MOSCOW, URUSI
URUSI imeadhimisha mwaka wa tano tangu ilipoliteka jimbo la Crimea lillilokuwa sehemu ya Ukraine katika sherehe zilzoongozwa na Rais Vladimir Putin jana.
Rais Putin aliwasili jimboni humo na kuhudhuria maadhimisho hayo kwenye mji mkuu wa jimbo hilo, Sevastopol.
Hatua hiyo ya Urusi ya kuliteka jimbo la Crimea mwaka 2014 ililaaniwa vikali na Ukraine na nchi za magharibi lakini ilipongezwa na Warusi wengi.
Ikulu ya Urusi imesema katika taarifa kuwa kilichotokea miaka mitano iliyopita ni kujiunga tena kwa rasi ya Crimea na Urusi.
Rais
Putin jana alifungua kituo kikubwa kipya cha nishati pamoja na kukutana na
wanaharakati wa asasi za kiraia.
Awali miaka mitano iliyopita Rais huyo alitia saini mkataba na wawakilishi wa
Crimea ili kuhalalisha jimbo hilo kuwa sehemu ya Urusi, muda mfupi tu baada ya
kufanyika kura ya maoni ambayo haikutambuliwa na jumuiya ya kimataifa.
Waziri wa Mambo ya nje wa Ukraine, Pavlo Klimkin amesema miaka yote mitano imejenga mazingira ya ugaidi dhidi ya watu wa Crimea.
Lakini pia utafiti uliofanywa mapema mwezi huu umebainisha kuwa ni asilimia 39 tu ya Warusi wanaoamini Crimea imeleta manufaa kwa Urusi.
Mwaka 2014 Warusi waliounga mkono uvamizi huo walikuwa asilimia 67 wakisema kutekwa kwa Crimea kulileta manufaa zaidi kuliko hasara kwa Urusi.