Aveline Kitomary, Dar es Salaam
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa rai kwa viongozi wa dini nchini kuhakikisha wanaepuka misongamano kwenye nyumba za ibada hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.
Waziri Ummy amewaomba viongozi hao kuhakikisha waumini wenye dalili za kikohozi, mafua na homa wanabaki nyumbani.
Skizungumza na waandishi wahabari jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Aprili 9, wakati wa kikao cha kitaifa cha viongozi wa dini kilichozungumzia jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.
“Ni mategemeo yetu viongozi wa dini kuepuka mikusanyiko ya watu wengi, tunategemea kupata ushirikiano wenu kuhakikisha kuwa ibada zinaendeshwa katika mazingira ambayo si hatarishi, rais ameeleza kuwa serikali haitafunga nyumba za ibada lakini ni wajibu wetu kuangalia sasa tutafanya ibada kwa namna ambayo si hatarishi kwetu na kwa waumini.
“Kingine tunachoomba ni kuwepo utaratibu wa kupunguza waumini wakati wa kutoka na kuingia katika nyumba za ibada, kuwa na ibada fupifupi zinazofanyika mara kwa mara, kufanya usafi wa mara kwa mara kwenye nyumba za ibada na utakasishaji,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, amewataka viongozi hao wa dini kutumia tekonojia katika mikutano yao ili kukwepa mikusanyiko.