28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

VYETI FEKI: WATUMISHI WENGINE 100,000 MATUMBO JOTO

Rais Dk. John Magufuli akiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakiangalia vitabu vyenye majina ya watumishi wa umma 9,932 waliogushi vyeti vyao vya elimu.

 

 

Na EVANS MAGEGE – Dar es Salaam

SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kupokea ripoti ya awamu ya kwanza na pili ya uhakiki wa vyeti vya kitaaluma vya watumishi wa umma ambayo imebaini watumishi 9,932 wana vyeti vya kughushi, watumishi wengine wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 100,000 nao hatima yao itajulikana ndani ya siku tano zijazo.

Watumishi hao ni wale wanaofanya kazi Serikali Kuu, kwa maana ya wafanyakazi wa wizara 18 isipokuwa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambayo tayari ripoti yake imekwishawasilishwa juzi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema ripoti ya tatu ya uhakiki itawasilishwa Ijumaa ijayo na imegusa wizara zote.

Alifafanua kwamba ripoti aliyoiwasilisha juzi kwa Rais Magufuli, ilikuwa ya awamu mbili ambazo ziligusa mamlaka za Serikali za mitaa na sekretarieti za mikoa, taasisi za Serikali, mashirika ya umma, tume na wakala za Serikali.

Kwa mujibu wa Kairuki, ripoti iliyowasilishwa juzi iligusa asilimia 75 ya watumishi wote wa Serikali.

Kwa msingi wa maelezo hayo, MTANZANIA Jumapili lilifanya makadirio ya kimahesabu kwa kuangalia kama asilimia 75 ya watumishi waliohakikiwa ni 400,035, basi asilimia 25 iliyobaki huenda ikawa ni watumishi 133,345.

Kwa mantiki hiyo, hatima ya watumishi hao itajulikana Ijumaa ijayo wakati ripoti yao itakapowasilishwa kwa Rais Magufuli.

Awali gazeti hili lilitaka kufahamu idadi ya watumishi wote wa umma, lakini ilishindikana baada ya Kairuki kusema kuwa anayefahamu hilo ni Katibu Mkuu Kiongozi, huku Ikulu nayo ilidai kuwa suala hilo lipo chini ya waziri huyo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Kairuki alisema katika mazingira aliyokuwapo ni vigumu kupata idadi moja kwa moja, hivyo akamshauri mwandishi amtafute Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi.

“Sasa unaniulizia hapa nitakujibu kweli? Mpaka na mimi niwasiliane na watu wangu au mpigie Katibu Mkuu labda yeye anaweza akawa na hizo takwimu karibu kwa sababu si unajua leo wanafutwa, mara wameondolewa  wengine. Basi wewe mpigie Katibu Mkuu, usipompata nitumie ujumbe mfupi wa maneno nimtafute,” alisema Waziri Kairuki.

Juhudi za kumpata Kijazi ziligonga mwamba baada ya simu yake kutokuwa hewani.

MTANZANIA Jumapili lilipowasiliana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, alisema mwenye dhamana ya kuzungumzia jambo hilo ni Waziri Kairuki.

Alipotafutwa kwa mara nyingine Waziri Kairuki, simu yake haikupokewa kila ilipopigwa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa mawasiliano kwa mujibu wa agizo lake, hakujibu chochote hadi gazeti hili linakwenda mtamboni.

Juzi wakati akiwasilisha ripoti ya awamu ya kwanza na ya pili, Kairuki alikaririwa akisema; “Ukiangalia watumishi wengi wako ngazi za halmashauri ambako wanafikia kati ya asilimia 75 hadi 80 na sisi ndio tumeanza hao, Ijumaa tunapata ripoti ya mawizara.”

 

ILIVYOKUWA JUZI

Waziri Kairuki akiwasilisha ripoti ya awamu ya kwanza na pili ya uhakiki wa watumishi wa umma mbele ya Rais Magufuli, alisema mpango wa uhakiki kwa watumishi wa umma haukuwagusa mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, kwa sababu sifa wanazotakiwa kuwa nazo ni kujua kusoma na kuandika pekee.

 “Uhakiki uliwahusu watumishi wa umma pekee, wakiwamo makatibu wakuu wote na viongozi mbalimbali katika ngazi ya utumishi wa umma.

“Hatua hii inatokana na ukweli kwamba kwa mujibu wa sheria, pamoja na miundo ya maendeleo ya utumishi serikalini, wanatakiwa kuwa na sifa za msingi za kuingilia na kutumikia nafasi zao ikiwa ni pamoja na vigezo vya elimu na vigezo vya kitaaluma, hivyo uhakiki haukuwahusisha viongozi wa kisiasa.

“Mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya na madiwani kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, wote mnafahamu uteuzi na uchaguzi unafanyika kwa misingi ya wahusika kuwa na sifa ya kujua kusoma na kuandika.

“Na hii ni kwa mujibu wa Ibara 61(1) ya Katiba, isije ikaonekana ni maneno ya Kairuki,” alisema.

Alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa kuimarisha usimamizi na mifumo maalumu, hususani ya upokeaji wa taarifa za watumishi ili kubaini wanaotumia vyeti vinavyofanana.

Kairuki alisema kwa kuzingatia maelezo ya Rais Magufuli, ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, ilielekeza Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kufanya uhakiki wa vyeti vya kidato cha nne, sita na ualimu.

Alitoa mfano wa nchi zilizowahi kufanya ukaguzi kama huo kuwa ni pamoja na Afrika Kusini, lakini haikuweza kuwafikia watumishi wote kwa wakati mmoja.

Akifafanua kilichogundulika kwenye ukaguzi, alisema kati ya watumishi 400,035  waliokaguliwa, 376,969 wamebainika kuwa vyeti vyao ni halali ambao ni sawa na asilimia 94.23, wengine 9,932 sawa na asilimia 2.4 wameghushi.

“Alama za siri pamoja na mhuri uliopo katika vyeti hivyo haufanani na vyeti husika vilivyotolewa na baraza hilo, kundi la tatu ni wenye vyeti vyenye utata ambao ni 1,538 sawa na asilimia 0.3 na vyeti hivyo vinatumiwa na watumishi 3,076. Hii inamaanisha kuwa cheti kimoja kinatumika na watumishi zaidi ya mmoja na vingine watumishi wawili hadi watatu.

 “Kundi la mwisho waliowasilisha vyeti pungufu ni 11,596 sawa na asilimia 2.8. Waliwasilisha vyeti vya kitaaluma. Inatutia shaka kwa sababu haiwezekani ukaenda kupata sifa ya kujiunga na vyuo vya kitaaluma haukuwa na cheti cha kidato cha nne na sita, baraza limewataka waajiri kuwasilisha vyeti hivyo ili wafanye uhakiki,” alikaririwa Kairuki juzi wakati akikabidhi ripoti ya awamu ya kwanza na pili.

Alisema kughushi cheti ni kosa la jinai na hatua za kisheria zitachukuliwa si kwa waliogushi tu, bali pia kwa mawakala wanaotengeneza na kuuza vyeti.

Kwa mujibu wa Kairuki, kanuni za kudumu za utumishi wa umma, zinasema mwombaji wa ajira serikalini akitoa taarifa za uongo na zikathibitika baada ya kuajiriwa, atachukuliwa hatua za kinidhamu na jinai.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles