27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wanazuoni wabakie hai, wasiwe wafu

Na ALOYCE NDELEIO



TANGU kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania umekuwapo uhusiano uliojaa taswira ya uhusiano kati ya paka na panya ambao umekuwa katika makundi ya kijamii iwe kwa wanasiasa wenyewe, wanataaluma, na wananchi wa kawaida kila moja likijibandika katika  masuala ya kiitikadi.

Uhusiano wa paka na panya  uliopo kati ya wanasiasa hususani waliopo upande wa upinzani na serikali huwa unakuwapo hususani inapotokea waliokuwa upande wa upinzani kufungamana na chama kilichopo madarakani.

Baadhi ya watu na hususani wanataaluma hujikuta wakiwa katika uhusiano wa paka na panya kati yao na jamii na hususani wengine wanapokuwa  wamefahamika kutokana na shughuli zao za kisiasa kuliko  inavyokuwa kwenye shughuli zao za ufundishaji au kazi zao za utafiti.

Katika shughuli za kisiasa wanaweza kuwa  ni watu waliokuwa wanatoa kauli, maoni au ushauri kwa serikali, au kuikosoa serikali ili iweze kuwajibika katika mahitaji ya msingi ya wanajamii.

Aidha pale inapotokea baadhi ya wanazuoni kufungamana na serikali ambayo walikuwa wanaikosoa kutokana na kuteuliwa kujiunga katika mifumo ya uamuzi mara nyingine hujikuta wakiangushiwa lawama kwamba wamefikia ukomo wao wa kukosoa au kuisemea jamii.

Kwa baadhi ya wanajamii humuona mwanazuoni anayeingia katika mkondo huo na kulingana na taaluma yake huonekana kuwa hataweza tena kutoa kauli zinazoweza kuisaidia jamii na huenda mbali zaidi kuitwa ni ‘Mtu Mfu’.

Hali hiyo husababishwa na sababu zinazoonekana kuwa   mtu huyo amenyamazishwa na kukaa kimya  kutokana na kukubaliana na utawala ambao hudhaniwa au kuonekana kuwa ni wa kiimla.

Hata hivyo kinachokuwa kimebainika baadaye ni kwamba hiyo ndiyo falsafa anayoweza kusulubiwa nayo  mtu anapokuwa ameungana au kufungamana na serikali hiyo na hivyo kuwa anakwenda au kujikuta akitekeleza majukumu kulingana na majukumu anayokuwa amekabidhiwa ayasimamie au ayatekeleze.

Katika mazingira mengine ni kwamba pindi inapotokea serikali kumpatia nafasi ya utendaji walio wengi huwa na fikra kuwa ingefaa mtu huyo aikatae  nafasi hiyo kutokana na kinachodhaniwa kuwa ni kuwapo kwa sera za serikali zilizokosa umaarufu.

Mara nyingi huelezwa kuwa kukosekana kwa umaarufu huo kunakuwa kumesababishwa na hali ngumu ya uchumi, kupigwa marufuku au kuvibana vyama, utendaji wa vyombo vya dola na hata hivyo kwa upande mwingine hali hiyo inaweza kusababishwa na matumizi mabaya ya rasilimali za umma kama si matumizi mabaya ya madaraka.

Walio wengi hukasirika kwamba ni kwanini mtu  anakubali nafasi hiyo. Unakuwapo mtiririko ambao humsabahi na kumshangaza hata mpokeaji. Lawana huwa ni kwanini amefungamana na serikali ambayo  imekuwa inalea sera nyingi zisizo maarufu.

Hufikia hatua ya kujiuliza kwamba  hawakuona  jambo baya  kuhudumu katika utawala huo  ambao umenyonga ‘mikondo’ (Hiyo mikondo huwa haitajwi lakini kwa walio na uelewa hutambua ni mikondo ya kifujaji au ya kujineemesha).

Wapo ambao huhoji kwanini akubali kupokea nafasi hiyo na hata kufikia hatua ya ‘hana haki ya kukalia kiti hicho’ na hata kunyambua  kuwa anaingia katika kundi la kuendesha magari katika barabara iliyojaa mashimo  lakini hawayaoni wanapita tu.

Huwapo lawama kwamba wanakula na kunywa ndani ya mfumo ambao utaziweka au kuzidhoofisha taaluma zao na kuzifanya  kama vyeo vya machifu ambavyo haviangalii taaluma zaidi ya kuonekana kama vile wamezaliwa katika mkondo au  ukoo wa kichifu.

Pindi wasomi hao wanapoibuka wakiwa na utetezi au kuwa na hoja za kujitetea kwamba hao wanaopinga au kupigia kelele kwamba wanaweza kuwa na maadili kiasi gani  ya kupokea udhamini au ruzuku  kutoka mamlaka za kisiasa ilhali wengine hawana rekodi safi hufanya hoja za lawama kusinyaa.

Mwanazuoni mmoja aliwahi kutoa hoja moja ya utetezi akisema kuwa wapo kwenye kongamano ndani ya ukumbi akisema, “Itakuwa vipi kwa kila mmoja  hapa tulipo katika kongamano hili linakuja kundi la watu wapo katika maandamano likiwa limejaza wafanyakazi na wanafunzi wanawapita walinzi, katika lango la kuingia, wanavamia ukumbi wakiwa na vitu vya mlipuko na mabango wakipiga kelele tuondokeeni hapa, hamtujali…”.

Baada ya kusema hivyo akaibua swali kwamba mwitiko kwa hali ya aina hiyo kwa kila mmoja itakuwa vipi? Badala ya kupata jibu wakabaki wanatazamana  kwa kukanganyikiwa na hapo ndipo ilipobainika kwamba wanazuoni hao wapo vizuri na hai na si mfu  kama inavyoweza kudhaniwa.

Hata hivyo zikawepo fikra  kwamba huenda ikawa ni fursa nzuri kwao ya kupambana na kadhia zinazoikabili jamii wakiwa ndani ya mfumo kuliko wakiwa pembeni, wakitumia maoni, ushauri na hata tafiti zao na kuendelea kuwa hai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles