa wako.
Mheshimu
Mwanamume anahitaji kuheshimiwa. Heshima ndio hadhi yake. Ninapozungumzia heshima kwa mwanamume, katika mazingira yetu, namaanisha hali ya kutamani kujiona ana hadhi ya juu, ana mamlaka zaidi pengine kuliko mwanamke. Kinyume chake ni kudharauliwa, kuwekwa katika mazingira ya kujiona hana hadhi, hana mamlaka, asiye na kauli wala uwezo wa kufanya lolote bila mwongozo wa mwanamke.
Kwa wanaume wengi, heshima ni namna unavyozungumza naye, maneno unayoyatumia katika kueleza mawazo yako, ishara za mwili wako katika mazungumzo, kumpa nafasi ya kwanza katika uamuzi na mambo kama hayo.
Heshima, mstahi mwanamume unayempenda hata anapokosea. Kosa linapotumika kama sababu ya kufanya vitendo vinavyodhalilisha hadhi yake ni kujipunguzia alama. Kadhalika, heshima ni kuwa tayari kumtunzia hadhi yake kwa watu wengine. Kumjengea taswira inayomwongezea thamani yake kwa watu unaojua anawaheshimu. Kuonesha fahari yako kwake unapozungumza na watu wengine kwa kauli, matendo na hisia kunaongeza alama za sifa anazozitafuta.
Heshimu faragha yake
Mwanamume anahitaji kujiona ni mtu mwenye uhuru wa kufanya mambo anayoyafurahia bila kuingiliwa. Uhuru unakwenda sambamba na kuhitaji faragha. Kimsingi, kama mwanamke, saa nyingine unatamani ufahamu kila anachokifanya mume wako.
Unahitaji kujua mawasiliano yake, ameongea na nani, ameandikiana na nani, anafahamiana na nani na ikiwezekana ujue kila nukta ya mawazo yake. Pengine unaweza hata kushawishika kumchunguza kwa siri.
Ingawa ni kweli wanawake hutamani mwanamume muwazi, kwa upande wao, wanaume hutamani nafasi ya kufanya mambo yao bila kupelelezwa. Hawapendi kuona wakinyang’anywa haki ya kuwa na faragha.
Ikiwa unatamani kuwa na uhusiano uliojengwa katika msingi
wa kuaminiana, mfanye akuamini ili kwa utashi wake akuruhusu kuingilia maisha
yake ya faragha kwa hiari yake. Kadri anavyokuamini ndivyo anavyoweza
kukukabidhi uhuru unaoutaka wewe bila kuleta mtafaruku.
Onesha kumhitaji
Kama mwendelezo wa mamlaka
tuliyoona kuwa ni kiini cha uanaume, mwanamume wa kawaida anatamani kujisikia
kuwa bado anahitajika. Anatamani kujiona kuwa mambo yako hayaendi bila yeye.
Wanaume wanakua wakiaminishwa na jamii, marafiki rika na
wakati mwingine kupitia matendo ya baba zao wenyewe kwamba wao ndio watatuzi wa
matatizo. Na kwa jinsi imani hii ilivyojikita mizizi kwenye akili ya mwanamume,
tukisema anaamini ni mtatuzi wa matatizo hatufiki kwenye uhalisia. Anapenda awe
jibu la mambo yote.
Jaribio lolote la kumwonesha
kuwa hata asipokuwapo, hata asipofanya chochote, hata asipotoa wazo lolote,
hakuna kitakachoharibika linaweza kumfanya ‘akahujumu’ uhusiano. Kumfanya
ajione hahitajiki, kunaathiri kiburi chake cha uanaume (ego) na inaweza kuwa
mwanzo wa matatizo.
Hata kama ni kweli unamzidi
kipato, hekima na uelewa, lakini jifunze kuwa chini yake na mwaminishe kuwa
anahitajika. Mwanamume anapojua anahitajika huhamasika kupenda. Usifanye kosa
la kumfanya ajione amekataliwa.
Usitake kumbadilisha
Hujisikia kudhalilika
anapogundua kuna vitabia vyake unakazana kuvibadilisha. Mwanamume anapofahamu
unambadilisha, anajiona kama mtu aliyepoteza mamlaka yake. Hawezi kukubali
kirahisi.
Ni kweli yapo mambo unayohisi ni muhimu ayabadilishe. Mfano, marafiki wanaompetezea muda wake ambao angeweza kuutumia na familia, labda hana hamasa na mambo ya kiimani, labda ni kazi anayofanya au tabia fulani zinazokukera. Usijaribu kuonesha nia ya kumbadilisha.
Ukitaka mwanamume afuate yale unayotaka ayafanye, mkubali vile alivyo na ajue umempokea bila masharti. Kukubaliwa ni motisha ya kubadilika. Hiyo ndio kanuni. Mume wako anapojua pamoja na upungufu wake bado umemkubali alivyo, kubadilika ni suala la muda.
Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, twitter: @bwaya