29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Wapatanishi wa Uhuru, Ruto wakana kuwapo mpango wa kurithisha

NAIROBI, KENYA

WANASIASA waliohusika katika kuwaunganisha Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2013, wamekanusha kuwapo makubaliano ya kurithishana urais mwaka 2022.

Maafisa wa vyama vilivyovunjwa vya The National Alliance (TNA) na United Republican Party (URP), wamefichua kuwa maelewano yaliyokuwepo yalihusu kipindi cha kwanza cha utawala wao hadi mwaka 2017.

Wakati huo, Rais Kenyatta alikuwa kiongozi wa TNA naye Dk. Ruto akiwa kinara wa URP.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa TNA, Onyango Oloo  ambaye pamoja na mwenzake wa URP, Davis Chirchir na maafisa wengine kama vile Johnson Sakaja (Mwenyekiti TNA) na Francis ole Kaparo (Mwenyekiti wa URP) walikuwa na majukumu muhimu katika makubaliano hayo.

“Nilikuwa Katibu Mkuu wa TNA na bado ninakumbuka vyema. Mkataba tuliopeleka kwa msajili wa vyama vya siasa ulistahili kudumu kwa miaka mitano,” alisema Oloo ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya masuala ya sheria wakati Chama cha Jubilee kilipoundwa Septemba 2016.

“Mkataba ulisema kama tungeshinda, Uhuru angekuwa Rais na Ruto Naibu Rais, na Serikali itaundwa kwa kugawana madaraka kwa nusu. La muhimu zaidi kwenye makubaliano hayo, ambayo nilitia sahihi pamoja na wenzangu watatu, ni kwamba hapakuwa na sehemu yoyote iliyosema Uhuru angehudumu kwa miaka mitano au 10, kisha ampishe Ruto kuongoza kwa miaka mingine mitano au 10,” alisema.

Aliongoza: “Hayo mengine ni maoni ya wanasiasa tu, ambao wanaamini wana haki kurithi urais kutoka kwa Uhuru.”

Oloo alisema ushirikiano wa Rais Kenyatta na Dk. Ruto ulionekana kama njia muhimu ya kuwawezesha kupata mamlaka ya kisiasa, ili iwasaidie kukabiliana na kesi kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Kwa upande wake, Kaparo pia alisema hapakuwa na makubaliano Rais atamkabidhi mamlaka naibu wake.

“Sidhani kulikuwa na kitu kama hicho. Lakini hata kama kingekuwepo, hivyo vilikuwa vyama viwili tofauti; URP na TNA, ambavyo kwa sasa havipo,” alikumbushia Kaparo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles