24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

UNAJUA KILICHOPO KWENYE NDOA? – 3

MARAFIKI tunaendelea na mada yetu kama inayoonekana hapo juu. Kwa wiki mbili mfululizo nimelizungumzia hili kwa mapana, lakini bado kuna vitu vya kujadiliana zaidi. Karibu tuendelee na darasa letu…

VIPI NDUGU ZAKE?

Kama ni kweli una matarajio mazuri kutoka kwa mwenzako, kipegele hiki ni muhimu kabla ya kufanya uamuzi wa kuingia kwenye ndoa.

Lazima uijue vizuri familia yake. Anatoka katika familia ya namna gani? Kabila gani? Ukiachana na hilo, hapa lazima ufahamiane na ndugu zake, japo kidogo na upate muda wa kuwazoea.

Kuna familia nyingine ni wakorofi, kama ukiolewa huko ni tabu tupu. Pengine ukiona katika familia yao, labda wana tabia ya udokozi…si ajabu ukaibiwa hata wewe.

Kweli umempenda na unataka kuishi naye, lakini utaratibu mbaya wa ndugu zake ni kielelezo cha matarajio ya maisha yenu ya ndoa. Kuwa makini.

 

UNAIJUA AFYA YAKE?

Baadhi ya watu kwa bahati mbaya wana matatizo ya kiafya ya kudumu. Utakuta huyu ana udhaifu wa kusumbuliwa na shinikizo la damu, mwingine vidonda vya tumbo, kifafa n.k.

Ni udhaifu ambao yeyote anaweza kuwa nao. Kwa nini nimegusia hili? Kuna baadhi ya rafiki zangu wanaingia kwenye ndoa wakiwa hawajui matatizo ya wenzao, hivyo kusababisha matatizo.

Hujui mwenzako anasumbuliwa na nini, mnagombana kidogo unaanza umpiga, unashangaa ameanguka chini, damu zinaanza kumiminika puani! Si kosa lako, maana hukujua!

Hapa kuna umuhimu mkubwa sana wa kujua afya ya mwenzako. Kama ana maradhi ya kudumu ni vyema ukajua, ili pia ufahamu utakavyotakiwa kuishi naye ndani ya ndoa.

Hakikisha unaijua historia ya afya yake vema. Hakuna maana mbaya kufahamu, isipokuwa utakuwa na uwezo wa kumchukulia kulingana na udhaifu wake.

 

MILA NA DESTURI

Kuna makabila mengi sana nchini, kila watu wana mila zao, lazima uzijue japo kwa ufupi. Unaweza kuzungumza naye au ukawashirikisha watu wazima ambao wana ufahamu mkubwa, watakusaidia.

Unaweza kuingia kwenye kabila ambalo mila zake siyo nzuri ikakuletea shida, lakini ukifahamu mapema itakusaidia kufanya uamuzi sahihi.

 

KUHUSU DINI

Inapendeza zaidi kama mkioana ndani ya imani moja ya dini. Upo utararibu wa wachumba kufunga ndoa bomani, ambapo kila mmoja huwa na dini yake. Siku za hivi karibuni wengi wanafanya hivi, lakini si sahihi kwa asilimia mia moja.

Ndoa imara, ukiacha juhudi za wahusika wenyewe hujengwa na hulindwa na imani thabiti ya dini ya wahusika. Mnapokuwa katika imani moja, ni rahisi kumfikia Mungu pamoja katika maombi au kwenda kwa viongozi wa dini moja na kupewa ushauri wa kiroho.

Jambo hili lisiwe la mwisho, kama tayari dalili za kuoana zinaonekana wazi, muanze kujadiliana mapema juu ya suala la dini. Lazima muwe madhehebu moja, kama mpo tofauati, mshauriane ili mmoja amfuate mwenzake. Hakuna kinachoshindikana kwenye mazungumzo.

 

MNIE MAMOJA

Hapa namaanisha kwamba ili ndoa yenu iwe bora lazima kuanzia mapema muwe na nia moja kwa kila jambo. Sina lugha nyepesi sana ya kudadavua hili, lakini kikubwa ni kwamba mnapaswa kuwa na mawazo ya aina moja kwa maana ya kushirikishana tangu mapema.

Jengeni mazoea ya kushirikishana kila kitu. Hii itawajengea uaminifu na kila mmoja kujiona sehemu ya mwenzake.

 

Kwanini yote hayo?

Ndiyo taswira ya kile unachokiendea ndani ya ndoa. Ikiwa uhusiano wenu awali haukuzingatia niliyoyataja hapo juu, matarajio ya ndoa yako yatakuwa kinyume.

Acha utaratibu wa kuamini kwamba kwenye ndoa kuna furaha, kuna starehe tu, kuna kusaidiana tu. Zipo changamoto ambazo lazima ukubaliane nazo au ujiandae kukutana nazo kuanzia mapema.

Kwa hakika hayo yakifuatwa kwa makini, ndoa yenu itakuwa bora na bila shaka utakuwa na matarajio mema katika ndoa yako ijayo.

Naishia hapa kwa leo, hadi wiki ijayo katika mada nyingine. HUTAKIWI KUKOSA!

 

Jiandae kupokea kitabu changu kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachokuwa mitaani hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles