25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ndoa za utotoni zinavyochangia maambukizi ya VVU

picha
Msichana huyu wa Kijiji cha Namikupa Tandahimba ni miongoni mwa waliokatisha masomo baada ya kupata mimba za utotoni.

 

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

NDOA na mimba za utotoni zinatajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa mtoto wa kike nchini kuweza kufikia ndoto zake za baadae kama ilivyo kwa mtoto wa kiume.

Shirika la Afya Duniani (WHO),linaitaja Tanzania kuwa ni moja kati ya nchi zenye viwango vya juu vya matukio ya ndoa za utotoni.

Utafiti uliofanywa na Shirika hilo na kuchapishwa Januari mwaka huu, uliitaja Tanzania kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa matukio ya ndoa na mimba za utotoni kwa kiwango cha asilimia 28.

Takwimu kutoka Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), zinaeleza kwamba kwa wastani watoto wa kike wawili kati ya watano huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 nchini.

Kulingana na Shirika hilo, takwimu zinaonesha asilimia 42 ya wasichana barani Afrika huolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 hivyo suala hilo si la kufumbiwa macho.

Aidha, takwimu za utafiti wa Idadi ya watu na Afya Tanzania (TDHS, 2010) zinaonesha asilimia 37 ya watoto wa kike Tanzania huolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini (NBS), zinautaja Mkoa wa Shinyanga kuwa ndio unaoongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni kwa kiwango cha asilimia 59.

Kwa mujibu wa NBS, Mkoa unaofuata ni Tabora ambao una asilimia 58, Mara (55), Dodoma (51), Lindi (48), Mbeya (45), Morogoro (42), Singida (42), Rukwa (40) na Ruvuma (39).

Mikoa mingine yenye idadi kubwa ya ndoa za utotoni ni Mwanza (37), Kagera (36), Mtwara (35), Manyara (34), Pwani (33), Tanga (29), Arusha (27), Kilimanjaro (27), Kigoma (29), Dar es Salaam (19) na Iringa asilimia nane.

Utafiti uliofanywa katika kipindi cha mwaka 2012/13 na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) ulionesha jumla ya matukio 228 ya mimba na matukio 42 ya ndoa za utotoni yaliripotiwa katika kipindi hicho.

Sababu kuu zinazotajwa kuchangia kukua kwa tatizo hilo ni mila na desturi potofu, sheria na sera kinzani, mifumo dhaifu ya uongozi katika ngazi ya kata, vijiji, Mitaa na vitongoji.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Afya ya Uzazi, katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hussein Kidanto, anasema ndoa za utotoni kwa kiasi kikubwa zinachangia ongezeko la idadi ya watu wanaopata maambukizi ya virusi vya ukimwi nchini.

Anasema pia zinachochea ongezeko la watu wanaougua saratani ya shingo ya kizazi ambayo inatajwa kuwa miongoni mwa magonjwa yanayopoteza maisha ya wanawake wengi.

“Kundi la vijana ambalo ni kubwa lazima wapewe elimu, hawa ndio Taifa letu la leo…tunashuhudia  ongezeko kubwa la ndoa za utotoni hivyo ni vema wakipata elimu hii ili wajue jinsi ya kujilinda,” anasema Dk. Kidanto.

Anasema pamoja na hayo bado ipo haja ya wadau, serikali na jamii kuunganisha nguvu za pamoja kuzikemea ndoa na mimba za utotoni.

“Hili ni jambo la msingi kwa sababu kama nilivyoeleza hapo awali zinachangia pia kuongezeka kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi na hata saratani ya mlango wa kizazi, tukikaa kimya maana yake ni kwamba idadi hiyo itaendelea kuongezeka mara dufu,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles