24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Umuhimu wa kipimo cha ukakamavu kwa afya

Ruud van Nistelrooy aliwahi kushindwa kipimo cha ukakamavu.
Ruud van Nistelrooy aliwahi kushindwa kipimo cha ukakamavu.

Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD

 VITU vikubwa na muhimu katika michezo ambavyo binafsi hudhani kwamba hupuuziwa hapa nchini ni kitu kile ambacho kitaalamu hujulikana kama fitness test au exercise test (kipimo cha ukakamavu).

 Kupata picha halisi ya mada tutakayojadili leo, kwa wale mnaofuatilia mchezo wa soka kwa karibu mtakuwa na kumbukumbu za kushindikana katika dakika za mwisho kwa baadhi ya mipango ya kuhamisha wachezaji maarufu kutoka katika timu moja kwenda nyingine.

Katika historia takribani wachezaji maarufu 17 wa soka la kulipwa wamepata kushindwa kipimo cha ukakamavu au fitness test hivyo kushindikana kwa uhamisho ama usajili wao.

Mifano michache ni pamoja na Leroy Fer, mholanzi na mchezaji wa kimataifa aliyeshindwa kuhamia katika timu ya Sunderland mwaka 2015, kutokana na kufeli au kushindwa kipimo cha ukakamavu. Ferr alishindwa kipimo hiki kutokana na kuwa katika matibabu ya ligament, kitu ambacho kilimkosesha fursa ya kufanya mazoezi ya kutosha na hivyo kutokuwa fit. Mchezaji huyu huyu amewahi pia kushindwa kipimo kama hicho mwaka 2013, alipokuwa akichezea timu ya Everton.

Mwingine ni mchezaji maarufu Ruud van Nistelrooy aliyeshindwa kipimo hicho baada ya kupata majeraha alipokuwa akiichezea timu ya Manchester united. Kushindwa huko kulimlazimu asubiri na kuanza tena kucheza mwaka mmoja baadaye.

Mfano mwingine ni John Carew ambaye alitakiwa kuungana na kikosi cha Inter Milan miezi saba baada ya kuondoka West Ham. Mipango hiyo ilishindikana  kutokana na mchezaji huyo kushindwa au kufeli fitness test.

Mifano iliyotolewa hapo juu ni kutokana na kushindwa fitness test ambayo ni sehemu moja tu ya uchambuzi wa kina wa afya unaofanywa kwa mchezaji kabla ya kuuzwa au kusajiliwa na timu. Wako wachezaji kama George Boyd ambaye uhamisho wake kutoka katika timu ya Poterborough kwenda Nottingham Forest ulishindikana kutokana na majibu ya kutatanisha kuhusu afya ya macho yake.

Lakini ikumbukwe pia kwamba Mnaijeria Nwankwo Kanu aligundulika kuwa na tatizo la moyo wakati wa fitness test iliyofanyika akiwa tayari amesajiliwa katika timu ya Inter Millan, tatizo ambalo lilichangia Nwanko kufanyiwa upasuaji wa moyo baadaye.

Sasa itakuwa rahisi kuelewa maana ya fitness test au kipimo cha ukakamavu na umuhimu wa kipimo hiki kwa afya na katika michezo.

Kwa kifupi kipimo cha ukakamavu ni kipimo kinachopima na kutoa fursa ya kufahamu uwezo, ukakamavu wa mchezaji au mtu anayefanyiwa kipimo hicho. Sehemu muhimu ya kipimo hiki ni ile inayopima uwezo wa mfumo wa moyo na ule wa mapafu (cardi-pulmonary) katika kukabiliana na kuhimili kazi ngumu kama vile mazoezi na michezo. Kipimo hiki pia hupima uwezo wa misuli kutumia hewa ya oksijeni (VO2max). Misuli ya watu wenye uwezo mkubwa na ukakamavu huweza kutumia oksijeni nyingi zaidi ukilinganisha ya wale wasio na uwezo mkubwa.

Kutokufanya mazoezi mara kwa mara, kupumzika kwa muda mrefu kutokana na majeraha au hata kutokuwa na uwezo na viwango ni mojawapo ya vitu ambavyo humsababisha mtu kutokuwa mkakamavu (low fitness levels), hivyo kushindwa au kufeli kipimo hiki.

Kama tulivyokwisha kuona kufahamu fitness ya mchezaji ni muhimu maana hii huelezea kiwango na uwezo wake katika michezo. Timu zinazonunua na kusajili wachezaji bila kufanya kipimo hiki ni dhahiri kwamba zinakuwa zinabahatisha na kutabiri uwezo wa wachezaji hao, wakati teknolojia inatoa fursa ya kuweza kufahamu uwezo huo kwa uhakika zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles