31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Namna tunavyoweza kukabiliana na changamoto mpya za kimalezi

Wazazi
Wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao

Na Christian Bwaya,

 KAMA kuna wakati tumeshuhudia upatikanaji wa maarifa na utaalamu mwingi kuhusu malezi ya watoto, ni sasa. Suala la malezi limekuwa likipewa uzito mkubwa kuliko ilivyowahi kuwa katika kipindi cha nyuma.

Sambamba na ongezeko la mijadala ya malezi katika majukwaa mbalimbali, eneo la malezi limevutia hisia za watafiti wengi kuliko ilivyopata kuwa. Kila siku, kwa mfano, zinachapishwa tafiti nyingi kujadili masuala yanayohusu malezi ya watoto.

Jambo hili linaweza kumtia wasiwasi mfuatiliaji makini wa mambo. Kwamba iweje kuwepo msisitizo huu mkubwa katika malezi? Iweje wazazi wetu ambao ‘hawakufundishwa’ namna ya kulea waliweza kutulea vizuri? Kwa nini sasa hivi pamoja na kuwepo kwa kila namna ya maarifa ya kimalezi kwa wazazi wa kisasa bado changamoto za kimalezi zimeendelea kuongezeka kuliko ilivyokuwa hapo zamani?

Jibu la swali haliwezi kuwa jepesi. Hata hivyo, kuna ukweli kuwa mfumo wa maisha tunayoishi katika siku za leo unaathiri kwa kiasi kikubwa namna tunavyolea watoto wetu. Kwa mfano, hii leo ni jambo la kawaida kwa wazazi kutumia muda mrefu mbali na familia zao. Kazi zinachukua muda mrefu wa wazazi kuliko ilivyopata kuwa hapo zamani.

Wakati zamani katika familia nyingi za kawaida baba na mama waliishi sehemu moja, siku za leo mambo yamebadilika. Huwezi kushangaa kwa mfano, kusikia mume anaishi Mwanza, wakati mama anafanya kazi mkoa wa Lindi.

Katika mazingira haya, wazazi hawa wanaweza kukutana kwa nadra na hata kuchukua miezi kadhaa kabla mzazi mmoja hajapata muda wa kwenda kusalimia familia yake inayoishi mbali nae. Jambo hili halikuwahi kuwa sehemu ya maisha katika siku za nyuma.

Kadhalika katika familia nyingi za kawaida mama alitarajiwa kuwa nyumbani muda mwingi kulea watoto. Wanawake wengi kwa kawaida, hawakuwa na kazi zingine zaidi ya kuwatunza watoto. Kazi ya kutafuta mkate wa familia ilikuwa ya wanaume. Watoto walilelewa kwa karibu sana na mama tangu wakiwa wadogo mpaka walipofikia umri wa kuondoka nyumbani na kujitegemea.

Mambo yamebadilika hii leo. Akina mama wameondoka nyumbani kuungana na wanaume kuongeza kipato cha familia. Dhana kuwa mwanamke ni mama wa nyumbani inafutika. Si wanawake wengi wanaweza kuwa tayari kuwa ‘mama wa nyumbani’ kulea watoto kama ilivyopata kuwa katika siku za nyuma.

Mwanamke kufanya kazi, kwa hakika si jambo baya. Jitihada za kubadili mitazamo ya wanajamii ili waweze kuwasomesha watoto wa kike zinaenda sambamba na fursa ya kiajira sawa na mwanaume. Ndio kusema, kama mwanamume anaweza kuajiriwa, haileti maana kufikiri kuwa mwanamke anapaswa kubaki nyumbani kufanya kazi za ndani kama ilivyokuwa imezoeleka hapo zamani.

Katika ajira wanawake wameonesha uwezo wa kumudu majukumu yao sawa na wanaume. Karibu kila sekta hivi sasa wapo akina mama. Wanawake wanaonesha uwezo mkubwa, wanashika madaraka makubwa kazini na wanafanya vyema tena mara nyingine kuliko wanaume.

Hata hivyo, mafanikio haya ya akina mama kikazi yametikisa maeneo mengineyo ya kijamii. Malezi ni eneo mojawapo kubwa lililokumbwa na tetemeko kubwa tangu akina mama walipoanza kuondoka nyumbani kuelekea makazini. Kuanzia juma lijalo tutajadili changamoto hizo katika safu hii na kujaribu kuangalia kile kinachoweza kufanyika.

Itaendelea

Blogu: http://bwaya.blogspot.com , Simu: 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles