28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mambo yanayosababisha matatizo wakati wa kujifungua

1-0

NA JOACHIM MABULA,

KADIRI mwanamke anavyofahamu mambo mengi zaidi kuhusu mimba yake ndivyo alivyo na nafasi nzuri ya kufanikiwa kujifungua kwa usalama. Kwa kujitunza kabla na wakati wa kujifungua na kufikiria mambo mbalimbali yanayohusiana na kujifungua, mwanamke atakuwa amefanya yote awezayo kuhakikisha mimba yake ni salama.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), linasema kila siku wanawake 800 hufa kwa matatizo ya mimba na uzazi yanayoweza kuzuilika. Asilimia 99 ya vifo vya kina mama wajawazito hutokea kwenye nchi zinazoendelea, nusu ya vifo hivi hutokea nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, Tanzania ikiwemo.

Hatari ya vifo vya kina mama wajawazito ni kubwa zaidi kwa mabinti walio na umri chini ya miaka 15 na matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua ndio chanzo kikubwa cha vifo hivyo.

Kwa mujibu wa WHO, mwaka 2013 wanawake 289,000 walikufa kwa matatizo ya mimba na uzazi.

Uwiano wa vifo vya kinamama wajawazito katika nchi zinazoendelea kwa mwaka 2013 ni vifo 230 kwa kila vizazi hai 100,000 wakati ni vifo 16 tu kwa kila vizazi hai 100,000 kwa nchi zilizoendelea.

Matatizo makubwa ya wakati wa ujauzito na kujifungua yanayobeba karibu asilimia 75 ya vifo vyote vya kina mama wajawazito ni kupanda kwa shinikizo la damu wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua (Kifafa cha mimba).

Uchunguzi unaonyesha kwamba mwanamke anapokuwa mjamzito magonjwa ya fizi yanaweza kusababisha kifafa, tatizo baya sana ambalo dalili zake ni pamoja na kupanda ghafla kwa shinikizo la damu, maumivu makali ya kichwa na kuvimba kwa mwili kwa sababu ya kuongezeka kwa maji.

Kifafa cha mimba kinaweza kumfanya mjamzito ajifungue kabla ya wakati unaofaa na mara nyingi watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wao viungo vyao havitokezi chembe nyekundu za damu.

Hali hiyo huchangia watoto hao kupungukiwa damu na kufa haraka na ndicho kisababishi kikuu cha vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua hasa katika nchi zinazoendelea.

Matatizo makubwa mengine ni pamoja na kutokwa damu (hasa baada ya kujifungua), maambukizi/magonjwa (hasa baada ya kujifungua), matatizo wakati wa kujifungua mfano mtoto kukaa vibaya tumboni na utoaji mimba usio salama.

Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayosababisha matatizo wakati wa kujifungua

Kutojitunza vizuri kwa mwanamke kipindi cha ujauzito.

Afya ya mama na mtoto aliyezaliwa vina uhusiano wa karibu sana. Akina mama wenye afya nzuri hujifungua watoto wenye afya nzuri.

Kukosa matibabu yanayofaa na yasiyohitaji vifaa tata.

Takwimu za WHO zinaonyesha karibu watoto milioni 3 hufa kila mwaka na watoto milioni 2.6 huzaliwa wakiwa wamekufa. Jarida la UN Chronicle linaripoti kwamba asilimia 66 ya watoto wanaokufa wanapozaliwa wangeweza kuzuiwa ikiwa akina mama na watoto hao wangepata matibabu yanayojulikana, yanayofaa na yasiyohitaji vifaa tata.

Kukosa huduma nzuri za afya kipindi cha ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.

Kulingana na jarida hilo, mwamamke asipopata huduma nzuri za afya anapokuwa mjamzito, anapojifungua na baada ya kujifungua, mtoto wake pia hatapata huduma za afya.

Itaendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles