24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Malengo ya kutokomeza Ukimwi 2030 yatafikiwa?

19480658_304

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya Ukimwi (UNAIDS), limeweka malengo ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Katika awamu ya kwanza, shirika hilo limeweka malengo ambayo yanatakiwa yawe yametekelezwa ifikapo mwaka 2020, ambayo yanajulikana kama 90 – 90 – 90.

Maana ya 90–90–90 ni kwamba asilimia 90 ya walioathirika na maambukizi ya VVU wajue hali zao kiafya, asilimia 90 ya watakaopimwa na kukutwa na VVU wapate dawa na asilimia 90 ya waliopo kwenye tiba wawe na kiwango kidogo cha virusi kwenye damu.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani, baada ya kutangazwa mkakati huo mwaka 2014, ilichukua hatua mbalimbali kuhakikisha inatimiza malengo yaliyowekwa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Uraghibishi na Habari wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Jumanne Isango, anasema wanatarajia kuwa watafikia malengo hayo kutokana na mikakati waliyojiwekea.

“Tunafuata maelekezo ya dunia na tayari mipango ipo na wadau wetu kama Marekani wameshaanzisha utaratibu wa kwenda sehemu ambazo zina maambukizi makubwa.

“Katika baadhi ya mikoa ambayo inaonekana kuwa na maambukizi makubwa kuna maeneo ambayo yametengwa na ambayo yatapata huduma zote muhimu.

“Tunakwenda katika maeneo ambayo yana mwingiliano mkubwa wa watu na ambayo tukiweka juhudi tutapata mafanikio makubwa.

“Tunahamasisha na kutengeneza uhitaji wa huduma za kupima na tunaimarisha miundombinu katika hospitali za kitaifa na zahanati ili papatikane dawa za ARV’s,” anasema Isango.

Anaitaja mikoa ambayo imeongezewa nguvu katika mapambano hayo ni Dar es Salaam, Mara, Simiyu, Tabora, Morogoro, Dodoma, Mbeya na Njombe.

“Tuna-invest (wekeza) mahali ambako patatoa matokeo makubwa. Mfano hapa Dar es Salaam utafiti unaonyesha watoto wengi wenye umri kati ya miaka 10 hadi 14 wanaishi mtaani na wengine wenye umri kati ya miaka 20 hadi 24 wana wenza ambao wanawazidi umri, kwahiyo hapa ni lazima tuongeze nguvu kwa sababu ni kundi ambalo ni rahisi kuathiriwa na ugonjwa huu,” anasema.

Kulingana na mkurugenzi huyo, Mkoa wa Mara umepewa kipaumbele katika mapambano hayo, hasa kutokana na tafiti kuonyesha kuwa watoto wengi huolewa chini ya miaka 15, wakati Simiyu watoto huolewa na watu wenye umri mkubwa, huku pia kukiwa na elimu ndogo juu ya kujikinga na VVU.

Anasema kwa Mkoa wa Morogoro watoto wengi wa kike wanaolewa au kuzaa chini ya miaka 15 wakati Njombe na Mbeya kumeonekana kuwa na maambukizi makubwa.

Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa TACAIDS, Richard Ngilwa, anasema wameandaa mwongozo wa uwekezaji kwenye Ukimwi, ambao pamoja na mambo mengine utaisaidia Serikali kufanya uamuzi wa uwekezaji katika shughuli za Ukimwi na hasa kutenga fedha kwa maeneo yenye tija.

Kwa mujibu wa Ngilwa, miongoni mwa mambo yanayopendekezwa katika mwongozo huo, ni wanafunzi waruhusiwe kupima shuleni na umri wa kuanza kupima ushushwe hadi miaka 15.

Awali mtoto chini ya miaka 18 alikuwa haruhusiwi kupima VVU bila idhini ya wazazi wake.

Hata hivyo, anasema utekelezwaji wa mwongozo huo utaanza baada ya kufanyika tathmini ya mkakati wa kudhibiti Ukimwi wa 2013/14 hadi 2017/18 mwanzoni mwa mwaka ujao.

HALI HALISI YA VVU, UKIMWI KATIKA UPIMAJI NA UNYWAJI DAWA

Kiwango cha maambukizi kwa Dar es Salaam ni asilimia 6.9 wakati kitaifa ni asilimia 5.1, na mkoa huo unatakiwa ufikie asilimia 80 ya malengo yote matatu (90 – 90 – 90) ifikapo mwakani.

