23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ushirikiano NMB, ZTC wamvutia Rais Dk. Mwinyi

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imevutiwa na ushirikiano baina ya Benki ya NMB na Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZTC), ambao umekuwa chachu ya kukuza utalii, huku ikiitaka kuziunga mkono wizara zote za SMZ na Mamlaka za Serikali za Mitaa, ili kuziwezesha kuziona fursa na kuzitumia kwa ustawi wa Uchumi wa Zanzibar.

 Hayo yamesemwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, alipokuwa akiwasilisha salamu za Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, katika Hafla ya Futari iliyoandaliwa na NMB, ikihudhuriwa na mawaziri wa SMZ, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, viongozi wa Dini na wateja wa benki waliopo visiwani hapo.

Akizungumza wakati wa kutoa neno la shukrani mbele ya waalikwa zaidi ya 400, Waziri Omar, ambaye alimwakilisha Rais Mwinyi, alisema ushirikiano wa NMB na ZTC ni mkubwa, ulioifungamanisha Kamisheni hiyo na fursa za kiuchumi, na kwamba Rais anatamani kuona NMB inazifikia wizara mbalimbali na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

 “Niko hapa kwa niaba ya Rais, Dk. Hussein Mwinyi na nichukue nafasi hii kuwapa salamu zake. Kwanza Rais amefarijika sana kwa aina ya ushirikiano uliokuwepo baina ya NMB na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, ushirikiano ambao unalenga zaidi kukuza Utalii wa Zanzibar. Ushirikiano huo unaangalia mbali zaidi ya yale tuliyoyazoea. 

 “Kwa muda mrefu utalii wetu ulikuwa umejikita katika kuuza fukwe, lakini NMB mmenyoosha mkono kwa ZTC na kuwaonesha fursa zingine za kiutalii zilizopo Zanzibar, hasa vivutio vya historia na mambo kale. Ni jambo zuri, la kupongezwa na kuungwa mkono. 

“Pia, SMZ inawakaribisha zaidi NMB kushirikiana na wizara yenyewe ya utalii kwa ujumla wake, najua ina mipango mingi mbali ya ile ya Kamisheni, lakini pia mshirikiane na wizara zingine zote za SMZ, kuanzia Wizara ya Elimu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo, hata Wizara ya Biashara na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa.

 “Mkikaa na Mstahiki Meya atawaambia fursa zilizopo katika kuendeleza miji na majiji yetu. Kwa hiyo niwaalike NMB mshirikiane na wizara zingine na naamini mtashiriki kwa mapana katika kuendelea kuuimarisha uchumi wa Zanzibar, kupitia dhana hii inayochakatwa na Rais Dk. Mwinyi ya Uchumi wa Bluu,” alisisitiza Waziri Omar.

Aidha, alibainisha kuwa yeye binafsi amefarijika sana kusikia NMB inaiunga mkono SMZ sio tu katika masuala ya utalii, bali uwekezaji wao wenye thamani ya Sh. Bil. 1 za kujenga Kituo cha Pamoja cha Malipo (One Stop Center), bandarini, ambacho kitakuwa chachu ya ufanisi na kukuza makusanyo.

 Kabla ya Mwakilishi huyo wa Rais, Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Alfred Shao, alisema NMB imekuwa na mahusiano ya muda mrefu na ZTC, ambako mashirikiano yao hayajaishia tu katika kuimarisha Sekta ya Utalii kwenye fukwe za bahari, bali pia unaangazia utamaduni wa Mzanzibar na vyakula asilia.

 “Hafla hii inafanyika katika muktadha huo wa mashirikiano baina yetu. Tunafanya mambo mengi katika Sekta ya Utalii, lengo ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya Zanzibar, kwani tunatambua Sekta ya Utalii ni kati ya maeneo yanayoiingizia pesa nyingi sana Serikali, nasi tumeelekeza nguvu zetu huko,” alisema Shao.

 Akizungumzia Kituo cha Pamoja cha Malipo, Shao alisema bandarini pamekuwa na malipo mengi tofauti, hivyo walipaji kupewa ‘Control Number’ tofauti tofauti na kwamba wao wanataka mteja anapopewa namba moja, aitumie kulipia malipo yote, jambo litakaloongeza ufanisi kwa makusanyo na kuondoa usumbufu kwa wateja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles