30.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

‘Ndoa ya Liwale’ kuponya maumivu kambi za Lipumba na Maalim Seif?

Na LEONARD MANG’OHA


HIVI karibuni gazeti dada na hili, la Rai, liliripoti taarifa za namna ambavyo kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Liwale mkoani Lindi uliofanyika Oktoba 13 mwaka huu zilivyoweza kurejesha mshikamano wa kisiasa ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).

Imani ya kuwapo uwezekano wa pande hizo hasimu yaani ule wa Mwenyekiti  Profesa Lipumba na ule wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, kuweza kuungana inatokama na hatua ya pande hizo kumuunga mkono aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mohammed Mtesa.

Ikumbukwe kuwa hii ni mara ya kwanza kwa pande hizi hasimu kuunga mkono jambo linaloungwa mkono na upande mmojawapo tangu zilipoingia katika mgogoro mwaka 2016, baada ya Profesa Lipumba kurejea ndani ya chama hicho alichokikacha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 akipinga uamuzi wa kupitishwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa mgombea urais chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) licha ya awali kushiriki kumkaribisha katika umoja huo.

Baada ya kurejea mwaka 2016, Lipumba alidai kuwa yeye ndiye mwenyekiti wa chama hicho kutokana na chama hicho kutojibu barua aliyoiwasilisha akiomba kujiuzulu wadhifa huo.

Lakini mgogoro huo uliibua mjadala zaidi baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutangaza kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti jambo ambalo lilisababisha pande hizo mbili kukimbilia mahakamani.

Wakati wanachama wa chama hicho na wananchi wakiwa hawaelewi wapi pa kuelekea, linaibuka hili la pande hizo hasimu kumuunga mkono mgombea mmoja, likaibuka baada ya upande wa Profesa Lipumba kufungua kampeni huku ule wa Katibu Mkuu Maalim Seif ukieleza kuwa ndiye atakayehitimisha kampeni hizo taarifa ambayo ilithibitishwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Mbarala Maharagande, huku akikiri kuwa fomu za mgombea huyo zilipitishwa na NEC baada ya kupelekewa na upande wa Lipumba ambaye anatambuliwa na tume hiyo kutokana na mgogoro ndani ya chama.

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma CUF, Abdul Kambaya, anayewakilisha upande wa Profesa Lipumba, alisema anashangazwa kuwapo kwa mvutano huo, akihoji msingi wa mvutano huo.

“Kwanza tunavutana na nani, mtu ambaye hayupo ofisini, hana nyenzo yoyote ya chama unavutana naye vipi,” anasema Kambaya.

Kutokana na pande hizi hasimu kuonesha nia ya kutaka kumuunga mkono mgombea mmoja katika uchaguzi huo uliomalizika kwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zuberi Kuchauka, kutetea kiti hicho baada ya kujivua uanachama wa CUF na kujiunga na CCM, unaweza kuwa mwanzo mpya wa pande hizi kutafuta suluhu ya mgogoro huu unaokididimiza chama chao.

Kwa sababu mara kadhaa upande wa Prof. Lipumba umekuwa ukieleza wazi kuwa uko tayari kufanya kazi na Maalim Seif kama atafuata taratibu za chama, hii inaweza kuwa nafasi adhimu kwao katika utatuzi wa mgogoro baina yao na kuanza maisha mapya katika ulingo wa kisiasa.

Ili mgogoro huu uweze kutatuliwa ni lazima upande mmoja wa mgogoro ukubali kuwa chini ya mwingine ili kuweza kukaa meza moja kutafuta suluhu ya jambo hili linaloelekea kukipoteza chama hiki kilichojijengea heshima kubwa Zanzibar na baadhi ya maeneo ya Bara kwa kutoa upinzani mkali kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwanza tunapaswa kukubaliana kuwa uamuzi wa Profesa Lipumba kukikacha chama muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 ulikuwa wa kuumiza na wenye kuacha mtikisiko katika chama chake na siasa za nchi hii kutokana na mchango wake kwa upinzani, jukwaani na nje ya jukwaa kiasi cha kushika nafasi ya pili katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 alipoiwakilisha CUF akishindwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.