Katika Wilaya ya Ilala ambako kiwango cha maambukizi ni asilimia 7.1, katika mkakati wa 90 – 90 – 90 wamefikia asilimia 60, Temeke asilimia 49 na Kinondoni asilimia 36.

Katika kipengele cha upimaji, Ilala wanatakiwa wapime watu 138,346 kwa mwaka, lakini hadi kufikia Oktoba mwaka huu, ilikuwa imepima watu 10,988.

Kwa kipengele cha dawa, malengo ni kutoa dawa kwa watu 20,407 lakini hadi kufikia Oktoba wilaya hiyo ilikuwa imetoa kwa watu 1,701.

“Kwa watoto wenye umri chini ya miaka 15, tumepima 32 kati ya 327. Juhudi nyingi tunazielekeza katika kundi hili ili kufikia malengo tuliyopewa,” anasema Mratibu Msaidizi wa Kudhibiti Ukimwi, Manispaa ya Ilala, Dk. Brenda Simba.

Mratibu huyo anasema pia zaidi ya asilimia 75 ya watu watakaopimwa na kukutwa na maambukizi wanatakiwa kufika kliniki kupata huduma endelevu, lakini kati ya watu 40,741 walioandikishwa katika manispaa hiyo, wanaofika kliniki ni 34,910.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Victorina Ludovick, anasema kwa takwimu ambazo wanazo  wanaona maambukizi yanapanda, hivyo wanatoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhari na kuendelea kujilinda kwa sababu Ukimwi bado upo.

“Tunawahamasisha watoa huduma waweze kujua 90 – 90 – 90 na lengo la kutokomeza Ukimwi ifikapo 2030 na utafiti wa nyumba kwa nyumba unaendelea,” anasema.

TABORA, KATAVI, RUKWA

Tabora, Katavi na Rukwa ni miongoni mwa mikoa 10 inayoongoza kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2011/2012.

Katika Mkoa wa Tabora ambako maambukizi ya Ukimwi ni asilimia 5.1, wilaya za Igunga (5.8%) na Nzega (5.1%) zinatajwa kuwa vinara wa maambukizi hayo mkoani humo, hivyo mkoa una mkakati wa kupima watu zaidi ya 10,000.

Taasisi ya Mkapa Foundation kwa kushirikiana na Shirika la Save the Children na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukimwi, wameanza kutoa mafunzo ya kuhakikisha wananchi wanaepuka maambukizi mapya.

Mratibu wa Ukimwi na Kifua Kikuu, Dk. Happines Wilbroad, anasema sababu zilizotajwa kuendelea kuchangia kukua kwa maambukizi katika mikoa hiyo ni pamoja na ndoa za utotoni, tohara za jadi, kukithiri kwa imani potofu za kishirikina na wananchi kutozingatia elimu juu ya kujikinga na Ukimwi.

“Mkoa unaoongoza kwa maambukizi ya VVU kati ya mikoa hii mitatu ni Rukwa wenye asilimia 6.2 ukifuatiwa na Katavi wenye asilimia 5.2 na Tabora asilimia 5.1. Takwimu za maambukizi zipo juu ukilinganisha na zile za kitaifa, hivyo jitihada mbalimbali zinahitajika kunusuru maisha ya wakazi wa maeneo hayo,” anasema Dk. Wilbroad.

Sheikh wa Mtaa wa Nzega Mjini, Mussa Kassim, ambaye ni miongoni mwa viongozi wa dini waliopata mafunzo hayo, anasema watayatumia sambamba na maagizo ya imani zao za kidini, kukemea jamii dhidi ya matendo maovu.

Mchungaji wa Kanisa la AICT Nzega Mjini, Isaya lyaka, anawaasa wanandoa kuendelea kuwa waaminifu kama mafundisho ya dini yanavyoasa na kwa wale ambao bado hawajafunga ndoa anasema kuwa wanapaswa kusubiri.

Mratibu wa Ukimwi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Kasara Bulemo, anasema wamejipanga kufika kwenye kata zote 16 za halmashauri hiyo ili kutoa elimu ya kupima maambukizi ya VVU kwa hiari.

Anasema maambukizi ya VVU katika Mkoa wa Katavi ni asilimia 5.9 na maeneo yalioathirika zaidi katika Halmashauri ya Mpanda ni yale ya mikusanyiko ya watu wengi, hasa wakati wa msimu wa mavuno.

Anayataja maeneo yaliyoathirika zaidi na maambukizi ya VVU katika halmashauri hiyo ni Karema, Ikola, Mnyagala na Kasekese.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles