SERIKALI imesema iko makini na itahakikisha kuwa nchi inakuwa na usalama wa kutosha wa chakula kwa kuongeza uzalishaji ili kuendana na idadi ya watu inayoongezeka.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Florence Turuka, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa mbolea toka ndani na nje ya nchi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema pamoja na juhudi nyingine zinazofanyika, wanasayansi na watafiti wametakiwa kuhakikisha kuwa taarifa zinazopatikana kuhusu udongo zinatumika ipasavyo ili kutoa suluhisho linalotakiwa pale inapohitajika.
“Taarifa hizi zitasaidia kufahamu maeneo yenye rutuba kidogo, sumu na hivyo kupata majibu yanayotakiwa,” alisema.
Katibu Mkuu huyo alitaja moja ya mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mazao kama ushirikiano kati ya Serikali na taasisi inayojulikana kama Africa Soil Information Services (AfSIS) na kitengo kipya katika Wizara hiyo kinachoitwa Tanzania Soil Information Services (TanSIS), ambapo ardhi yote nchini itapimwa na kufanyiwa tathmini ili kujua ubora wake.
Alisema mkakati huo utasaidia kujua mahitaji ya maeneo husika na kuwasiliana na kampuni za kuzalisha mbolea.
Aliiomba taasisi ya African Fertilizer and Agribusiness Partnership (AFAP) na wadau wengine kushirikiana na TanSIS ili kuhakikisha kuwa panakuwa na matumizi bora ya mbolea nchini.
Takwimu zinaonyesha kuwa matumizi ya mbolea bado ni madogo sana katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mwaka 2005 hadi 2010, wastani wa matumizi ya mbolea Afrika ilikuwa metriki tani milioni 3.2 kwa mwaka, ikilinganishwa na metriki tani milioni 74.1 (Asia), 19.5 (Marekani) na 13.0 (Ulaya).
Kwa mujibu wa Dk. Turuka, matumizi haya madogo ya mbolea yanatakiwa kuboreshwa haraka kama kweli Afrika inataka kuzalisha chakula cha kutosha kwa watu wake.
“Maboresho katika sekta ya kilimo hayana budi kuimarishwa sasa kuliko kipindi chochote kutokana na idadi ya watu inayoongezeka na mabadiliko ya hali ya hewa,” alisema.
Wakati wa uhuru mwaka 1961, Tanzania ilikuwa na watu takribani milioni 9. Idadi hiyo imeongezeka kufikia karibu watu milioni 50 mwaka 2016 katika eneo la ukubwa wa ardhi lile lile la kilometa za mraba 945,000,000.