SANAA, SYRIA
SERIKALI ya Shirikisho la Urusi kupitia Waziri wa ulinzi wa nchi hiyo, Sergei Shoigu, amesema kiasi cha waasi 88,000 wameuawa nchini Syria katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita tangu nchi hiyo kuingia kijeshi nchini humo kuwasaidia wanajeshi wa Serikali ya Rais Bashar al Assad.
Sergei Shoigu amesema katika kipindi hicho cha operesheni, zaidi ya waasi 87,500 wameuawa, makazi 1,411 yamekombolewa.
Shoigu amesema pia kwamba majeshi ya angani ya Urusi yamefanya mashambulizi ya angani zaidi ya 40,000, yakiyalenga maeneo 120,000 ya waasi.
Waziri huyo wa ulinzi wa Urusi amesema majeshi ya Syria hivi sasa yanadhibiti asilimia 90 ya maeneo nchini humo ambayo raia wanaishi. Shirika la kuchunguza haki za binadamu Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema zaidi ya watu 365,000 wameuawa Syria katika kipindi cha miaka saba ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.