27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Upinzani DRC wasambaratika

KINSHASA, DRC



MUUNGANO wa vyama vya upinzani nchini hapa umegawanyika baada ya kuteuliwa kwa Martin Fayulu kuwa mgombea pekee wa urais kwenye uchaguzi ujao Desemba 23.

Kwa mujibu wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani – DW, vigogo wa vyama vikuu, kikiwemo UDPS, wametupilia mbali chaguo la viongozi wao hapo juzi mjini Geneva, Uswisi, huku wafuasi wa vyama hivyo wakielezea huzuni yao kuhusu uteuzi huo, licha ya mashirika ya kiraia kuipongeza hatua ya upinzani ya kuweka mgombea mmoja kwenye uchaguzi wa rais.

Katika Makao Makuu ya UDPS yaliyopo katika mtaa wa Limete, DW iliwakuta wafuasi hao wakijadili uteuzi huo wa Fayulu kuwa mgombea wa upinzani.

Taarifa hiyo imezusha mshangao kuona kwamba kiongozi wao Felix Tshisekedi hakuteuliwa kuwa mgombea pekee wa upinzani.

Mfuasi wa UDPS, Jean –Yves Kamale alisema ni vigumu kuamini walichofikia viongozi saba wa upinzani huko mjini Geneva.

“Nimehuzunishwa sana, nimehuzunishwa sana kuona kwamba Kamerhe, Bemba, Matungulu, Felix, Katumbi na Muzito kumteua Martin Fayulu kuwa mgombea wetu… nini Fayulu anaweza kuchangia kwenye upinzani? Hana ngome yoyote… Ukienda kwenye jimbo jirani la Kongo ya Kati nani anamjua Fayulu?” alihoji mfuasi huyo.

Vigogo wa UDPS waliobaki mjini hapa pia wametupilia mbali uteuzi wa Fayulu, huku wakiahidi kuitisha mkutano wa chama baadaye jana.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Augustin Kabuya alisema chaguo hilo haliwezi kukubalika na wafuasi wao.

Kwenye chama kingine cha upinzani cha UNC kinachoongozwa na Vital Kamerhe nako kumeibuka papandembili tofauti zinazopingana baina ya viongozi wake.

Msemaji wa chama hicho, Jolino Makelele, amepongeza uteuzi wa mgombea mmoja, lakini mkuu wa tawi la vijana, Billy Kambale, alisema kwa vyovyote vile Kamerhe atagombea kiti cha urais.

Lambert Mende ambaye ni msemaji wa mgombea wa chama tawala, Ramazani Shadary, alikataa kutoa maoni yake kuhusu uteuzi huo, lakini aliiambia DW kwamba wapigaji kura ndio watakaotoa uamuzi wa mwisho kwa wagombea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles