JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limetangaza operesheni kali ya kuwaondoa wapigadebe katika vituo mbalimbali vya mabasi.
Uamuzi huu wa polisi, si wa kwanza kutangazwa maana kwa kipindi kirefu tumekuwa tukisikia agizo kama hili, lakini mafanikio yamekuwa hayaonekani.
Polisi wanasema wamefikia uamuzi huo, baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
Miongoni mwa malalamiko hayo, ni hatua ya wananchi wengi kulalamikia kukithiri kwa vitendo vya kihalifu ikiwamo uporaji, ambavyo hufanywa na baadhi ya wapigadebe katika vituo vya basi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alisema kwa muda mrefu wezi katika vituo vya daladala wamekuwa wakifanya uhalifu kwa mwamvuli wa upigaji dege.
Tamko la polisi la kuagiza kuwaondoa wapigadebe katika vituo hivyo, linaweza kuwa ni sawa na mchezo wa kuigiza.
Tunasema hivyo kwa sababu Dar es Salaam ina vituo vingi vya daladala na magari mengi, ikilinganishwa na idadi ya polisi ambao hawawezi kusambazwa kwenye vituo vya mabasi, hasa nyakati za jioni na asubuhi.
Jambo hili linatupa wasiwasi mkubwa iwapo dhamira ya polisi ya kuwaondoa wapigadebe itafanikiwa kama walivyokusudia.
Kwa mfano leo ukifika katika kituo cha mabasi cha Ubungo ni aibu kutokana na kutapakaa kwa wapiga debe ambao baadhi yao wamekuwa wakifanya uhalifu.
Jambo hili limekuwa kero kubwa kwa sababu msafiri hujikuta akivutwa huku na kule utafiriki ni mchezo wa kuigiza.
Hili halina ubishi hata kidogo, hapo ndipo wasafiri wengi hujikuta wanapoteza au kuibiwa na hata wanapokwenda kushtaki polisi inakuwa kumpata mhusika eneo lilelile.
Kwa mfano, mwaka mmoja uliopita Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),George Simbachawane aliwahi kutoa agizo kwa mamlaka za Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha zinawaaondoa wapigadebe wote kwenye vituo vya mabasi kwa madai kuwa wanafanya vitendo vya kihalifu.
Alisema kazi ya kupigadebe si rasmi na haina kipato kitakachoweza kumkwamua kijana kuondokana na tatizo la umasikini.
Ni kweli kwamba inawezekana wasiwe na kipato kikubwa cha kuwakwamua na umasikini, lakini umefika wakati mamlaka husika kuweka njia mbadala za kuwezesha vijana hawa.
Tunaamini wapo wakubwa na wadogo ambao wanategemea kuendesha maisha yao ya kila siku kwa kujipatia kipato hicho.
Je mamlaka zinazohusika zimewahi kuwaita na kuwapa darasa la ujasiriamali ambao utawawezesha kuondokana na hali hiyo?
Kama hakuna umefika wakati mzuri sasa wa kufanya hivyo, badala ya kutanguliza vyombo vya dola.
Sisi MTANZANIA, tunasema katika suala hili polisi wachukuwe hatua zinazostahili bila kumwonea mtu wala kumbambikizia kesi eti kisa tu amekutwa kwenye kituo cha daladala.
Tumeshuhudia vitendo vya aina hiyo ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa na vijana wengi wanaokamatwa kwenye operesheni za aina hii ambazo kwa kweli zimekuwa ni za zima moto.
Kwa msingi huo, hatutegemei kupita tena maeneo ya daladala na kukutana na wapigadebe. Huu ndiyo mtihani wa kwanza wa Kamanda Mkondya ambaye amekaimu nafasi hiyo baada ya mtangulizi wake Simon Sirro kupandishwa cheo hivi karibuni.
Tunamalizia kwa kusema operesheni hii, isiwe nguvu ya soda kama ambavyo tumezoea kuona.