Vile vile Profesa Lipumba amekuwa miongoni mwa wanasiasa wenye heshima ndani ya nchi kwa kipindi chote hicho, akikumbukwa kwa hoja mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa katika mijadala na majukwaa ya kisiasa.

Maalim Seif ni miongoni wa wanasiasa wenye historia ndefu katika uga wa siasa nchini tangu alipokuwa CCM ambako pamoja na nafasi nyingine aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanzia 1984 hadi 1988.

Baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, alianza historia mpya katika ulingo wa siasa za nchi hii, akiwa miongoni mwa wanachama wa mwanzo na waanzilishi wa CUF na tangu wakati huo Seif ndiye Katibu Mkuu wa chama hicho.

Tangu wakati huo, Maalim Seif, ameendelea kuwa miongoni mwa wanasiasa wenye nguvu ndani ya Chama cha CUF na nje ya chama chake.

Hadi sasa ndiye mwanasiasa aliyegombea urais mara nyingi zaidi kuliko mwanasiasa mwingine yeyote nchini ambapo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 aliwania urais wa Zanzibar kwa mara ya kwanza kupitia chama cha CUF dhidi ya Salmin Amour wa CCM.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Seif alipata asilimia 49.76 dhidi ya 50.24 alizopata Salim Amour.

Mwaka 2000, Maalim Seif, alipata asilimia 32.96 ya kura dhidi ya asilimia 67.04 alizopata Karume mara hii akianguka zaidi ikilinganishwa na 1995.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, umaarufu wa Seif ulionekana kuongezeka baada ya kupata asilimia 46.07 dhidi ya 53.18 alizojinyakulia mshindi wa uchaguzi huo, Abeid Karume, aliyekuwa akitetea kiti chake.

Maalim Seif alirejea katika kinyang’anyiro hicho mwaka 2010 dhidi ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye aliibuka mshindi kwa asilimia 50.1 huku Maalim Seif akipata asilimia 49.1.

Kutokana na mgogoro ulioibuka baada ya uchaguzi huo, yalifikiwa makubaliano ya kuundwa kwa Serikali ya umoja wa kitaifa ambapo Maalim Seif aliteuliwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar nafasi ambayo alidumu nayo hadi mwaka 2015.

Vile vile katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 jina Maalim Seif lilikuwamo katika orodha ya wagombea kabla ya Tume ya Uchaguzi (ZEC) kutengua matokeo ya uchaguzi huo na kuamuru urudiwe Machi mwaka 2016.

Kwa wasifu wa viongozi hawa ni wazi kwamba wote wanahitajika ndani ya CUF ili kuhakikisha wanakijenga chama hicho kuendelea kuwa shindani kama awali na hili linawezekana endapo pande husika zitaamua kufanya hivyo.

Kama kila upande utaendelea kujiona bora kuliko mwingine, siuoni uhai mrefu wa CUF katika ulingo huu wa siasa, badala yake vyama vingine vitaendelea kukimegua chama hiki kwa kuchukua wanachama wake ikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kimeonesha nia ya kumnyakua Maalim Seif kuwa mgombea wake katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Nadhani upande wa Maalim Seif unayo nafasi kubwa ya kuiinua CUF kwa kukubali kukaa chini na hasimu wake kutafuta mwafaka wa chama chao kwa masilahi ya Taifa.

Ninaamini hili kwa sababu licha ya Profesa Lipumba kutajwa kama kiini cha mgogoro huu, pia upande uliobaki wakati huo haukuchukua hatua stahiki kukomesha uongozi wake baada ya kuomba kujitoa katika nafasi ya uenyekiti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles