JOTO la Uchaguzi Mkuu wa Urais limeanza kupanda nchini Kenya kuelekea siku ya uamuzi Agosti 8 mwaka huu.
Viongozi wa miungano miwili mikuu ya vyama wametawanyika kote nchini humo hasa katika ngome zao wakiwahimiza wafuasi wao kujiandikisha kwa wingi katika daftari la wapiga kura.
Harakati hizo zinakuja baada ya kuzaliwa upya kwa miungano hiyo, kuanzia ule unaotawala wa Jubilee unaojumuisha vyama vya National Alliance (TNA) kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, United Republican Party (URP) cha Naibu Rais William Ruto.
Kingine ni United Democratic Front (UDF) na vyama vingine vidogo, ambapo vilijivunja na kuunda Chama cha Muungano wa Jubilee (JAP) chini ya kauli mbiu yao ‘tuko pamoja.’
Wakati JAP ikizinduliwa Septemba 2016, mpinzani wake Muungano wa Mageuzi na Demokrasia (CORD) nao ukaunda umoja mpya; National Super Alliance (Nasa) mapema mwezi huu.
Ushirika huo unajumuisha vyama wanachama wa CORD; Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, Wiper Democratic Movement cha aliyekuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka.
Kingine ni Forum for the Restoration of Democracy (Ford)-Kenya cha Moses Wetang’ula – na Amani National Congress (ANC) cha Makamu Rais wa zamani Musalia Mudavadi.
Lakini mshtuko ulikuwa uwepo wa Katibu Mkuu wa kilichokuwa chama tawala tangu uhuru Kenya African Union (KANU), Nick Salat.
Uwepo wa Salat ulichukuliwa kuwa chama hicho kimejiunga na upinzani, hali ambayo iliwafanya baadhi ya maofisa wake kukana hilo.
KANU ikalazimika kuitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama hicho (NEC), ambayo ilimpa Mwenyekiti wake, Seneta wa Baringo, Gideon Moi kuangalia umoja upi baina ya hiyo miwili ijiunge nao na kuwasilisha ripoti ndani ya wiki mbili.
Hakika kila msimu wa uchaguzi nchini Kenya huja na muungano mpya mkubwa, (kuanzia ule wa NARC ulioing’oa KANU na kumwingiza Rais Mwai Kibaki madarakani mwaka 2002) pamoja na ahadi ya mabadiliko.
Licha ya kuwa lengo kuu kisiasa ni kuunganisha nguvu ili kurahisha ushindi, moja ya faida, ambazo wanasiasa hupenda kuziimba kuhusu miungano hii ni kwamba inajenga umoja na mshikamano kwa maslahi ya taifa na hivyo kuondoa harufu ya ukabila,
Bahati mbaya, ushahidi huonesha wazi ikiwamo kupitia kauli za wanasiasa, ukabila bado ni karata muhimu kufanikisha ushindi kuliko chochote kile.
Utafiti uliowahi kufanywa na Michael Bratton na Mwangi Kimenyi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Michigan na Chuo Kikuu cha Connecticut mwaka 2008 ulionesha: “Ijapokuwa Wakenya wanapinga kujipambanua kwa misingi ya ukabila, vitendo vyao wakati wa kupiga kura kuchagua huwa havifichi rangi yao halisi.
Kenyatta, mtoto wa Rais wa kwanza Jomo Kenyatta, anadhibiti kura za kabila kubwa la Kikuyu na ameahidi kuziunganisha na Ruto anayetokea kabila lingine kubwa la Kalenjin kwa ajili ya JAP yao.
Kama shukrani, Kenyatta ameahidi kuzitoa kura za Kikuyu kwa Ruto wakati atakapowania Urais mwaka 2022.
Kwa upande wa upinzani, Odinga ameihakikishia NASA kura za Waluo, wakati Mudavadi akileta zile za Waluhya, jamii ambayo amejitangaza kuwa msemaji wake ile Desemba 31 mwaka jana, msimamo unaopingwa na Wetang’ula, ambaye pia anautaka urais.
Musyoka ana kura kutoka jamii yake ya Wakamba.
Licha ya viongozi wa JAP na NASA wakati wa uzinduzi wa miungano hiyo kuonesha kulenga kuzika chembe za ukabila, kauli wanazozitoa katika mikutano ya kisiasa ni kinyume.
Jamuari 10 mwaka huu kwa mfano, Ruto aliwasihi Wakalenjin: “Mna hisa katika Serikali ya Jubilee. Hakuna chama mbadala kwa ajili yenu. Mnatakiwa mhimize wafuasi wote kumpigia kura Rais Kenyatta. Tunahitaji fadhila za kisiasa mwaka 2022 wakati Rais Kenyatta atakapomaliza muhula wake wa urais.
“Mwaka huo, hakuna namna nyingine itakayonifanya nipate kura kutoka jamii nyingine ikiwamo za katikati ya Kenya (Wakikuyu) iwapo hatutaunganisha kura zetu kwa ajili ya Kenyatta.
“Sisi sote hapa si Wakenya, bali Wakalenjin, wakati jamii nyingine ni Wakikuyu.”
Mfano huo mdogo kati ya mingi iko pia kwa upande wa NASA, ambao hatima yake iko hati hati iwapo mgombea hatatoka jamii ya Waluhya iliyoapa lazima mgombea urais atoke kwao.
Wanasiasa na wazee wa kabila hilo wanalalamika kusaidia makabila mengine kutoa rais, ilhali wao hawapewi fursa na hivyo safari hii wameapa kutokubali.
Hilo limeshuhudia pia juhudi za kuwaunganisha wanasiasa waandamizi Mudavadi na Wetangula ili kuepusha kuzigawa kura za jamii yao hiyo.